Mashabiki wa soka nchini bado wanaendelea kuijadili penalti iliyopewa Simba katika mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons na kuwapa ushindi wao wa kwanza baada ya kucheza dakika 339 bila ya bao wala ushindi.
Waamuzi maarufu nchini, wamemaliza utata kwa kuweka bayana kwamba, lile lilikuwa tuta preshi na hawaoni tatizo lolote. Simba ilipata ushindi huo wa nane katika Ligi ya msimu huu na kufikisha pointi 28 baada ya mechi 14 kwenye pambano kali lililopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini gumzo likiwa ni penalti ya dakika ya 69.
Penalti hiyo ilifungwa na Meddie Kagere aliyefikisha bao lake la tano msimu huu, na kuiacha Prisons mkiani, lakini gumzo ni jinsi mwamuzi Ahmad Simba alivyotoa adhabu hiyo na kufanya mashabiki waliokuwa uwanjani kupigwa na butwaa.
Baadhi ya waamuzi nchini wamemaliza sintofahamu kuhusu penalti hiyo ya Simba iliyokuwa ya sita msimu katika mechi zao 14, ikipata mbili ikiwamo hiyo ya juzi na nne zikapotezwa.
Mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania, Omary Abdulkadir alisema kwa mtizamo wake ile ilikuwa ni penalti halali kwa Simba.
“Sheria za mpira zinabadilika, kwa mimi ile ilikuwa ni penalti halali kwa Simba japo kila mwamuzi ana misimamo yake, ila kwangu ni penalti.”
Alisema sasa hakuna ‘ball in hand’ na kwa mjongeo wa namna penalti ya Simba ilitokea, huwezi kusema aliyeisababisha mikono yake ilikuwa mirefu au mifupi, lakini mpira ulimgusa mikono.
Naye Isihaka Shirikisho alisema japo aliangalia mechi hiyo kidogo, lakini amesikia malalamiko mengi juu ya penalti ile.
“Ili mwamuzi utoe penalti lazima ujiridhishe haswa kuwa hii ni penalti, naamini hata kwenye mechi ile ilikuwa hivyo.
“Ila binafsi nimeiangalia kidogo, lakini nimeona malalamiko mengi kuhusu penalti waliyopewa Simba,” alisema. Gumzo la Penalti hiyo limekuwa kubwa kwenye mitandao huku video za mechi hiyo zikisambaa kwa wingi.