Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waamuzi vinara wa kadi nyekundu

Kayoko Pic Data Mwamuzi Ramadhan Kayoko

Fri, 17 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Huenda msimu huu kadi nyekundu zikaongezeka zaidi, kuliko uliopita ambapo hadi Ligi Kuu Bara ilipomalizika zilikuwa kadi 24 tu.

Msimu huu hadi sasa zikiwa zimebaki mechi nane kwa kila timu kabla ya ligi kumalizika, kadi 23 zimeshatolewa, huku Polisi Tanzania inayoburuza mkiani kwenye msimamo wa ligi ikioongoza baada ya kuvuna kadi tano, ikifuatiwa na Mtibwa Sugar yenye nne.

Mwamuzi Ramadhan Kayoko wa Dar es Salaam ndiye kinara wa kulima wachezaji umeme akiwa ameshatoa kadi nne nyekundu sawa na Jonesia Rukyaa wa Bukoba wakati Ester Adalbert anafuatia akiwa ametoa kadi tatu na Tatu Malogo akiwa ametoa mbili.

Beki wa Polisi Tanzania, Mohammed Mmanga ndiye kinara wa kupata kadi nyingi nyekundu akiwa amepata mara mbili hadi sasa msimu huu.

Kadi 18 zimetolewa kipindi cha pili na tano tu zimetolewa kipindi cha kwanza huku kuanzia dakika ya 70 hadi 90 ukiwa ndio muda hatari zaidi kwa wachezaji kupata kadi nyekundu kwani muda huo umezalisha kadi 12.

MOHAMED MMANGA - POLISI TANZANIA

Beki huyu wa Polisi Tanzania ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kupata kadi nyekundu msimu huu baada ya kuonyeshwa katika mchezo dhidi ya Yanga uliofanyika Agosti 16 mwaka jana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.

Kayoko alimpa Mmanga kadi hiyo dakika ya 87 baada ya kumkwatua Heritier Makambo wakati akieleeka eneo la hatari.

COLLINS OPARE - DODOMA JIJI

Mshambuliaji huyu alionyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi, Hans Mabena dakika ya 84 kwa kumchezezea rafu James Msuva katika mchezo dhidi ya Singida Big Stars uliofanyika Septemba 11 mwaka jana Uwanja wa Liti Singida.

EMMANUEL ASANTE - NAMUNGO

Alionyeshwa kadi nyekundu na Ester dakika ya 79 baada ya kumsukuma Samson Joseph wa Ruvu Shooting katika mchezo baina yao uliofanyika Septemba 11 mwaka jana Uwanja wa Majaliwa Ruangwa. Asante alipewa kadi hiyo baada ya kupewa kadi ya pili ya njano.

RODGERS KOLA - AZAM FC

Mshambuliaji huyu wa Azam raia wa Zambia aliingia uwanjania dakika ya 86 na dakika saba baadaye akaonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na Kayoko kwa kumfanyia madhambi kipa wa Mbeya City Haroun Mandanda katika mchezo uliofanyika Septemba 13 mwaka jana kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

JAMAL MASENGA - PRISONS

Mwamuzi Ahmed Arajiga wa Manyara alimuonyesha kadi nyekundu kiungo huyu wa Prisons dakika ya 90+1 baada ya kumwatua mshambuliaji wa Simba Moses Phiri. Alipewa kadi hiyo baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano katika mchezo huo uliofanyika Septemba 14 mwaka jana kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

MOHAMED MMANGA - POLISI TANZANIA

Ni Mmanga tena baada ya beki huyu wa Polisi Tanzania kupewa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting uliofanyika Septemba 19 mwaka jana kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Hiyo ilikuwa kadi ya pili nyekundu kwa mchezaji huyo msimu huu akiwa ameonyeshwa dakika ya 61 na Jonesia baada ya kumvuta mkono Samson Joseph wakati akielekea eneo la hatari.

DAVID KAMETA - MTIBWA SUGAR

Beki huyu alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 87 na mwamuzi, Ester Adalbert baada ya kumpiga kiwiko Hassan Nassor Maulid wa Mtibwa Sugar katika mchezo baina ya timu hizo uliofanyika Oktoba 2, 2022 kwenye uwanja wa Manungu Turiani.

ADEYUM SALEH - GEITA GOLD

Dakika ya 78, beki Adeyum Salehe wa Geita Gold alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na mwamuzi, Joackim Akamba baada ya kumuangusha Blanchard Ngabonzinza wa Polisi Tanzania katika mchezo uliofanyika Oktoba 4 mwaka jana kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.

PASCAL KITENGE - MTIBWA SUGAR

Kiungo huyu alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 41 na mwamuzi, Tatu Malogo baada ya kumkanyaga tumboni winga wa Simba, Pape Sakho katika mchezo baina ya timu hizo uliofanyika Oktoba 30 mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.

CASSIAN PONERA - MTIBWA SUGAR

Dakika ya 67, Ponera alimvuta jezi Augustine Okra wa Simba na mwamuzi, Tatu Malogo kumuonyesha kadi ya pili ya njano kisha nyekundu kwani awali dakika ya 40 alishaonyeshwa kadi ya kwanza ya njano kwa kumfanyia madhambi Phiri mchezo kati ya Simba na Mtibwa Oktoba 30 mwaka jana.

JUMA NYOSSO - IHEFU

Beki huyu wa zamani wa Ashanti, Simba na Kagera Sugar, alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na Mwamuzi, Hery Sasii dakika ya 42 kwa kunyanyua mguu na kumpiga teke la mgongoni Kipre Junior wa Azam katika mchezo uliofanyika Oktoba 31 mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

BENEDICT HAULE - SINGIDA BIG STARS

Alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 58 na mwamuzi, Thabit Maniamba baada ya kumkwatua Iddi Kipagwile nje kidogo ya eneo la hatari katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania uliofanyika Novemba 6, 2022 kwenye Uwanja wa Black Rhino, Karatu Arusha.

ABDUL OMARY - NAMUNGO

Dakika ya 75 alipewa kadi ya njano ya pili na nyekundu kwa kumkwatua Reliants Lusajo katika mchezo dhidi ya Azam uliofanyika Novemba 20 mwaka jana kwenye Uwanja wa Majaliwa Ruangwa Lindi.

SADIO KANOUTE - SIMBA

Mwamuzi Jonesia Rukyaa alimuonyesha Kanoute kadi nyekundu dakika ya dakika 90+4 baada ya kumfanyia madhambi mchezaji mmoja wa Coastal Union Desemba 3 mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Chanzo: Mwanaspoti