Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waamuzi tatizo ni rushwa, wanabeti ama mchezo unaenda kasi zaidi yao?

FEDHA Waamuzi tatizo ni rushwa, wanabeti ama mchezo unaenda kasi zaidi yao?

Fri, 12 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mjadala mkubwa uliotawala kila kona ikiwamo kwenye mitandano ya kijamii kuanzia juzi ni utata uliozunguka kona iliyozaa bao la kusawazisha la Simba dhidi ya Singida Fountain Gate lililofungwa katika dakika ya 90+8 ya mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Kamati ya Waamuzi ya Zanzibar ikamuonya mwamuzi Nasri Salum 'Msomali' kwa "makosa ya kibinadamu ya kuipa Simba shambulizi la kona" ambayo haikustahili, ikiwa ni siku moja tu tangu kuwafungia waamuzi wengine wawili kwa kushindwa kutafsiri sheria za soka.

Hoja nzito na maswali kuhusu uamuzi tata wa waamuzi vinaegemea katika mambo kadhaa yakiwamo tuhuma za rushwa, waamuzi kujihusisha na michezo ya kubashiri matokeo (betting), mapenzi binafsi kwa baadhi ya timu ama wanazidiwa kasi na soka la kisasa ambalo matukio mengi hutokea kwa haraka sana?

RUSHWA

Tuhuma za rushwa zimekuwa zikitajwa kama anguko kuu la waamuzi katika nchi nyingi duniani kote. Ushawishi wa kifedha na mali umekuwa ukifanywa na klabu nyingi duniani na jambo hilo limetajwa kuwaweka katika wakati mgumu waamuzi ambao wakati mwingine mazingira yao ya kazi hayaridhishi yakiwamo malipo ya mishahara ama posho zao.

Katika ligi zilizoendelea, waamuzi wamekuwa wakilipwa mishahara ya kila mwezi/ wiki nje ya posho za kuchezesha mechi.

Kwa nchi za kimasikini, waamuzi wamekuwa wakikopwa hata kupata nauli ya kuwafikisha katika kituo cha kuchezesha mechi, pesa ya malazi na hata chakula. Hii inawaweka katika wakati mgumu kukabiliana na ushawishi wa vibunda vya pesa na zawadi nono kutoka kwa watu wa klabu tajiri.

Lakini pia tamaa ya kupata manufaa ya haraka ni kati ya vinavyowaangusha baadhi ya waamuzi.

WAZEE WA MIKEKA

Katika soka la dunia, kumekuwapo na ushawishi wa kampuni za kubeti ambazo hutoa pesa na kupanga matokeo kwa kuwahusisha waamuzi kwa kuwatengea fungu la pesa. Aina fulani ya matokeo inaweza kuzinufaisha kampuni za kubeti.

Waamuzi wasio waadilifu pia wanaweza kujihusisha ni michezo ya kubeti kwa kuhakikisha aina fulani ya matokeo inapatikana ili kuwawezesha wao ama watu wao wa karibu kupiga pesa kutokana na walichobashiri katika 'mikeka' yao.

MAPENZI BINAFSI

Waamuzi wasio waadilifu, wanaweza kutoa uamuzi wa utata kutokana na mapenzi binafsi ya timu bila hata ya kuonwa na vigogo wa timu fulani. Mapenzi ya soka ni kitu kinachokuja tu ama kwa sababu fulani tangu utotoni, kwa walio wengi. Ni ngumu sana kwa mtu wa mpira kutokuwa na timu anayoipenda. Mtu hadi kufikia hatua ya kuwa mwamuzi ni kwamba alipenda soka tangu akiwa kijana na bila ya shaka alikuwa na timu anayoishabikia. Hii inaweza kuwa chanzo cha mwamuzi asiye mwadilifu kutoa upendeleo fulani ili kuibeba timu yake.

KASI YA MCHEZO

Soka la sasa limekuwa ni la kasi sana. Wachezaji wanaoitwa wana 'mwendo balaa' wamekuwa na thamani zaidi ya wale ambao wanaitwa 'wakimbia kama konokono' uwanjani. Hii hali ya imefanya mchezo mzima kutawaliwa na kasi. Ni lazima waamuzi pia wawe na pumzi zaidi, spidi zaidi na wawe fiti zaidi ya ilivyokuwa zamani. Hitaji hili linawafanya waamuzi wakati mwingine kutoona matukio kwa ukaribu unaotakiwa wa angalau mita 15 na katika engo ya mshazari (diagonal).

Spidi ya mchezo ya panda shuka, kwa mwamuzi ambaye hayuko fiti na katika mazingira ya joto na jua kali vinaweza kumfanya awe mwenye kujisikia kizunguzungu na kushindwa kuona tukio kwa ukaribu na usahihi. Kiujumla kuliona kila tukio kwa usahihi na ukaribu huku unakimbia spidi kali sio jambo rahisi kulimudu kwa dakika zote 90.

WASIKIE MAKOCHA, MAGWIJI WA SOKA

Akizungumzia sakata la waamuzi, mwamuzi wa zamani Othman Kazi alikerwa na kitendo cha baadhi mashabiki kuwashambulia bila ya kujua sheria, huku akiweka wazi hakuna shinikizo lolote linalopo isipokuwa wanaolalamika hawaulizi ili kujifunza.

"Nakasirika sana kuona waamuzi wanashambuliwa kila siku kwa sababu hao wanaoongea sana kwa kiasi kikubwa hawajui sheria ilivyo, sasa mimi nashangaa watu wa aina hii wanapata wapi huu ujasiri wa kukosoa kitu wasichokijua?" Alihoji Kazi na kuongeza;

"Watu wanasema Simba ilibebwa dhidi ya Singida Fountain Gate, lakini swali jepesi la kujiuliza, kama mwamuzi alitaka iwe hivyo kwanini asiwape penalti iliyosababishwa na Abdulmajid Mangalo aliyedaka mpira eneo la hatari, au ya Moses Phiri aliyeangushwa pia? Watu watambue kwanza sheria kabla ya kuanza kulalamika kwa sababu naona hoja zao hazina mashiko."

Kocha wa zamani wa timu za Yanga na Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa anasema suala la waamuzi nchini limekuwa na changamoto kubwa huku akieleza sababu anayoiona ni kuendekeza ushabiki, shinikizo au rushwa japo ni ngumu kuthibitisha.

"Mwamuzi ana wasaidizi wake sasa anapoona hajaelewa ni lazima aulize kwanza kabla ya kufanya uamuzi, mara nyingi sana tumeona hayo yakitokea pindi timu zinazopambana ili zisishuke daraja ingawa ni vigumu kuthibitisha suala hilo," anasema.

Winga Simba wa zamani, Dua Saidi alisema, shida ipo hasa kwenye upeo mdogo wa waamuzi kufikiria ukilinganisha na wakati waliokuwa wanacheza wao, lakini aliongeza kuwa hata wao ni binadamu wanakosea.

Alisema kuwa hata wachezaji wenyewe ni chanzo cha makosa ambayo marefa wanatupiwa kesi, ila kwa kutokujua sheria au kwa makusudi wanafanya mambo mengi yanayoathiri michezo mingi.

"Hakuna kinachoamuliwa na mwamuzi kama wote hawajakubaliana hadi wale wa pembeni nao wanaungana, hivyo hakuna haja ya wao kumdondoshea lawama mtu mmoja tu kwa sababu hayuko pekee yake.

"Kosa la mchezo wa Singida na Simba watu wanamsema mwamuzi kumbe shida ni wachezaji mfano, wakati Saido Ntibazonkiza anataka kupiga shuti Kelvin Kijili alizuiua na kipa akawahi akaudaka nje na kupelekea kona."

Boniphace Pawasa, mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, anasema kuna umuhimu mkubwa wa kupunguza ushabiki na kujua sheria kwani mwamuzi anachokiangalia ni saa yake ambayo kama kutatokea chochote kitakachosimamisha mchezo naye anasimamisha muda na lazima ataufidia ndio maana watu wanaenda tofauti na yeye.

Alisema wakati mwingine kosa linatokea nyuma yake na yeye kushindwa kuliona, lakini pia wawe wanatakiwa kupata mafunzo ya mara kwa mara mwanzoni na mwishoni mwa msimu ili kuwafanya wawe sawa zaidi.

"Malipo yao pia yawe mazuri ili kuwaepusha na vishawishi ambavyo wengi wanavipitia kwani nao ni wanadamu lakini changamoto nyingine ni mashabiki kutokujua sheria 17 za mpira wa miguu.

"Mwamuzi anatakiwa kutoa uamuzi ndani ya sekunde tatu, kama kutakuwa na kosa na wakati huo huo anakimbia na kutakiwa kuangalia yanayoendelea, sio rahisi. Lakini kama wakipata mafunzo na mazoezi, itapunguza lawama. Pia wachezaji wajielewe kuwa wanatakiwa kucheza na sio kujiangusha wanajipotezea muda," alisema Pawasa.

CHANZO CHA YOTE

Kamati ya Waamuzi ya Zanzibar jana ilitangaza kumpa onyo mwamuzi Nasri Salum 'Msomali' kwa kuipa Simba shambulizi la kona kimakosa, jambo ambalo liliwapa Wekundu wa Msimbazi nafasi ya kusawazisha bao katika dakika ya mwisho na kisha kwenda kushinda kwa penalti 3-2 zilizowapeleka fainali, ambayo kesho watawavaa mabingwa watetezi Mlandege kwenye uwanja huo huo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Waziri Shekha alisema baada ya kikao kilichofanyika jana (juzi) kupitia ufanisi uliofanywa na Msomali na wasaidizi wake waligundua kwamba mwamuzi huyo hakuwa sahihi kwenye uamuzi wake huo wa kuipa kona Simba katika mechi hiyo ya nusu fainali lakini akasisitiza kwamba kosa hilo ni la kibinadamu "kwani waamuzi nao hufanya makosa ambapo wamebaini ndio kosa pekee alilofanya Msomali kwenye mchezo huo wa juzi usiku".

“Nilikwambia kwamba tutachunguza na tumekutana leo (jana) kikao ambacho kimemalizika dakika chache zilizopita, tumebaini kwamba kulikuwa na makosa kwa mwamuzi,” alisema Shekha ambaye ni mwamuzi mstaafu.

“Haikupaswa kuwa kona hakuna sehemu ambayo mpira uliochezwa na mchezaji wa Singida na kipa aliudakia nje hivyo haikuwa sahihi kuwa kona, haya ni makosa ya kibinadamu na ndio kosa pekee ambalo tumeliona baada ya kupitia ripoti na marudio, sehemu nyingine zote alikuwa sahihi.

“Tumeona hakuna sababu ya kumpa adhabu kubwa zaidi ya kumuonya kwasasa, kwanza mashindano haya yamebakiza mechi moja ya fainali lakini narudia hili ni kosa moja kati ya mazuri aliyoyafanya kwenye mchezo husika, tumemuonya na kumtaka awe makini asirudie makosa ya namna hii.”

Uamuzi wa refa Msomali uliibua hasira za wachezaji wa Singida. Kiungo Morice Chukwu aliyejiunga na walima alizeti hao msimu huu akitokea Rivers United ya Nigeria, alisema kuonewa katika soka hakuwezi kuisha lakini ile dhidi ya Simba ilivuka mpaka na akatuhumu: "Hapa hakuna timu nyingine zinazotakiwa kupata ushindi zaidi ya Simba na Yanga tu kwa nilivyoona."

Naye beki wa Singida, Hamad Wazir ‘Kuku’ ambaye ni mume wa muigizaji Esha Buheti, alidai kwamba mechi hiyo ni bora isingefanyika. “Kama walipanga Simba ndio iende fainali ni bora wangetuambia mapema tusije uwanjani,” alisema kwa hasira.

Onyo kwa Msomali, limetolewa siku moja tu baada ya kamati hiyo kuwafungia waamuzi wawili wasaidizi Yusuf Shombe Issa na Mohamed Mwadini kwa kuruhusu jumla ya mabao matatu yasiyosahihi katika mechi mbili tofauti.

Kocha Msaidizi wa APR FC, Aime Ndizeye alionyesha kutoridhishwa na uamuzi wa waamuzi wa mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya Mlandege FC ambao APR ilipoteza kwa penalti 4-2 baada ya mchezo huo kumalizika bila timu hizo kufungana.

Ndizeye wakati anazungumza na wanahabari baada ya mchezo huo, alisema: "Hii ni aibu. Waamuzi hawakuwa fair. Sisi ni mara yetu ya kwanza kushiriki lakini hawakuwa fair. Hatutakuja tena kwenye mashindano haya."

Chanzo: Mwanaspoti