Kuna kijana amekuwa akipigania falsafa ya uchumi wa soka (football economy), lakini amegeuka kuwa kichekesho kwa ‘watu wa mpira’ ambao hupenda zaidi watu wanaozungumza vitu vya kufikirika kuliko halisi.
Huyu kijana akitumia jukwaa la vipindi vya michezo redioni, anajaribu sana kueleza ni kwa nini suala la kiuchumi linapaswa kuzingatiwa katika kila mipango ya klabu na vyama vya mpira wa miguu, lakini kwa kuwa matokeo yake ni ya muda mrefu, hakuna anayemsikiliza.
Badala yake ‘watu wa mpira’ humzungumzia kwa kejeli kana anaota ndoto za Alinacha, yaani vitu visivyowezekana katika hali ya kawaida.
Hawa ni watu ambao ukiwaeleza kuwa mbona wenzetu huko barani Ulaya wanafanya kama huyu kijana anavyoeleza, huwa na majibu mafupi yasiyo na tafakuri ndani yake.
Kwamba ‘eti’ wale walishaendelea. Achana nao’. Kuachana nao maana mambo yaendelee kuendeshwa kiholela kwa kutegemea fikra na mipango ya kampuni kubwa zinazoleta fedha kwenye soka kama fadhila na si biashara.
Nadhani ni fikra kama hizo ndizo zinafanywa na wapangaji wa mashindano ya soka. Kwamba unatangaza tu mechi iwe Jumatano, bila kufikiria mambo yanayouzunguka mpira na hasa uchumi wake.
Wiki iliyopita Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza mikoa ya Arusha na Mwanza kuwa ndiyo itakayokuwa mwenyeji wa mechi za nusu fainali ya Kombe la Shirikisho linalodhaminwa na benki ya CRDB.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirikisho hilo, mechi ya fainali itafanyika Juni 3 kwenye Uwanja wa Kwaraa uliopo Babati.
Mechi hiyo itakutanisha mshindi wa mechi ya kwanza ya nusu fainali baina ya Azam FC na Coastal Mei 18 itakayofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na ya pili baina Yanga na Ihefu FC utakaofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Hii imekuwa ni kawaida kwa waandaaji wa mashindano hayo kutangaza viwanja vitakavyotumika katika mechi za hatua za mwisho siku chache baada ya timu zilizofuzu hatua hiyo kujulikana.
Kwamba Mei 4 na Mei 18 ni siku nyingi ambazo wadau wanaweza kuandaa shughuli zao zinazohusiana na soka kiasi kwamba siku hizo ziwe kama tamasha jijini Mwanza, Arusha na huko Babati.
Pengine kigezo kikubwa ambacho TFF inatumia ni uwanja mzuri unaoweza kutumika kwa mechi hizo muhimu za Kombe la CRDB, kigezo ambacho hakuna shaka kwamba ni muhimu sana kwa mchezo wa mpira wa miguu.
Lakini mikoa husika imejiandaaje na mechi hizo na imeshirikishaje wadau wake kuzipokea mechi hizo.
Yaani mechi hizo si kitu kidogo cha kupita mara moja, bali kuacha kumbukumbu za miaka na miaka kwa wanaohusika.
Kwamba mkoa unaweza kuandaa program zake za watoto ambazo zitahusishwa na maandalizi ya mechi hizo kama vile kliniki ambazo huhusisha wachezaji nyota wa klabu za Ligi Kuu.
Itakuwa ni kumbukumbu ya aina yake kwa mtoto mdogo mwenye ndoto ya kuwa nyota wa soka atakapohudhuria kliniki inayomuhusisha mchezaji anayemsikia redioni au kumwona kwenye televisheni kama Feisal Salum “Fei Toto” au Stephane Aziz Ki.
Kwa mchezaji kama huyo itakuwa ni kumbukumbu itakayomuongezea hamasa ya kucheza soka kufikia kiwango cha juu.
Lakini wafanyabiashara wa mkoa huo na ya jirani watawezaje kutumia fursa ya mechi kubwa kufanya biashara wakati imetangazwa ndani ya muda wa siku 12 tu.
Hata kampuni kubwa inakuwa vigumu kuanza kuvunjavunja bajeti zao ili ziweze kutumia fursa hiyo kwa ajili ya biashara zao.
Kampuni nyingi zikifuatwa wakati huu unaweza kukuta labda hazikujumuisha suala hilo katika bajeti zao ambazo mara nyingi hufanyika Aprili, wakati taasisi za serikali zinasubiri bajeti zao zipitishwe.
Wanaoweza kunufaika ni wale wauzaji wa bidhaa zinazoweza kuzalishwa harakaharaka bila ya mchakato mkubwa wa kutathmini ukubwa wa shughuli za soko linalozalishwa na mechi hizo.
Kwa hiyo zile jezi za kutundikwa mitini zitakuwa nyingi, lakini ni nadra kwa hoteli kubwa na sehemu za starehe na burudani kuanza kujitangaza eti kuvutia watu watakaoenda kushuhudia mechi hizo.
Ndio maana kwa wenzetu tangu siku ya kwanza klabu hujua mechi ya fainali ya mashindano ya vikombe itafanyika linin a mji gani.
Kwa Waingereza mechi hizo ni Uwanja wa Wembley tu, lakini nchi nyingine mechi hizo huhamishwa na yako mataifa ambayo yanataka mechi kama hizo za nchi nyingine zifanyike kwao, kama Marekani na Saudi Arabia.
TFF inaweza hata kuitaka mikoa ambayo inataka kuandaa mechi hizo iwasilishe maombi na mikakati yao ya kuhakikisha zitachezwa kwenye uwanja bora kabisa na jinsi zitakavyozinogesha.
Hii itasaidia wadau wote kuanza kujipanga mapema kwa ajili ya kuzifuata, kutumia fursa zinazozalishwa na mambo mengine ya kiuchumi.
Huko ndiko tunakotakiwa kwenda. Kwamba mipango iwe mapema kabisa ili fursa za kiuchumi zinazotengenezwa na mechi za mpira wa miguu zitumiwe vizuri na klabu na wadau wa mpira wa miguu.