Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viwango duni vya marefa,TFF iamke

Karia Wallace Rais Rais wa TFF, Wallace Karia

Sat, 23 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tanzania imekuwa nchi pekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kufuzu kushiriki fainali za ubingwa wa Mataifa ya Afrika (Afcon). Bila kujali namna ilivyofuzu, maana kwenye mpira matokeo ndiyo kila kitu, hili ni jambo la kujivunia sana.

Wakati vumbi la sherehe za kufuzu Afcon halijatulia, inatangazwa orodha ya waamuzi wa Afcon ambako tunaambulia patupu.Hakuna mwamuzi hata mmoja kutoka Tanzania atakayepuliza kipyenga pale Pwani ya Pembe (Ivory Coast) mwakani.

Tunapoongelea Tanzania katika mpira wa Afrika, tunaongelea nchi ambayo wananchi wake wanaupenda mpira wa miguu mpaka wanaumwa. Watanzania huwambii kitu kuhusu mpira wa miguu.Uongozi wa nchini sehemu ya wapenzi hao wa mpira wa miguu.Mpira wa miguu kwa Watanzania ni sehemu ya maisha. Kumbuka Ligi ya Tanzania inatajwa kuwa moja ya ligi bora barani Afrika.

Vinazopotajwa klabu 10 zenye wafuasi bora barani Afrika, klabu za Simba na Yanga haziachwi nje.Swali la kujiuliza hapa ni namna gani tutaendeleza mpira huu tunaoupenda bila ya kuwa na waamuzi wa viwango vya juu?

Huko nyuma nilibahatika kuwa kamishna na mtathimini wa mchezo katika mashindano ya CAF nikisimamia waamuzi mbalimbali. Ukweli usemwe, waamuzi wanaopewa nafasi na CAF wengi ni wasomi au wenye uelewa mkubwa na uwezo mkubwa wa kujieleza katika lugha zinazotumiwa na CAF.

Tulikaa kwenye vikao vya kabla ya mchezo (pre-match meeting) waamuzi waliweza kujieleza na kueleza kwa ufasaha mipango ya mchezo ulio mbele yao. Bila uwezo wa kuelewa au kujieleza katika lugha ni vigumu ukawa na uwezo wa kutafsiri sheria katika lugha hiyo.

Lengo hapa si kuwakatisha tamaa wasiojua kiingereza, hapana. Lengo ni kuwatia moyo waliokwisha kufanya uamuzi wa kuwa waamuzi wapambane sana katika kuongeza elimu hasa ya lugha. Kwa hapa kwetu angalau mwamuzi awe na uwezo wa kujieleza kwa kiingereza kama kweli ana ndoto za kuwa wa kimataifa.

Mwamuzi akienda mbele zaidi na kumudu lugha ya ziada kama kifaransa, kireno au kiarabu, itamwongezea nafasi ya kuangaliwa na kupewa nafasi kimataifa. Huo ndio ukweli kwa maana uamuzi ni kazi ya mawasiliano na watu na mawasiliano kufanyika na kutafsirika vizuri inahitajika sana lugha.

Ni vizuri ikaeleweka kuwa huwezi kuwa hakimu mzuri kama huwezi kumudu lugha. Hata kama una uelewa mkubwa wa suala unalolifanyia maamuzi, bado utakuwa na mtihani wa kuwaeleza wadau wakakuelewa kwa nini unafanya maamuzi unayoyafanya. Mwamuzi yeyote mwenye ndoto ya kuwa wa kimataifa ni muhimu akaweka juhudi kwenye lugha.

Tanzania imewahi kutoa waamuzi wazuri waliosifika barani Afrika kama kina Marehemu Hafidhi Ally na wengine. Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) linatakiwa likae na kutathmini juu ya nini kimetokea, nini mapungufu yetu na kutafuta suluhisho la sasa na la muda mrefu.

Mengi ya matatizo ya waamuzi ambayo huenda yanachangia viwango duni tumeyataja katika safu hii mara nyingi. Waamuzi kucheleweshewa posho zao au kulipwa posho kidogo, upendeleo katika upangaji wa waamuzi, kuwaingilia waamuzi katika utendaji wao na mengine mengi ambayo yako kwenye uwezo wa TFF kuyamaliza kama ikiamua.

Wakati TFF inashughulikia haya inatakiwa kwenda mbele zaidi kwa kujenga tasnia ya waamuzi wenye uelewa, nidhamu na weledi. Eneo la waamuzi si la kufanyia mchezo. Siyo eneo la kufuga waamuzi chawa watakaoitika ndiyo mzee na kutekeleza maagizo ya watu binafsi badala ya kuchezesha mpira kwa mujibu wa sheria 17 za mchezo.

Ni muhimu kukawa na utaratibu wa wazi na unaoeleweka wa jinsi ya kuwa mwamuzi.Vyama vya mikoa na wilaya viwe na taarifa hizo.

Shirikisho linatakiwa kuandaa mtaala wa mafunzo ya uamuzi ambao watapewa wadau wote kuanzia mashuleni, wilayani, mikoa hadi taifa.Hii itawezesha waamuzi kupata kozi zilizo sahihi kwa mujibu wa matarajio ya shirikisho.

Watoto pia wanaweza kufundishwa uamuzi hata kabla ya kufikisha miaka 14 inayowekwa na Fifa kama umri wa kufundisha waamuzi.Waamuzi waliojifunza tangu utotoni wanaweza kuwa wepesi kutafsiri sheria na pia wanakuwa na kiwango cha juu cha kujiamini.

Pamoja na kuweka taratibu za kufundisha uamuzi wilayani na mikoani, ni vizuri shirikisho likajenga uhusiano na taasisi mbalimbali hasa zile zinazotoa elimu ya juu au zile zinazofundisha walimu ili uamuzi wa mpira wa miguu uweze kufundishwa huko.

Ni kupitia taasisi hizi wanaweza kupatikana waamuzi wenye viwango vya kimataifa kwa sababu tayari wana mafunzo ya kozi nyingine na mtazamo wa kimataifa.Inawezekana sana wanafunzi wa stashahada au wale wa shahada wakapewa mafunzo ya ziada ya uamuzi katika muda wa ziada au wakati wa likizo.

Shirikisho liweke wazi madaraja ya waamuzi na ngazi wanazoweza kuchezesha. Utaratibu wa kupanda daraja pia uwekwe wazi kama ni kwa uzoefu au kwa mafunzo maalumu.Kozi za mafunzo ya kupanda daraja zitolewe bila upendeleo kama ambavyo pia uchaguzi wa waamuzi wa kuchagua waamuzi wa kuchezesha ngazi tofauti za mashindano.

Kwa mfano katika England waamuzi wanapoanza kozi za awali huwa daraja la 9, 8 mpaka 7 wakifundisha timu zisizo za ligi na za vijana kisha baada ya kuangaliwa kwa michezo isiyopungua mitano na mitihani pia wanaweza kupanda mpaka daraja la 6, 5 na 4 wakichezesha ligi za mikoa au ligi za chini (kama daraja la 3) za taifa na baada ya hapo mwamuzi anaweza kuendelea kwa kiwango cha daraja la 3, 2 na 1. Kwa hiyo mwamuzi kwenda mpaka kiwango cha FIFA anakuwa amepita utaratibu unaoeleweka.

Kwa mujibu wa Bodi ya Mpira wa Miguu (IFAB) ambayo ndiyo hutengeneza sheria za mpira kwa niaba ya FIFA, mwamuzi ndiye mtu mwenye wajibu wa kutafsiri na kuhakikisha utekelezaji wa sheria za mpira wakati wa mchezo.

Mwamuzi ni mtu mwenye mamlaka ya maamuzi ya mwisho kwa mambo yote yanayohusiana na mchezo. Nafasi ya mwamuzi ni ya muhimu kuliko nafasi yoyote katika mchezo wa mpira wa miguu.Kuamua kutochukulia waamuzi kwa umuhimu ni kuamua kutouchukulia mpira wa miguu kwa umuhimu.

Chanzo: Mwanaspoti