Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyuma vitatu vinashuka Simba, kocha Mreno kuiona Mbeya City Jumatano

Vigogo Simba.jpeg Vyuma vitatu vinashuka Simba, kocha Mreno kuiona Mbeya City Jumatano

Sun, 20 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kwenye dirisha dogo linalofunguliwa Desemba 15, Simba itashusha mashine tatu, taarifa za uhakika zinathibitisha.

Chanzo cha kuthibitika kinadai kwamba ndege zitaanza kupishana kwa fujo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kuanzia wiki ijayo.

Ataanza kwanza Kocha Mkuu ambaye ni raia wa Ureno. Achana na yule wa viungo kutoka Afrika Kusini na Makipa wa Morocco ambao wote wameshatua tayari. Bosi Mkubwa atatua Jumatatu jioni.

Habari za uhakika zinasema kwamba uongozi pamoja na benchi la ufundi chini ya kocha Juma Mgunda baada ya kukifanyia tathimini ya kutosha kikosi chao wamekubaliana kuleta mashine tatu na tayari wameanza kuwafuatilia wachezaji mbalimbali.

Mmoja wa viongozi wa usajili wa Simba ameliambia Mwanaspoti kwamba usajili wa kwanza utakuwa na mastraika wawili wenye uwezo wa kufunga zaidi ya waliyopo wakati huu yaani John Bocco na Habibu Kyombo. Na inaweza kuwa sapraizi mmoja wa mastaa hao akatua hata kabla dirisha halijafunguka.

Inaelezwa Mgunda amewambia mabosi zake anataka mastraika wawili wa maana watakaocheza hadi Ligi ya Mabingwa Afrika ili kuwa na machaguo nani wa kumtumia wakati gani na yupi ataanzia benchi au kuanza wote wawili kwa pamoja kulingana na mchezo ulivyo kupunguza presha kwenye makundi Afrika.

Bocco amepungua makali yake na hatumiki mara kwa mara wakati Kyombo anaingia na kutoka kikosi cha kwanza, wakati Mserbia Dejan Georgijevic alishavunja mkataba na kusepa zake.

Lakini habari zinasema pia Mgunda ambaye ni kipenzi cha mashabiki, amewaeleza mabosi zake anahitaji kiungo mwingine wa ukabaji atakayecheza mashindano hayo ya CAF, kwani Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute wanaotumika mara kwa mara ikitokea mmoja kati ya hao amekosekana eneo hilo huonekana mapungufu.

Wachezaji wanaocheza kwenye nafasi hiyo ya kiungo, Jonas Mkude, Nassoro Kapama, Victor Akpan na Erasto Nyoni wameonekana kushindwa kucheza kwenye kiwango cha juu kama benchi la ufundi linahitaji.

Eneo lingine ambalo benchi la ufundi na viongozi wamekubaliana kuliongeza nguvu ni beki mwenye uwezo wa kucheza mlinzi wa kushoto na kulia, kwani inaonekana Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ametumika zaidi huku Gadiel akishindwa kumpa ushindani wa kutosha.

Beki wa kulia, Shomary Kapombe na Israel Mwenda wamekutana na majeraha ya mara kwa mara hadi nafasi hiyo muda mwingine hutumika wachezaji ambao asili yao sio hapo kama Jimsony Mwanuke ambaye ni mshambuliaji.

Alipoulizwa Mgunda kuhusiana na mipango yake ya dirisha dogo la usajili msimu huu alikiri kwamba lazima atafanya maboresha ya kikosi chao kwa kuongeza nguvu baadhi ya maeneo kulingana na mahitaji.

“Muda bado haujafika wa usajili kuna mechi zipo mbele yetu tunahitaji kupata ushindi ili kuendelea kuwa kwenye mazingira mazuri katika msimamo wa ligi na baada ya hapo tutaweka nguvu ya kutosha kwenye dirisha la usajili baada ya kufunguliwa,” alisema Mgunda na kuongeza kwamba:

“Uongozi wetu upo makini kushirikiana nasi benchi la ufundi ndio maana limetuongezea nguvu kwa kuleta wataalamu wawili na naamini hivyo kwenye usajili tutaleta wachezaji wengine wa maana ili kufanya vizuri kwenye mashindano ya ndani pamoja na CAF.”

Simba imepania kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na kurejesha makombe yake ya ndani yaliyobebwa na Yanga msimu uliopita. Katika msimu huu wa mashindano ya Afrika, Simba imetinga makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Chanzo: Mwanaspoti