Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waafrika 5 wanaovuta mkwanja mrefu zaidi

Mane Hela Ndefuuu Sadio Mane amejiunga Al Nassr ya Saudi Arabia

Sat, 5 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Sadio Mane amekamilisha uhamisho wake wa kujiunga na klabu ya Saudi Pro League, Al-Nassr, msimu huu wa joto na fowadi huyo wa Senegal amekuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa pesa nyingi zaidi klabuni hapo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 alifanyiwa vipimo vya afya mapema wiki hii kabla ya kukamilisha uhamisho wake kwenda Saudi Arabia kutoka kwa mabingwa wa Bundesliga, Bayern Munich, ambako alishindwa kuonyesha makali yake.

Kulingana na ripoti zilizopo, Mane atapokea kitita cha pauni 650,000 kwa wiki katika klabu ya Al-Nassr, huku kwa mwaka ikivuna pauni 34 milioni.

Hata hivyo, fowadi huyo wa Senegal atakuwa na kipato kidogo kuliko mchezaji mwenzake mpya, Cristiano Ronaldo, ambaye anapokea kitita cha pauni 177 milioni katika klabu hiyo ya Saudia.

Mkongwe huyo wa Ureno ameorodheshwa kama mwanasoka anayelipwa pesa nyingi zaidi duniani kwa mara ya tatu katika maisha yake ya soka na Forbes baada ya kuhamia Saudi Arabia.

Akiwemo Mane hii hapa orodha ya wachezaji watano kutoka Afrika ambao wanavuta mkwanja mrefu zaidi duniani kwa sasa.

SADIO MANE

Baada ya kufanya makubwa kwenye soka la ushindani barani Ulaya kwa miaka mingi akiwa na Liverpool ambako alitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2018-19 huku akiwa na medali ya mshindi wa pili 2017-18 na 2021-22, Mane ambaye mambo hayakumwendea vizuri Ujerumani ameamua kutua zake kwa Wasaudia ambako atakuwa akivuta mkwanja mrefu zaidi kuliko mchezaji yeyote kutoka Afrika (pauni 650,000 kwa wiki).

Hakuna ambacho Mane alikuwa amebakisha Ulaya ndio maana licha ya mambo kutomuendea vizuri akiwa na Bayern ilikuwa rahisi kwake kukubali ofa ya Al-Nassr ikumbukwe kuwa aliondoka Liverpool akiwa na mataji ya Ligi Kuu England, Kombe la FA na EFL Cup.

Ndani ya msimu wake mmoja ambao aliichezea Bayern amebeba Bundesliga na DFL-Supercup.

RIYAD MAHREZ

Julai 19, 2023, iliripotiwa na BBC kuwa Manchester City imekubali kumuuza nyota wake Mahrez kujiunga na Al Ahli ya Saudi Pro League kwa ada ya pauni 30 milioni.

Usajili wake ulithibitishwa Julai 28, 2023 kwa Mualgeria huyo kusaini mkataba ambao utamalizika 2027. Mkataba huo utamfanya kuwa anakunja pauni 481,000 kwa wiki kwa mantiki hiyo ni mchezaji wa pili kutoka Afrika ambaye atakuwa akilipwa mkwanja mrefu zaidi duniani.

Mahrez ameondoka England akiwa amebeba taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita wa 2022-23, manne ya Ligi Kuu England kwa msimu wa 2018-19, 2020-21, 2021-22, 2022-23 na mawili ya FA 2018-19, 2022-23 na matatu ya Carabao 2018-19, 2019-20, 2020-21.

KALIDOU KOULIBALY

Juni 25, 2023, ilitangazwa kuwa Koulibaly ambaye alikuwa akiichezea Chelsea alisaini klabu ya Saudi Pro League, Al-Hilal kwa ada ya pauni 20 milioni.

Beki huyo wa Kimataifa wa Senegal ambaye alizaliwa Saint-Die-des-Vosges, Ufaransa hakufurahia maisha yake ya soka akiwa England kutokana na Chelsea kupitia kipindi kigumu msimu uliopita kabla ya kuuzwa.

Kwa sasa Koulibaly ambaye alifanya makubwa kwenye soka la Ulaya akiwa na Napol atakuwa akuvuna pauni 412,000 kwa wiki.

MOHAMED SALAH

Nyota wa Liverpool, Mohamed Salah anashika nafasi ya nne kwenye orodha ya wachezaji wa Kiafrika ambao wanakusanya fedha nyingi kwa wiki kutokana na mishahara yao, anavuta pauni 350,000 kwa wiki na kwa wale ambao wanacheza soka la kulipwa Ulaya tu anashika namba moja.

Salah ni moto wa kuotea mbali, Januari 7, 2023, alimpita Kenny Dalglish katika nafasi ya sita kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo, na kufikisha mabao 173 kwenye mechi 280, alipofunga bao la pili katika sare ya 2-2 dhidi ya Wolves wakiwa Anfield kwenye Kombe la FA.

EDOUARD MENDY

Mendy alisajiliwa na klabu ya Saudi Pro League, Al Ahli Juni 28, 2023 kwa mkataba wa miaka mitatu, kwa ada iliyoripotiwa na vyombo vya habari vya Uingereza kuwa karibu pauni 16 milioni.

Kipa huyo ambaye alibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Chelsea, anatufungia orodha hii kwa kuwa anakusanya pauni 227,000 kwa wiki.

Chanzo: Mwanaspoti