Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

WPL kuna vipigo vizito usipime

Vipigo WPL WPL kuna vipigo vizito usipime

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) inaendelea kushika kasi huku ushindani na burudani zikiwa za kumwaga katika mechi za raundi ya saba.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, JKT Queens na Simba Queens ndizo pekee hazijapoteza mchezo wowote kati ya timu 10 zinazoshiriki huku Geita Queens ikiwa haijaonja ladha ya ushindi ikicheza michezo saba, kufungwa sita na kutoka sare mara moja.

JKT ni vinara wa ligi hiyo na pointi 18, ikishinda mechi zote sita ikifuatiwa kwa karibu na Simba iliyoshinda mitano na sare moja ikiwa na pointi 16, kisha Ceasiaa Queens ya tatu na pointi 13.

Yanga Princess ambayo mchezo wake wa mwisho ilishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Bunda Queens lililofungwa na nyota mpya wa kikosi hicho Mmarekani Kaeda Willson, imeendelea kusalia katika nafasi ya nne na pointi 12.

Fountain Gate Princess na Bunda Queens ziko nafasi ya tano na sita mtawalia na pointi nane kila moja, Baobab Queens ikiwa ya saba na pointi saba, huku Amani Queens na Alliance Girls zikiwa na pointi sita kila moja zikiwa nafasi ya nane na tisa mtawalia.

Geita Queens inaburuza mkia hadi sasa katika ligi hiyo yenye msisimko baada ya kuambulia pointi moja.

Ukiachana na matokeo hayo na namna msimamo ulivyo ila moja ya burudani inayopatikana ni idadi kubwa ya mabao yanayofungwa na Mwanaspoti linakuletea vipigo vikubwa vilivyojitokeza katika raundi saba za mwanzoni.

Aman Queens 0-10 JKT Queens

Hii ndiyo mechi inayoshikilia rekodi ya timu kuchezea kichapo cha mabao mengi zaidi hadi sasa kwenye Ligi Kuu ya Wanawake.

Mchezo huo ulipigwa Januari 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ilulu mjini Lindi ikiwa ni duru ya tatu tu ya ligi hiyo na wenyeji Aman Queens ikakubali kichapo hicho kutoka kwa maafande hao wa JKT.

Mabao ya JKT katika mchezo huo yalifungwa na Winfrida Gerald aliyefunga manne dakika ya 20, 44, 47 na 90, Amina Bilal akifunga matatu ‘hat trick’ dakika ya 25, 54 na 57.

Stumai Abdallah alifunga mabao mawili katika dakika ya 11 na 63 huku Fatuma Makusanya akihitimisha karamu ya mabao kwa kufunga moja katika dakika ya 17.

Simba Queens 7-0 Alliance Girls

Januari 27, mwaka huu Simba ikafanya unyama kwa kuifunga Alliance mabao 7-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Katika mechi hiyo iliyokuwa ya raundi ya saba mabao ya Simba yalifungwa na Jentrix Shikangwa aliyetupia matatu ‘hat trick’ dakika ya 48, 77 na 80 huku mengine yakifungwa na Aisha Mnunka dakika ya 51, Asha Djafari aliyecheka na nyavu mara mbili dakika ya 54 na 67 na Vivian Corazone aliyefunga bao moja dakika ya 90.

Yanga Princess 6-1 Amani Queens

Wananchi na wao hawako nyuma kwenye ligi hiyo licha ya kujikongoja tofauti na ilivyo kasi ya kaka zao kwenye Ligi Kuu lakini nao wapo kwenye orodha ya timu zilizogawa dozi nzito msimu huu.

Mchezo huo uliopigwa Desemba 27, mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex ikiwa ni raundi ya pili, mabao hayo ya Yanga yalifungwa na Janeth Bundi na Precious Christopher ambao kila mmoja alitupia mawili huku mengine yakifungwa na Noela Luhala na Madina Traole huku lile la kufutia machozi kwa upande wa wageni Amani Queens likifungwa na Janeth Nyagali.

JKT Queens 5-0 Alliance Girls

JKT Queens iliendelea kushusha vipigo kwa wapinzani inaokutana nao baada ya kuifunga Alliance Girls mabao 5-0.

Mchezo huo wa mzunguko wa tano ulipigwa pia kwenye Uwanja wa Azam Complex Januari 15, mwaka huu na mabao ya JKT yaliwekwa nyavuni na nyota wa timu hiyo, Stumai Abdallah aliyefunga manne huku Jamila Rajabu akitupia nyavuni moja.

Simba Queens 5-0 Ceasiaa Queens

Huu ulikuwa mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Wanawake na Simba kuanza kwa kishindo ikiigaragaza Ceasiaa kwa mabao 5-0.

Mchezo huo ulipigwa Desemba 20, mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na mabao ya wenyeji yalifungwa na Aisha Mnunka aliyefunga matatu yaani ‘hat trick’, huku mengine mawili yakifungwa na Asha Djafari na Mwanahamisi Omari ‘Gaucho’.

Bunda Queens0-4 J KT Queens

Mechi hiyo ilipigwa kwenye Uwanja wa Karume, Mara Desemba 20, mwaka jana, ikiwa ni ya mzunguko wa kwanza na JKT kushinda mabao 4-0.

JKT ikiwa ugenini ilipata mabao yake manne kupitia kwa Winfrida Gerald aliyefunga mawili na mengine yakifungwa na Stumai Abdallah na Donesia Minja.

Simba Queens 5-2 Baobab Queens

Mchezo huo ulikuwa wa mzunguko wa nne ambapo Simba ilishinda 5-2 dhidi ya Baobab katika mechi iliyopigwa Desemba 28, mwaka jana.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex mabao ya Simba yalifungwa na Ainembabazi Joanita, Asha Djafari akafunga mawili huku mengine yakifungwa na Vivian Corazone dakika ya 37 na Asha Mwalala.

Kwa upande wa mabao ya kufutia machozi ya Baobab yalifungwa na Elizabeth Nashon huku kipa wa Simba Queens, Carolyene Rufa akijifunga.

Amani Queens 4-1 Alliace Girls

Wakali hao kutoka mkoani Lindi, licha ya kuwepo kwenye orodha ya timu zilizopokea vichapo vikubwa kwenye ligi hiyo, lakini nao wanaingia katika orodha hiyo.

Mchezo huo ambao Amani Queens ilishinda kwa mabao 4-1 dhidi ya Alliance Girls ulikuwa wa mzunguko wa nne ukipigwa katika Uwanja wa Ilulu, Lindi, Januari 9, mwaka huu.

Chanzo: Mwanaspoti