Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waamuzi Ligi Kuu pasua kichwa, majanga kibao

Emmanuel Mwandembwa.jpeg Waamuzi Ligi Kuu pasua kichwa, majanga kibao

Tue, 2 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

“Mwamuzi Emmanuel Mwandembwa (Arusha) amefungiwa miezi (6) kufanya kazi ya uamuzi wa mpira  wa miguu kwa kosa la kushindwa kutafsiri vyema sheria 17 za mpira wa miguu jambo lililosababisha ashindwe kumudu mchezo tajwa hapo juu, adhabu hii kwa kuzingatia kanuni ya 42:1(1.1) ya ligi kuhusu udhibiti kwa waamuzi’.” Hizi ni hukumu zimekuwa mara kwa mara zikijitokeza kwenye taarifa ya kamati ya usimamizi wa ligi inayopitia ripoti mbalimbali za michezo ya Ligi Kuu Bara.

Hukumu hizi za waamuzi zimekuwa ni jambo la kawaida kujitokeza kwenye taarifa hizo zinazotokana na makosa mbalimbali ya waamuzi katika michezo ambayo wanaisimamia kuhakikisha sheria 17 za soka zinafuatwa kikamilifu na klabu zote.

Makosa ya waamuzi yamekuwa ni changamoto kwa klabu, wadau na hata mamlaka zenyewe zinazosimamia soka, licha ya kuwa na matamko mengi ya kutamani kuona  makosa yanapungua na adhabu hizi zinapungua.

Kufuatia hali hii gazeti hili likaamua kuingia msituni kusaka undani wa kinachosababisha makosa ya waamuzi kwa kuwahoji waamuzi wenyewe na wadau mbalimbali wa soka ambao wamefunguka mengi ambayo yanasababisha udhaifu wa taaluma hii muhimu kwenye soka.

Wengi ambao wametoa ushirikiano wameomba kufichwa majina yao wakihofia kuingia kwenye chuki na baadhi ya wale ambao wamekuwa wakitajwa kwenye changamoto za waamuzi kushindwa kusimama imara kusimamia usahihi wa taaluma yao.

MCHAKATO WA KUPATA WAAMUZI

Mwamuzi mmoja mstaafu anaeleza eneo la kwanza ambalo limekuwa likileta shida kwa waamuzi kuonekana hawakidhi viwango ni jinsi ambavyo waamuzi wamekuwa wakizalishwa hadi kufikia kusimamia michezo mikubwa ya Ligi Kuu.

“Chimbuko la kwanza kabisa ambalo mnatakiwa kujiuliza ni jinsi gani waamuzi hawa wamekuwa wakipatikana sisi zamani tulikuwa tunapatikana mashuleni, wanafuatwa walimu au wana taaluma wenginme hata kwenye mabenki kwa kuzingatia vigezo na baadaye wanaanza kufundishwa hii taaluma,” anaeleza mwamnuzi huyo wa zamani kutoka Jiji la Mwanza.

“Ukishamchukua mtu mwenye taaluma kama huyu kwanza anakuwa hana njaa kubwa sana na wakati huo mwamko wa rushwa haukuwa mkubwa kama ulivyo hivi sasa lakini kubwa hapa tulikuwa tunaangalia umakini wake na haanzi moja kwa moja juu huku ataanza kuchezesha mechi za madaraja ya chini huku akiwa anapanda taratibu kuja juu kulingana na ubora wake.

“Ndio maana mlikuwa mnaona mwamuzi akija huku juu anakuwa na umakini kuliko makosa, sio kwamba waamuzi wa zamani walikuwa hawafanyi makosa hapana yalikuwa ni yale makubwa sio kama sasa ambapo tunaona vitu vya ajabu mpaka unajiuliza huyu amefundishwa na nani mpaka amefika hapa.

“Kwa sasa unaona kabisa mambo yamekuwa tofauti waamuzi wanaotoka kwenye taasisi ni wachache sana, wengi ni wale ambao wanatoka mashuleni na wadogo ambao wamekuwa ni rahisi kupokea maelekezo tu na wengine wanabebana mpaka kufika huku juu, Ligi Kuu sasa unaona kijana mdogo kabisa unajiuliza huyu kakomaa kweli kuja kusimamia mechi kubwa kama hizi?”

Mwamuzi huyo anaeleza  wanaosaka waamuzi wamekuwa wakisita kuwafuata wana taaluma wakubwa wakihofia haitakuwa rahisi kwao kuwapa maelekezo ya wale wanaoharibu mpira ambao wamekuwa wakitumia udhaifu wa wamauzi wadogo kuwapa maelekezo.

“Huwa tunawauliza waamuzi hawa vijana wa sasa mnakuwaje mnashindwa kusimamia mechi kwasasa wanawataja wakubwa wao kwamba wamekuwa wanakuja na maelekezo na mashinikizo haya yanakuja kwao wakiwaambia hii ni oda kutoka juu sasa ukiangalia wao wanataka pesa wanajikuta wanaingia kwenye huo mtego, ni vigumu kwao kuwafuata wana taaluma kama madaktari, wanajeshi kwasasa wanajua kwamba haitakuwa rahisi kwao kuwapa maelekezo hayo.

“Hivi sasa chunguzeni mtajua kila mwamuzi mnayemuona  anachezesha mara kwa mara ujue huyo ana kiongozi wake kamshika mkono kwa hapa ndani na mwamuzi wa namna hiyo hata akivurunda atalindwa tu hatasumbuliwa kama wale wengine ambao watakuwa makini.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Nassoro Hamduni anaelezea namna mchakato ulivyo wa kuwapata waamuzi; “Waamuzi wote ni mali ya FRAT (Chama cha Waamuzi Tanzania) ndiyo wanaowazalisha, sisi tunaletewa pale kunapokuwa na mashindano, ikumbukwe sisi hatuna ligi huwa tunaenda kuwaombea kwa wenye mashindano ndiyo hutuambiwa wanataka waamuzi wangapi katika ligi ipi ama mashindano yapi.

“Lakini ukiona mwamuzi ama waamuzi baadhi wanachezesha mara kwa mara ni uwezo wa mwamuzi mwenyewe, huwezi kuchukua mwamuzi ambaye unaona uwezo wake ni mdogo, hii ni kama inavyokuwa kwenye timu ya mpira, mchezaji akifanya vizuri mazoezini ndiye anayecheza kwa wakati huo.

“Kuhusu mabadiliko ya waamuzi kwenye baadhi ya mechi inategemea na sababu kuu mbili, ratiba ya CAF wakati mwingine waamuzi huchaguliwa kuchezesha mechi za CAF huku tayari akiwa amepangwa kwenye ratiba ya ligi, hivyo lazima aondolewe maana kule ni kukubwa kuliko huku.

“Pia, wenye ligi yao wakiona tumepanga mwamuzi ambaye wanaona alichezesha vibaya baadhi ya mechi huwa wanatuomba tubadilishe kwani wanakuwa hawana imani naye, hivyo mabadiliko yanafanyika kutokana na mashauriano kama hayo.

“Wakati mwingine huwa tunaambiwa mwamuzi huyu aliyepangwa kwenye mechi hii ana ukaribu ama kuna kitu na upande mmoja, napo mabadiliko hufanyika, ingawa sisi viongozi huku juu wakati mwingine hatuwezi kujua kila kitu kinachoendelea kati ya waamuzi na mabosi wa timu.”

Naye mwamuzi wa zamani mwanamke, Elizabeth Kalinga katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, alielezea namna mabosi wa kamati wanavyobadilisha mwamuzi kwenye mechi kubwa hasa za Simba na Yanga.

“Nakumbuka iliwahi kunitokea nikiwa mwamuzi, nilipangwa kuchezesha mechi ya Simba na Yanga pale Shamba la Bibi (Uhuru), wakati huo Simba ilikuwa katika hali mbaya sana, ingefungwa na Yanga basi ingeshuka daraja. Nilikuja hadi Dar es Salaam nikitokea Mbeya lakini Simba iliiomba sana TFF ili nibadilishwe maana nilikuwa na misimamo yangu, kiukweli ingeshuka daraja maana walikuwa wabovu.

“Nilibadilishwa na kwenda kuchezesha mashindano ya Taifa Cup kule Shinyanga wakapewa mwamuzi mwingine ambaye nadhani aliwaokoa wasishuke daraja,” anasema Elizabeth

Katibu Mkuu wa FRAT, Kennedy Mapunda anaelezea juu ya hilo; “Tunafanya kozi mbalimbali za waamuzi, tukimaliza tunawapa Kamati ya Waamuzi ya TFF, maana wao ndio wanatambulika na FIFA sio sisi, hivyo hao wanakuwa na jukumu la kuwaongoza kazi yetu inakuwa imemalizika, ndio maana hata kwenye ratiba za mechi hupanga wao sio sisi, huku ni kuzalisha na sasa waamuzi wapo wengi.”

UHABA WA WAKUFUNZI

Aidha mwamuzi huyo aliongeza eneo la pili ni wakufunzi waliopo sasa ambao licha ya idadi yao ndogo lakini nao wameshindwa kuzalisha waamuzi walio bora ambao wangekuja kulinufaisha taifa na kubaki kuleta waamuzi wa kawaida.

“Jiulizeni kwa miaka mingapi sasa tumekuwa kama taifa tumelala na mkufunzi mmoja peke yake na je, tangu amekuwa akifanya hii kazi amezalisha waamuzi gani bora ambao wamekwenda kutupa heshima kubwa huko nje kwa kuchezesha mashindano makubwa?Tumekwama hatuzalishi tena wakufunzi na kubaki na watu walewale ambao wameshindwa kuonyesha ubora wa kazi yao. Hatua nyingine bora kwetu ni kufanya mabadiliko hapa lakini haitawezekana wanaokula pamoja hubaki pamoja.

“Nimesikia hivi karibuni wamefanya mchakato wa kupata wakufunzi wapya lakini tunaambiwa humo ndani kuna watu wamefanikiwa kufuzu lakini mamlaka haziwataki pengine ndio maana wanachelewa kutangazwa mtaona jinsi mambo yalivyo magumu.”

Hata hivyo, Hamduni anafafanua juu ya hilo; “Kila mkoa una wakufunzi wawili, mkufunzi wa utimamu wa mwili na mkufunzi wa sheria, halafu ukija ngazi ya taifa ambao pia wanatambulika na CAF, FIFA kuna kama wakufunzi 10 na ndio waalimu wa wakufunzi wote wa mikoa wanaotambulika na TFF.

“Hivyo TFF inajitahidi kwa kiasi kikubwa na bado inaendelea kuendesha kozi mbalimbali za waamuzi pamoja na wakufunzi.”

Baadhi ya wakufunzi wa waamuzi nchini ni Leslei Liunda, Samwel Mpenzu, Sudi Abdi, Israel Mujuni na John Kanyenye.

KAMATI YA WAAMUZI

Mwamuzi mmoja wa sasa anayechezesha mechi za ligi kutoka Dar es Salaam anaeleza kitendo cha kamati ya waamuzi kutokuwa huru nalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuzalishwa kwa makosa mengi ya waamuzi kutokana na ndani ya kamati hiyo kumekuwa yakipita maelekezo ya viongozi wao wa juu wa soka na hata wale wa klabumbalimbali.

“Kamati yetu ya waamuzi haipo huru kabisa shida ipo hapo maelekezo yote ya wakubwa lazima yapitie hapo kwenye kamati kwamba mwamuzi gani asipewe mechi na mwamuzi gani apewe mechi hata ukizalisha waamuzi bora lakini waje kufanya kazi na kamati kama hii wataharibika tu.

“TFF na Bodi ya ligi ilitakiwa kuwapa uhuru hawa ili taaluma yao iwahukumu na sio hiki kinachofanyika sasa, viongozi wa hawa wa mpira hawahawa ndio wale ambao wanaongoza klabu au wana klabu zao wanashusha maelekezo tu mechi hii klabu fulani inataka matokeo hakikisha unampeleka fulani na hapo sio bure ujue kuna nguvu imeshatumika kufanya maamuzi hayo.

“Nyie mnajua kuna waamuzi ambao wanachezesha mechi za klabu moja tu wakiwa wengi sana hawazidi watatu watazunguka haohapo na wakiwa kati au pembeni hiyo timu lazima ishinde tukiuliza tunajibiwa ulitaka maamuzi ya wakubwa yasitekelezwe? Mpira wetu umefia hapo kaka, kama simu zao zingewezwa kunaswa kwa teknolojia hawa Takukuru wangeyapata mengi sana yanayoendelea kwenye huu mpira wetu.

“Shida inaanza kwenye hii kamati inavyopata viongozi wake ambao ni lazima kwanza wawe watu wa viongozi wa juu wakati mwingine ipo klabu moja ambayo imekuwa ikishinikiza hata nani aingie kwenye ile kamati na nani asiwepo lengo ni kuhakikisha wanaoingia pale wanatakiwa kuwa watu ambao wataendana nao kwenye yale ambayo watayataka yafanyike na sio kwenda kinyume.

“Kuna kipindi bosi wetu mmoja aliwahi kuniita akanionesha ujumbe wa simu kutoka kwa mtu wa juu wa shirikisho akimpa maelekezo ya upangwaji wa waamuzi, akaniuliza mimi ningekuwa kwenye nafasi yake ningeweza kumwambia hapana hatutafanya hivyo kwahiyo ndugu zangu mpira wetu umeharibika pakubwa sana.”

MIZINGA YA VIGOGO

Bosi mmoja wa kamati ya waamuzi ambaye ameshamaliza muda wake anaweka wazi kutosimama imara kwa kamati yao wakati mwingine kunasababishwa na mambo yanayofanywa na viongozi baadhi wa shirikisho na hata bodi kwa kuomba misaada kwa viongozi wenye nguvu ya fedha wa klabu mbalimbali.

“Hayo mambo yapo mnaweza kuwalaumu viongozi wa kamati lakini shida wakati mwingine hainzii hapo inaanzia mbali sana mimi nilishawahi kuitwa wakati flani nikiwa pale nilikuwa nakataa haya maelekezo ya kubadilisha waamuzi.

Kuna siku nikaitwa na huyo kiongozi wa klabu moja kubwa ya hapa Dar es Salaam pale ofisini kwake akawa ananionyesha jinsi ambavyo viongozi wa juu wanavyomuomba misaada wakati mwingine kutengenezewa magari yao, kununua magari, yapo mambo ya fedha na wao ndio wakaenda kwake kunitaja kwamba mimi ndio shida.

“Bahati mbaya yule kiongozi ule ujumbe wa mimi kutajwa kwamba ndio nina shida akanitumia kwangu kwa Whatsap kisha nilipomaliza kusoma akaufuta hapo hapo huo ujumbe umeandikwa kabisa tatizo ni huyu lakini asijali wataniondoa na kweli baadaye ikala kwangu.”

UBINGWA SIMBA & YANGA

Klabu za Simba na Yanga zimetajwa kwa kina katika matatizo ya kuharibiwa kwa waamuzi ambapo matokeo yanapikuwa tofauti mwamuzi aliyesimamia hiyo mechi atawindwa mpaka kuondolewa kwenye mfumo wa waamuzi ilimradi kuhakikisha anakomolewa kwa kile alichofanya.

Mwamuzi mmoja wa pembeni kutoka Pwani ambaye aliwahi kukutana na kifungo  anaeleza kuwa makosa mengi ya waamuzi yanatokana na uhitaji wa ushindi na ubingwa kutoka kwa klabu hizo kubwa mbili na wakati mwingine Coastal Union ambazo hazitakiwi kupoteza kirahisi.

“Mechi ngumu ni za Simba,Yanga na Coastal Union hizi timu tatu ukipewa kazi lazima uwe makini wakati wowote lolote linaweza kukukuta ukapotea kwenye mpira wa nchi hii hasa unapokuwa zimepoteza mechi zao yaani hizi timu hazitakiwi kupoteza.

“Yanga ilikuwa miaka ya nyuma lakini hivi karibuni presha kubwa imekuwa kwenye mechi za Simba, ikipoteza tu lazima mwamuzi aingie lawamani na wakatri mwingine kufungiwa au hata kupotezwa kabisa endapo watakushikilia kwa nguvu.

“Jiulizeni mnafahamu Arajiga tangu achezeshe mechi ya Simba na Yanga umemuona wapi akichezesha tena mechi yoyote? Hayupo tena kwa kuwa hazungumzi vizuri anaonekana alichangia Simba kupoteza vibaya ile mechi.

“Kuna bao ambalo Yanga ililifunga wakati Kanoute (Sadio akiwa ameangushwa anaonekana hakufanya maamuzi yenye usawa lakini hawaangalii aliacha penalti ya wazi wakati Kapombe akimvuta mtu mguu ndani ya eneo la hatari na hilo la Kapombe huoni Yanga wakilalamika kwa kuwa wao walishinda.

“Msipoangalia Arajiga anaweza kuishia mechi ile kwa kuwa wakubwa wanasema alikuwa na uwezo wa kuzuia yale mabao yasiendelee kuwa mengi, hapa juzi pia Simba ilipata sare tusubiri kuona sijui kama yule dogo atapona kuna maneno yameshaanza kusemwa juu yake na ndio yanaanzaga hivyo hivyo hivyo.

“Wapo waamuzi wengi hawatakiwi sasa hivi na mpira wetu kina Sasii (Heri), mbona hamumulizii Komba (Frank) mwamuzi mkubwa kama yule ambaye Afrika ilishaanza kuona kitu kwake lakini sasa hivi mechi anazopewa utashangaa kuna Kayoko naye (Ramadhan) mtamuona mezani tu au mechi ya kawaida sana.

“Shida kubwa ni kwamba hawa wameshakataliwa na hizi klabu kubwa zinaona wakipewa hizi mechi basi wanapata shida nao kwahiyo ndio wanapotea hivyo taratibu.”

MALIPO YA WAAMUZI VS RUSHWA

Shida nyingine iliyobainika katika makosa ya waamuzi ni nguvu ya ushawishi kupitia rushwa ambapo uchunguzi unaonyesha waamuzi wa mechi zote za ligi malipo ni Sh 200,000 kama posho huku rushwa ikiwa ya viwango vya juu zaidi.

“Jiulizeni tunalipwa kiasi gani kila mechi ya ligi mwamuzi analipwa Sh 200,000 hiyo haijalishi mechi ya Simba na Yanga au Tabora na Kagera alafu hapohapo unamlipa mtu kiasi hicho wakati anaweza kukutana na mpaka Sh 10 milioni kama rushwa tena kwa klabu zote mbili kipi kitafanyika hapo?

“Malipo yetu ni madogo sana kuna wakati hizi timu zinaweza kukupa mpaka tiketi ya ndege kama zinakwenda kucheza mikoani au kukuleta  Dar es Salaam.”

Hata hivyo Hamduni anasema; “Kwanza hakuna pesa ndogo wala kubwa katika maisha ya binadamu na wala pesa haitoshi kabisa, ni tamaa ya mwanadamu kutaka kupata kingi.

“Kabla ya mashindano Bodi ya Ligi hutoa utaratibu wote wa malipo kama wanaona malipo ni kidogo unaruhusiwa kuacha na unasema ili uondolewe kwenye ratiba.

“Kuna ucheleweshaji wa malipo kweli lakini sio kwamba hawalipwi, Bodi ya Ligi inatuambia wamewalipa waamuzi pesa zao lakini waamuzi hawasemi wamelipwa zote ama hawajalipwa zote, maana hiyo ni siri ya mwajiri na mwajiriwa hadi wao waseme kuwa wamelipwa hiki na hawajilipwa hiki.

“Waamuzi huwa wanatuchonganisha viongozi, na hata familia zao kwasababu sio wawazi, matokeo yake tunapata taarifa kwenye vyombo vya habari kama wangekuwa hawalipwi wasingekuja tena, hakuna mtu anayekubali kuendelea kufanyakazi bila kulipwa.

“Uchelewesha upo na utaratibu wa kifedha, huwa wanapewa taarifa, wakilipwa natumiwa taarifa kuwa wamelipwa, waamuzi wengine ni waaminifu wanasema,” anasema

MECHI YA FA MALIPO JUU

“Mechi ambayo kidogo unaweza kukutana nayo ikawa na malipo makubwa ni fainali ya FA au nusu fainali na hapo zikikutana hizi timu kubwa kwa kuwa hizi zinasimamiwa na TFF hapo unaweza kukuta posho ikafika sh 500,000.”

Hamduni anasema; “Kila mashindano yana taratibu zake, haiwezekani kila kitu kikawa sawa, FA inasimamiwa na TFF wakati Ligi Kuu, Championship na First League ni za Bodi ya Ligi, hivyo waamuzi wasilinganishe, hata ligi za chini nazo zimetofautiana namna ya malipo kwa waamuzi.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live