Idadi ya viwanja 18 vimetumika kwa mechi za Ligi Kuu ya NBC ambapo kabla ya mchezo wa juzi usiku baina ya Namungo FC na Dodoma Jiji, vilikuwa vimeandaa idadi ya mechi 232.
Katika mechi hizo 232, idadi ya mabao ambayo ilikuwa imefungwa ilikuwa ni 537 ikiwa ni wastani wa mabao 2.3 kwa mechi.
Viwanja hivyo 18 vilivyotumika kwa mechi za Ligi Kuu ya NBC msimu huu ni Benjamin Mkapa, Azam Complex, Uhuru, Jamhuri Morogoro, Jamhuri Dodoma, CCM Liti, CCM Kirumba, Nyankumbu, Kaitaba, Kassim Majaliwa, Sokoine, Manungu, Highland Estates, Nelson Mandela, Black Rhino, Ushirika, Mkwakwani na Sheikh Amri Abeid.
Kati ya viwanja hivyo, vipo vile ambavyo nyavu zao zilitikiswa mara nyingi lakini kuna vile ambavyo vilikuwa vigumu kwa kuruhusu idadi kubwa ya mabao kufungwa.
Ifuatayo ni orodha ya viwanja nane ambavyo vimeongoza kwa idadi kubwa ya mabao katika msimu huu.
Benjamin Mkapa- Mabao 89
Idadi ya mechi 31 za Ligi msimu huu zimechezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla haujapunguzwa idadi ya mechi zinazochezwa hapo na katika mechi hizo zilizochezwa, mabao 89 yalipachikwa ikiwa ni wastani wa mabao 2.9 kwa mechi.
Mechi iliyozalisha idadi kubwa ya mabao uwanjani hapo ilikuwa ni ile ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Tanzania Prisons.
Azam Complex- Mabao 60
Kwa wastani wa mabao kwa mechi, Azam Complex ni kinara kwani wastani wa mabao yaliyofungwa hapo msimu huu ni mabao 3.3.
Hata hivyo, kwa namba ya mabao, unashika nafasi ya pili ukuwa na mabao 60 yaliyopachikwa katika mechi 18.
Sokoine-Mabao 68
Kutumiwa kwa Uwanja wa Sokoine na timu za Tanzania Prisons na Mbeya City umefanya uwe umeandaa idadi ya mechi 28 msimu huu ambazo ni mbili pungufu ya zile za Benjamin Mkapa unaoongoza kwa kuwa na mechi nyingi msimu huu.
Katika mechi hizo 28 zilizochezwa Uwanja wa Sokoine, idadi ya mabao iliyofungwa ni 68 huku mechi iliyokuwa na mabao mengi ni ile ambayo Geita Gold ilipata ushindi wa ,abao 4-2 dhidi ya Prisons.
CCM Liti-44
Baada ya kutoandaa mechi za Ligi Kuu kwa muda mrefu, safari hii wakazi wa Singida walipata fursa ya kuona idadi ya michezo 22 ya ligi kuu. Idadi ya mabao 44 ilifungwa katika Uwanja wa CCM Liti ambayo iliufanya ushike nafasi ya nne katika orodha ya viwanja vilivyokuwa na mabao mengi msimu huu.
Manungu Complex- Mabao 39
Msimu huu Mtibwa Sugar ilipata bahati ya kucheza mechi zake zote katika uwanja wake wa nyumbani wa Manungu Complex ambapo kabla ya mechi ya mwisho ilichezea hapo mara 14.
Nyavu za uwanja huo hazikuwa salama katika mechi hizo 14 kwani idadi ya mabao 39 ilipachikwa ikiwa ni wastani wa mabao 2.8 kwa mechi.
Uhuru-Mabao 37
Idadi ya mechi 21 zimechezwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambao mara kwa mara ulikuwa ukitumiwa na timu za KMC na Ruvu Shoting.
Mechi hizo 21 zilizochezwa katika Uwanja wa Uhuru, zimezalisha mabao 37 ambayo yanaufanya ushike nafasi ya sita katika chati ya viwanja vyenye mabao mengi.
Highlands Estates- Mabao 30
Ihefu SC imeutumia Uwanja wake wa Highlands Estates kwa mechi 13 za Ligi Kuu ya NBC msimu huu, na katika mechi hizo, idadi ya mabao 30 yalipachikwa.
Nyankumbu-Mabao 27
Unatajwa kama miongoni mwa viwanja vigumu zaidi kwa timu pinzani kupata matokeo mazuri na tangu Geita Gold ilivyopanda Ligi Kuu hadi sasa, imepoteza mechi mbili tu katika uwanja huo ambazo ni dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City.
Geita Gold imeutumia uwanja huo kwa mechi 11 za ligi msimu huu na katika mechi hizo, mabao yaliyofungwa ni 27.