Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyuma vilivyotua na mitihani inayowakabili

Jobe A0001 Vyuma vilivyotua na mitihani inayowakabili

Thu, 18 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Labda msilete timu. Ndivyo ambavyo mashabiki wa Simba na Yanga wanavyotambiana huko mtaani kufuatia usajili ambao umefanywa na miamba hiyo ya soka la Tanzania katika dirisha dogo la usajili ambalo lilifungwa usiku wa Jumatatu ya Januari 15.

Katika dirisha hilo la usajili, Simba, Yanga na Azam FC zimeendelea kuonyesha ubabe wao kwa kusajili wachezaji wa kigeni na awamu hii kwa mara ya kwanza watashuhudiwa wachezaji kutoka Colombia wakicheza soka la kulipwa nchini.

Wachezaji hao ni Franklin Navarro na Yeison Fuentes waliosajiliwa na Azam FC huku nyota ambao wamebeba matumaini ya mashabiki wa Yanga ni Augustine Okrah (Bechem United) na Joseph Guede (huru), wakati kwa upande wa Simba majembe mapya ni washambuliaji Freddy Michael (Green Eagles) na Pa Omar Jobe na kiungo mkabaji, Babacar Sarr.

Nini ambacho nyota hao na wengine ambao wamesajiliwa kwenye dirisha hili la usajili wanaenda kukiongeza kwenye vikosi hivyo kwa kuangalia udhaifu ulioonekana hadi mabenchi yao ya ufundi yakapendekeza fasta kuletewa wachezaji wengine kwa ajili ya kuongeza nguvu.

Uchambuzi huu, utamuangazia mchezaji mmoja baada ya mwingine hasa majina makubwa ambayo yanaonekana kuwa na nafasi ya kuingia kwenye mipango ya timu kwa sasa kwa kuangalia nini ambacho alikuwa akifanya huko alipotoka, anawezaje kuwa msaada kwa kuangalia wapi ambapo wenzake wamekwama.

PAR OMAR JOBE

Mgambia huyo amejiunga na Wekundu wa Msimbazi kwa kusaini mkataba wa miaka miwili akitoka Kazakhstan  ambako alikuwa akicheza soka la kulipwa akiwa na  FC Zhenis inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.

Nchini Gambia Pa Omar anajulikana kwa jina la utani la Drogba. Moja ya rekodi yake ni kuwa mfungaji bora wa ligi ya Senegal akicheza pamoja na Babacar Sarr kwenye ligi hiyo kabla ya kwenda Ulaya.

Jobe anaweza kuwa na nafasi ya kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha Simba kutokana na fagio ambalo limepitishwa na Abdelhak Benchikha kwa Jean Baleke na Moses Phiri ambao awali ndio waliokuwa wakiongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kabla ya kibao kuwageukia na kupewa ‘Thank You’.

AUGUSTINE OKRAH

Hii itakuwa mara yake ya pili kucheza soka la kulipwa Tanzania, mara yake ya kwanza alikuwa na Simba na sasa yupo na Wananchi ambao wana kibarua cha kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara na kuvuka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya msimu uliopita kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho.

Okrah namba zake zinatisha huko ambako ametoka Ghana, anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji hatari zaidi, unajua kwanini? Alifunga mabao tisa na kutoa asisti mbili kwenye mechi 16, hivyo Wananchi wakaona ni ingizo sahihi kwenye kikosi chao kwa ajili ya kuongeza makali kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Ukiitazama nafasi ya Okrah kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga unaweza kutatizika kutokana na kufanya vizuri kwa Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua na Maxi Mpia Nzengeli lakini hesabu za Miguel Gamondi ni kubwa na ndio maana aliwaambia mabosi wa timu hiyo kumletea winga huyo mwenye uwezo pia wa kucheza kama namba 10.

Kwanini Okrah ameongezwa? Gamondi anahitaji kuwa na kikosi kipana chenye ubora, hivyo uwepo wa winga huyo unaweza kumfanya kocha huyo kuwa na machaguo zaidi kwenye kikosi chake cha kwanza maana wale ambao alikuwa nao benchi walionekana kushindwa kumpa kile ambacho alikuwa akihitaji.

FREDDY MICHAEL

Hili ni ingizo lingine kwenye kikosi cha Simba kwa ajili ya kutatua changamoto ya mabao ambayo ilikuwa ikimuumiza kichwa Benchikha hadi kuongea wazi kwenye moja ya mahojiano yake kwamba hakuwa akiridhishwa na utendaji wa safu yake ya awali ya ushambuliaji, iliyokuwa ikipoteza nafasi nyingi za wazi.

Freddy ni raia wa Ivory Coast ambaye amesajiliwa na Simba SC akitokea Green Eagles FC ya Ligi Kuu nchini Zambia ambapo ameondoka akiwa kinara wa mabao. Hadi Desemba 30 alikuwa tayari amefunga magoli 14 kwenye mashindano yote.

Ukimuangalia Freddy ni mshambuliaji mzoefu ambaye naye atakuwa na nafasi sawa na Jobe, hivyo yule ambaye atachanga karata zake vizuri anaweza kukamatia ufalme kwenye kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi.

YEISON FUENTES

Kipindi fulani kocha wa Azam FC, Yousouph Dabo ilimbidi kumtumia  Edward Manyama kama beki wa kati yote hiyo ni kutokana na kukosa kile ambacho alikuwa akihitaji kutoka kwa wachezaji wengine, inawezekana kuwa ni urefu na vitu vingine vya kiufundi zaidi, alikuwa akicheza sambamba na Daniel Amoah.

Hatimaye sasa, Dabo ameletewa Yeison ambaye anapewa nafasi ya kuingia moja kwa moja kwenye kikosi hicho kama atakuwa amefikia kile ambacho alikuwa akikihitaji kocha huyo, anaweza kucheza sambamba na Amoah kwenye eneo la beki ya kati.

Hata hivyo, Yeison mwenye miaka 21, atatakiwa kupewa muda kuzoea soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla. Ni beki mwenye akili ya mpira, ana uwezo mzuri wa kutumia nguvu kuanzisha mashambulizi kulingana na mikanda yake ya video.

BABACAR SARR

Huyu kiungo mkabaji, raia wa Senegal mwenye umri wa miaka 26 ambaye Simba imemsajili kutoka US Monastir kwa mkataba wa miaka miwili.

Sarr ni kiungo mwenye uzoefu wa kucheza soka la Afrika ambapo mbali na Monastir amewahi kuzichezea Olympique Beja ya Tunisia, Teungueth FC, AS Pikine na Mbour P.C zote za Senegal.

Sarr mwenye uwezo mkubwa wa kucheza kama kiungo mkabaji na wakati mwingine kama kiungo mshambuliaji, kwa mara ya kwanza Wanasimba walipata nafasi ya kumuona kwenye Kombe la Mapinduzi. 

Nyota huyo anatazamiwa kuongeza nguvu kwenye eneo la kiungo ambalo kwa sasa muhimili wake ni Fabrice Ngoma huku Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin wakionekana kupungua ubora wao hivyo ujio wake unaweza kuwatoa usingizini.

JOSEPH GUEDE

Matumaini ya mashabiki wa Yanga yapo kwake kutokana na uhitaji wa timu hiyo kwa sasa maana bado hawajapata marithi wa Fiston Mayele ambaye aliwafanya kila wakati kutetema kwenye michezo yao mbalimbali ya ushindani.

Mwanzoni mwa msimu, Yanga ilimsajili Hafiz Konkoni kwa lengo la kuziba pengo la Mayele aliyejiunga na Pyramids FC, lakini mshambuliaji huyo wa Ghana alishindwa kuwika akiwa na Wananchi hivyo amempisha Guede.

Guede ni mshambuliaji mzoefu ambaye aliwahi kucheza soka la kulipwa Ulaya, wasiwasi wa wadau wengi wa soka la Tanzania ni juu ya kuwa kwake nje ya uwanja tangu Septemba 15 mwaka jana kufuatia kuachwa na Tuzlaspor ya Uturuki.

FRANKLIN NAVARRO

Mzaliwa huyo wa Sabanalarga huko Colombia, anaweza kuwa na kazi ngumu na kubwa ya kufanya kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Azam FC kutokana na kufanya vizuri kwa washambuliaji, Prince Dube na Alassane Diao.

Ni kama Dabo kuna bomu anataka kulisuka kwenye kikosi hicho ndio maana akaona kuna haja ya kuongeza mshambuliaji mwingine kwenye kikosi hicho licha ya kufanya vizuri kwa safu yake ya ushambuliaji.

Ujio wa Mcolombia huyo ulifungua milango ya kuondoka kwa Idris Mbombo ambaye amerejea Zambia kuichezea Nkana FC.

WENGINE

Kiungo mshambuliaji, Saleh Masoud Karabaka (JKU), Ladaki Chasambi (Mtibwa Sugar) na Edwin Balua (TZ Prisons) walitua Simba, kipa Mohamed Mustafa (El Merreikh ya Sudan) katua Azam na Shekhan Ibrahim Khamis kutoka JKU alisajiliwa Yanga. Kazi wanayo!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live