Ndo hivyo, maisha yanakwenda kasi si mchezo. Na hivi unavyosoma hapa, makinda wa soka wawili wa England, ndiyo wanasoka wenye thamani kubwa zaidi duniani kwa sasa. Kwa kuzingatia soko, ukitaka huduma zao, basi utavunja benki.
Unawajua? Ni hawa hapa, staa wa Borussia Dortmund, Jude Bellingham, 19, na winga wa Manchester City, Phil Foden, 22, ambao wote wamemfunika na kumwondoa kileleni supastaa wa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe.
Bellingham, ambaye alionyesha kiwango bora kabisa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar alipokuwapo na kikosi cha England, amekuwa kwenye rada za klabu kubwa wakiwamo Real Madrid wakihitaji saini yake.
Na sasa thamani yake huko sokoni inatajwa kuwa Pauni 183.9 milioni kwa mujibu wa CIES Football Observatory.
Jambo hilo linamfanya Bellingham kuwa mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi huko sokoni, akimzidi mchezaji mwenzake kwenye kikosi cha Three Lions, Foden, anayethaminishwa kwa Pauni 177.5 milioni, wakati Mbappe, ambaye alifunga hat-trick kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 2022 wakati Ufaransa ilipochapwa na Argentina, anatajwa kuwa na thamani ya Pauni 168.7 milioni.
Fowadi wa Real Madrid, Vinicius Jr yupo kwenye namba nne, akithaminishwa kwa Pauni 168.5 milioni. Na kiwango hicho ni kikubwa kuliko alichothaminishwa straika wa Man City, Erling Haaland, anayetajwa kuwa na thamani ya Pauni 154.8 milioni na kushika namba tano kwenye orodha ya wanasoka wenye thamani kubwa duniani.
Bellingham, ambaye alikuwa namba tano awamu iliyopita, amepaa hadi namba moja huku Haaland akiwa kwenye namba tano.
Na hiyo imekuja licha ya straika huyo wa kimataifa wa Norway kufunga mabao 27 hadi sasa akiwa na kikosi cha Man City alichojiunga nacho kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwaka jana.
Wakati huo huo, viungo wawili wa Barcelona, Pedri (Pauni 150.6milioni) na Gavi (Pauni 130.6 milioni) wameachwa nyuma kidogo tu na Haaland kwenye msimamo huo mpya unaohusu thamani za wanasoka duniani.
Fowadi wa Bayern Munich, Jamal Musiala (Pauni 128.5 milioni), ambaye amebadili utaifa kwa kuitumikia Ujerumani badala ya England kwenye soka la kimataifa na kwenye orodha hiyo anashika namba nane.
Beki wa kati wa Croatia, Josko Gvardiol (Pauni 111.4 milioni) anashika namba tisa na hakika alikuwa kwenye kiwango bora kabisa katika fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qayat, huku kiungo wa Uruguay, Federico Valverde anakamilisha 10 bora ya wanasoka wenye thamani kubwa zaidi duniani kwa sasa, akithaminishwa kwa Pauni 109.3 milioni.
Jumla ya wachezaji 14 wengine wa England wamejumuishwa kwenye 100 bora ya wenye thamani kubwa sokoni kwa sasa, akiwamo Bukayo Saka (Pauni 96.2 milioni), Reece James (Pauni 87.9milioni) na Raheem Sterling (Pauni 82.3milioni).
MASTAA WENYETHAMANI KUBWAZAIDI SOKONI
1.Jude Bellingham - Pauni 183.9 milioni
2.Phil Foden - Pauni 177.5 milioni
3.Kylian Mbappe - Pauni 168.7 milioni
4.Vinicius Jr - Pauni 168.5 milioni
5.Erling Haaland - Pauni 154.8 milioni
6.Pedri - Pauni 150.6 milioni
7.Gavi - Pauni 130.60 milioni
8.Jamal Musiala - Pauni 128.5 milioni
9.Josko Gvardiol - Pauni 111.4 milioni
10.Federico Valverde - Pauni 109.3 milioni