Ile siku ndiyo leo. Baada ya miezi minane kupita bila kushuhudia mtanange wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), sasa imerudi na leo michezo kadhaa itapigwa kwenye viwanja tofauti mabingwa JKT Queens wataikabili Bunda Queens kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, Simba Queens ikiikaribisha Ceasiaa Queens katika Uwanja wa TFF Kigamboni, huku Alliance Girls ikiikaribisha Geita Gold Uwanja wa Nyamagana, Fountain dhidi ya Amani Queens Uwanja wa Jamhuri na mechi zote zikipigwa saa 10 jioni. Hizi hapa takwimu fupi za vikosi:
1.Simba Queens (Dar)
Kocha : Juma Mgunda (Tanzania)
Nahodha : Violeth Nicholaus(Tanzania)
Staa : Fatuma Issa ‘Fetty Densa’(Tanzania)
Msimu uliopita Simba ilipokonywa ubingwa wa Ligi Kuu na JKT iliyokata pia tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake na kuishia hatua ya makundi.
Msimu huu imeanza vyema kwa kubeba ubingwa wa Ngao ya Jamii baada ya kuitoa JKT Queens kwa mikwaju ya penati 5-4 kwenye fainali zilizofanyika Uwanja wa Azam Comlex, Chamanzi, Desemba 12 mwaka huu.
2.Yanga Princess (Dar)
Kocha Mkuu: Charles Haalubono (Zambia)
Nahodha: Irene Kisisa (Tanzania)
Staa: Precious Christopher (Nigeria)
Yanga imeanza kuonyesha upinzani kwa mtani wake, Simba kwani kwa misimu miwili imefuta uteja wa kufungwa mabao mengi. Kwenye michuano ya ngao ya jamii, Yanga ilionyesha ushindani hadi dakika 90 zikitamika bila ya kuruhusu bao na mikwaju ya penati 4-5 iliyoipata ikiwakosesha kwenda fainali na kuchukua mshindi wa tatu.
3.JKT Queens (Dar)
Kocha Mkuu: Ester Chabruma (Tanzania)
Nahodha: Donisia Minja (Tanzania)
Staa:Stumai Abdallah (Tanzania)
Ndio bingwa mtetezi wa ligi msimu uliopita na bingwa wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA. Mbali na hayo, pia timu hiyo wachezaji wake na benchi la ufundi ni wazawa na ilibeba ubingwa wa ligi bila ya kupoteza mchezo wowote.
4.Fountain Gate (Dodoma)
Kocha Mkuu: Masoud Juma (Tanzania)
Nahodha: Acquila Gasper (Tanzania)
Staa: Hasnath Ubamba (Tanzania)
Licha ya kushika nafasi ya tatu kwenye ligi msimu uliopita, timu hiyo imekuwa ikizalisha vipaji vingi vya kike vinavyotumiwa na timu tatu zenye ushindani nchini yaani Simba, Yanga na Fountain na nje ya nchi.
Kuna wachezaji kama Winifrida Gerald, Joyce Lema ambao wamesajiliwa na JKT msimu huu na Nabbosa Ritticia akiibukia Simba wote ni zao la Fountain.
5. Alliance Queens (Mwanza)
Kocha Mkuu: Ezekiel Chobanka
Nahodha: Anitha Odongo
Staa: Winifrida Charles
Alliance ilimaliza ligi msimu uliopita ikishika nafasi ya tano na pointi 27 juu ya Yanga iliyomaliza nafasi ya nne na pointi 34. Msimu uliopita ilikuwa moja ya timu tano zilizofunga hat-trick angalau mbili na zote zilifungwa na staa wao, Winifrida aliyemaliza msimu na mabao 13.
6.Amani Queens (Lindi)
Kocha Mkuu: Said Chuma
Nahodha: Sabina Mbuga
Staa: Sabina Mbuga
Haikufanya vizuri msimu uliopita kwani ilimaliza nafasi ya nane kati ya timu 10, ikishinda mechi mbili kwenye michezo 18.
Ilikuwa kwenye hatihati ya kushuka daraja kwani ilimaliza na pointi nane sawa na Tigers Queens iliyoshuka daraja wakitofautiana mabao ya kufungwa, ikiruhusu 41 na Tiger ikiruhusu mabao 45.
7.Baobab Queens (Dodoma)
Kocha Mkuu: Juma Maulid
Nahodha: Martha John
Staa: Jamila Mnunduka
Haikuwa nafasi mbaya msimu uliopita kwani ilimaliza ya sita ikikusanya pointi 22 kwenye mechi 18, ikishinda mechi sita, sare nne na kupoteza nane.
Imetoa wachezaji wawili kwenda Yanga, beki Neema Charles na winga Mariana Keneth ambao walikuwa tegemeo kwenye kikosi.
8.Bunda Queens (Mara)
Kocha Mkuu: Alley Ibrahim
Nahodha: Ester Marwa
Staa:Ester Marwa
Imeandika historia kwa mara ya kwanza timu kutoka Mara kupanda Ligi Kuu msimu huu. Ni miongoni mwa timu zitakazoshiriki msimu huu ikipata nafasi hiyo baada ya Mkwawa na The Tigers Queens kushuka.
9.Ceasiaa Queens (Iringa)
Kocha Mkuu:Emmanuel Massawe
Nahodha:Asphat Kasindo
Msimu uliopita nayo haikukaa kinyonge ilimaliza nafasi ya saba ikikusanya point 21, ushindi mechi sita, sare tatu na kupoteza tisa.
Aliyekuwa mshambuliaji wao Anembabazi Joanita ambaye kwa sasa anakipiga Simba alifunga hat-trick dhidi ya Tiger.
10.Geita Gold Queens (Geita)
Kocha Mkuu: Joseph Charles
Nahodha:Naomi Samwel
Geita ilipanda daraja msimu huu na kuungana na Bunda baada ya kushinda michezo yao ya nusu fainali kwenye Ligi Daraja la Kwanza mkoani humo.