Simba jana ilikuwa uwanjani katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku watani zao, Yanga wakitarajiwa kushuka leo, lakini wakimalizana na mechi hizo watakuwa na michezo migumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika wiki ijayo waliyopewa marefa pasua kichwa na wasiotabirika.
Simba ilicheza na Kagera Sugar, huku Yanga itavaana na Mtibwa Sugar kabla ya Jumanne Mnyama kuialika Wydad Casablanca ya Morocco na siku inayofuata Yanga itaikaribisha Medeama ya Ghana katika mechi za makundi na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetangaza waamuzi watakaozichezesha kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.
Wakati watani wakihitaji ushindi, Simba itakayoshuka uwanjani saa 10:00 jioni ilipoteza ugenini Marrakech mchezo uliopita, huku Yanga itakayocheza kuanzia saa 1:00 usiku ilitoka sare ya bao 1-1 mjini Kumasi, Ghana na zote zinaburuza mkia kwenye makundi.
Timu hizo zinatakiwa kushuka kwenye mechi hizo kwa tahadhari na nidhamu ya hali ya juu kutokana na rekodi za waamuzi waliopangwa kuchezesha.
Simba yenye pointi mbili kundi B itachezeshwa na Pierre Ghislain Atcho kutoka Gabon ambaye rekodi zinaonyesha amechezesha michezo 18 ya kimataifa na timu za nyumbani zilishinda tisa, sare nne na za ugenini zikishinda mara tano, huku akitoa jumla ya kadi za njano 77 na nyekundu moja.
Hesabu za Simba ni zilezile za kushinda mchezo ili pia kulipa kisasi kwani itafikisha pointi tano ikiiombea Jwaneng Galaxy ya Botswana itakayoifuata Asec Mimosas nchini Ivory Coast ipoteze ili ikae nafasi ya pili.
Simba ina kumbukumbu ya kuifunga Wydad kwa bao 1-0 kwa Mkapa lililofungwa na Jean Baleke kwenye robo fainali ya michuano hiyo msimu uliopita, Aprili 22.
Kwa Yanga imepangwa kuchezeshwa na mwamuzi Redouane Jiyed kutoka Morocco ambapo rekodi zinaonyesha ameshachezesha michezo 38 ya kimataifa huku wenyeji wakishinda 18, sare 12 na za ugenini zimeshinda minane.
Katika michezo aliyochezesha ametoa kadi za njano 169 na nyekundu 10 huku akikikumbukwa zaidi kuwahi kuchezesha mechi ya kirafiki kati ya PSG ya Ufaransa ilipoifunga Inter Milan ya Italia bao 1-0, Desemba 30, 2014.
Hii ni mara ya pili kwa Jiyed kuchezesha mchezo kati ya timu hizo kwani mwanzo ilikuwa Kombe la ShirikishoAfrika hatua ya makundi ambapo Medeama ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Yanga mjini Ghana Julai 26, 2016.