Mabosi wa Simba wameitana chemba na kufanya kikao kizito kujadili ripoti ya kocha Pablo Franco aliyetaka ifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa Januari 15.
Kutoka ndani ya kikao hicho kizito, Mwanaspoti linafahamu wanahitaji mashine tatu mpya katika nafasi tofauti kulingana na upungufu ulioonyeshwa na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara mpaka sasa.
Nafasi ambazo Pablo ametaka zifanyiwe kazi kwa kuletewa wachezaji wapya ni straika mwenye uwezo wa kufunga zaidi ya John Bocco, Meddie Kagere na Chriss Mugalu; kiungo mshambuliaji (namba nane au kumi), winga mwenye uwezo wa kucheza kushoto na kulia, kiungo mkabaji na beki wa kati. Mwanaspoti limepata taarifa kutoka ndani ya Simba kuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa ni Clatous Chama na kuna wengine wawili wapya waliopendekezwa na wakati huu na wanaendelea kujadiliwa.
Nyota wa kwanza ni straika wa Nkana, Alex Bazo Ng’onga anayetazamwa kama anaweza kwenda kufanya kazi zaidi ya ile iliyoonyeshwa na Kagere na Bocco tangu Pablo atue Simba.
Pablo anataka straika mpya kutokana na kutoridhishwa na viwango vya mastraika wake, lakini majaraha ya muda mrefu aliyonayo Chris Mugalu ambaye hajacheza mechi tangu kocha huyo alipoanza kazi ya kukinoa kikosi.
Vilevile mezani Simba kuna jina la winga wa Ligi Kuu ya Zambia anayekipiga klabu ya Kabwe Warriors, Harrison Mwendwa ambaye anatazwa kuja kuongeza makali Msimbazi.
Pablo baada ya kupendekeza majina hayo mawili mabosi wa Simba wamemtaka atulie wanayafanyie kazi kwa kuwafuatilia nyota hao, lakini nao kuna wachezaji wengine wanawaangalia katika maeneo ambayo anataka kisha watawapambanisha na ambao watakuwa bora ndio watasajiliwa.
“Majina hayo yapo. Kuna ambao tutawapendekeza ili kila nafasi moja ambayo tunataka kusajili wawepo wachezaji chaguo la kwanza na la pili kisha yule bora ndiye tutakubaliana kwa mujibu wa kocha anaweza kuwa ametoka upande wake au wetu,” alisema kiongozi mmoja wa juu Msimbazi.
“Mahitaji ya timu yalikuwa ni wachezaji wapya watatu lakini hili la kiungo mkabaji limekuja kutokana na Taddeo Lwanga kuwa majeruhi wa muda mrefu na hatufahamu atarudi akiwa katika hali gani ya utimamu wa mwili.”
Ikumbukwe kwa nyakati tofauti baada ya kucheza mechi ya ugenini na Red Arrows viongozi wa juu wa Simba, mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ na mtendaji mkuu, Barbara Gonzalez walieleza watafanya uamuzi mgumu kusajili nyota wapya wa maana.
Bazo alijiunga na Nkana FC mwishoni mwa Aprili 2021 akitokea Power Dynamos ambapo alimaliza msimu akiwa mfungaji bora wa Nkana na mabao tisa katika mechi 13 alizocheza.