Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vivier: Tunahitaji ushindi kurejesha imani

Vivier Bahati Kesho Kocha Mkuu wa Biashara United, Vivier Bahati

Mon, 21 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kocha Mkuu wa Biashara United, Vivier Bahati amesema wanahitaji kushinda mchezo wa kesho dhidi ya Azam FC ili kurejesha imani ya mashabiki na kiwango chao walichokuwa nacho msimu uliopita wakimaliza kwenye nafasi ya nne.

Bahati amesema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza juu ya maadalizi ya mchezo huo utakaopigwa kesho Jumanne Februari 22, mwaka huu katika uwanja wa CCM Kirumba.

Mchezo huo ulipaswa kupigwa uwanja wa Karume mkoani Mara lakini ukahamishiwa jijini Mwanza kutokana na uwanja huo kuwa kwenye marekebisho.

Amesema baada ya kuondolewa kwenye michuano ya kombe la shirikisho na Yanga wamejipanga kikamilifu kupata ushindi kwenye mechi zao la Ligi Kuu wakianza na Azam kesho huku akikiri kiwango chao cha sasa hakilingani na walichokuwa nacho msimu uliopita na kuwaomba mashabiki kuendeleza uvumilivu.

Kocha huyo Mrundi amesema kwa sasa anaridhishwa na mabadiliko ndani ya kikosi hicho tangu alipokabidhiwa majukumu mapema mwaka huu ambapo kikosi kinacheza kwa maelewano, kujiamini, kutengeneza nafasi na kufunga mabao huku akisema bado kuna kazi kubwa ya kufanya kukiboresha zaidi.

"Tuko vizuri baada ya kupoteza FA tumejipanga mechi ya nyumbani tufanye vizuri, ni kweli hali ya timu kimatokeo siyo nzuri na tunahitaji kutafuta alama tuwe pazuri na kuifanya Biashara iwe sehemu nzuri, kiukweli ukitazama biashara ya msimu uliopita na sasa ni tofauti,"

"Tunaingia uwanjani kutafuta ushindi ili kuleta furaha hadi sasa naridhishwa na mabadiliko ya timu nahitaji tutafute nafasi na tufunge mabao, mabadiliko ya uwanja hayana athari kwetu Kirumba ni uwanja mzuri na ni kama nyumbani kwahiyo wachezaji wamejiandaa," amesema Kocha Bahati.

Nahodha wa timu hiyo, Abdulmajid Mangalo amesema awali kikosi kilikuwa kinakabiliwa na changamoto ya kutumia nafasi za mabao zilizokuwa zinatengenezwa huku akitamba kuwa wamejiandaa kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo.

 "Sisi wachezaji tumejiandaa vizuri tunatambua umuhimu wake kwa sababu utakuwa mchezo muhimu tumejiandaa kupambana tupate ushindi, hatuko vibaya sana tumekuwa tunatengeneza nafasi nyingi lakini hatupati bahati ya kufunga kwahiyo naamini mwalimu amekuwa akilifanyia kazi na bila shaka kuanzia mchezo huu tutaanza kuonyesha mabadiliko," amesema Mangalo.

Katibu Msaidizi wa chama cha soka mkoa wa Mwanza,  Khalid Bitebo amesema mashabiki watapata fursa ya kupata huduma ya chanjo ya Uviko-19 ambapo mashabiki 50 wa kwanza watakaochanja wataingia uwanjani bure kuushuhudia mchezo huo.

Viingilio vya mchezo huo ni Sh 5,000 jukwaani na 2,000 kwa mzunguko ambapo utakuwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu kupigwa uwanjani hapo kwa mwaka 2022.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz