Imekwisha hiyo! Ndivyo utakavyoweza kusema baada ya mabosi wa Yanga, kukamilisha usajili wa nyota wanne wapya akiwepo mzawa mmoja pekee ambaye ni Nickson Kibabage.
Kibabage alijiunga na Yanga na kuwa mchezaji wa kwanza kutambulishwa rasmi hivi karibuni akitokea Singida Fountain Gate kwa dau la Sh 220Mil.
Wakati Yanga ikikamilisha usajili wa Kibabage anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji na beki wa kushoto, timu hiyo imetangaza kuachana na Abdallah Shaibu ‘Ninja’, David Bryson, Tuisila Kisinda, Bernard Morrison na Erick Johora.
Mmoja wa mabosi wa Yanga, amelsema kuwa, timu hiyo, katika usajili wao wa msimu ujao umekamilika kwa kuwasajili wachezaji wanne pekee, huku Kibabage akiwa mchezaji wa kwanza kutambulishwa.
Bosi huyo aliwataja wengine ni winga wa Meniema FC ya DR Congo, Maxi Nzengeli Mpia, Fred Gift ambaye ni beki wa kati kutoka SC Villa ya Uganda, wa mwisho ni kiungo mkabaji wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Mohammed Zoungrana ambaye ndiye anakuja kupewa jezi namba 6.
Aliongeza kuwa, baada ya kukamilika kwa usajili huo, hawatasajili mchezaji mwingine kuelekea msimu ujao ambao wamepanga kufanya vema katika michuano ya ndani na kimataifa.
“Yanga tumewasajili wachezaji wanne pekee ambao ni Kibabage, Gift, Zoungrana na Maxi, baada ya hao hatutasajili mchezaji mwingine.
“Hatutaki kufanya usajili wa wachezaji wengi katika usajili huu wa dirisha kubwa, hiyo ni kutokana na ubora na viwango vya wachezaji wetu ambavyo wamevionesha msimu uliomalizika.
“Ukiangalia mafanikio ambayo tumeyapata katika msimu uliopita kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutetea mataji yote ya ndani ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports, inathibitisha hilo,” alisema bosi huyo.
Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, alizungumzia hilo la usajili kwa kusema: “Katika dirisha hili la usajili hatutafanya usajili mkubwa wa wachezaji na badala yake tutasajili wachache watakaokuja kukiimarisha kikosi chetu.
“Wachezaji hao wamesajiliwa kwa mujibu wa ripoti ya benchi la ufundi lililopita chini ya Nabi (Nasreddine) aliyemaliza muda wake kuifundisha timu yetu ya Yanga.”
Katika hatua nyingine, Zoungrana, juzi aliwaaga viongozi, wachezaji na mashabiki wa ASEC Mimosas baada ya kudumu hapo kwa kipindi cha takribani miaka miwili kuanzia 2021 hadi 2023, huku akitajwa muda wowote kutambulishwa Yanga.