Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viunzi vinne kocha mpya Simba SC

Steve Komphela ,, Steve Komphela

Fri, 7 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Simba ipo kwenye mazungumzo ya mwisho na Kocha Steve Komphela (56) kutoka Afrika Kusini ili arithi mikoba ya iliyoachwa na Mualgeria Abdelhack Benchikha siku chache kabla ya msimu kumalizika.

Kama kila kitu kitaenda sawa basi Komphela atatambulishwa kuwa kocha mkuu wa Simba kwa msimu ujao wa 2024/2025, licha ya kwamba anapingwa na baadhi ya viongozi wa juu wa timu lakini anaonekana kuwa na nafasi kubwa.

Komphela ni mzoefu wa soka la Afrika kwani amefundisha timu mbalimbali tangu mwaka 2002, lakini kubwa zaidi ni Kaizer Chiefs, Mamelodi Sundowns na timu ya taifa ya Afrika Kusini Bafana Bafana.

Msimu uliomalizika alikuwa na Lamontville Golden Arrows iliyomaliza nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Afrika Kusini.

Hata hivyo, kama atakuwa yeye au mwingine kuna mambo manne yanayomsubiri kocha mpya ndani ya Simba iwapo atakabidhiwa mikoba ya kukinoa kikosi hicho ambacho kilimaliza ligi chini ya kocha wa muda Juma Mgunda ambaye naye anapigiwa debe abaki.

Simba mpya

Kama Komphela ataajiriwa Simba au kocha mwingine, moja kazi atakayokuwa nayo kwenye kikosi hicho ni kutengeneza timu mpya kabisa.

Hii ina maana sehemu kubwa ya wachezaji wa Simba wataondoka baada ya baadhi kumaliza mikataba, lakini wengine wataachwa na kuuzwa, kutokana na wachezaji wengi msimu uliopita kuonekana kuwa chini ya kiwango hali ilyochangia timu hiyo ikose matokeo mazuri kwenye mechi zake.

Uongozi wa timu hiyo tayari umeshasema kuwa kuna wachezaji wataondoka kwenye timu hiyo na hivi karibuni itawatangaza pia kusajili wapya.

Hapo kocha mkuu atakuwa na kazi ya kuijenga timu hiyo upya bila kujali wachezaji atakaowasajili yeye ama atakaowakuta.

Mazingira ya kazi

Eneo lingine ambapo ni gumu kwa Komphela au kocha yeyote atakayetangazwa Simba ni mazingira ya kazi kutokana na historia ya nyuma.

Makocha wengi waliopita Simba wamekuwa wakilalamikia baadhi ya vitu kwenye timu hiyo kuwa vimechangia wao kushindwa kufanikiwa.

Mfano wapo wanaotamani kufanya kazi na wasaidizi wanaowataka wao lakini wanapata changamoto katika hilo kutokana na timu hiyo kuwa na bajeti ndogo na kuajiri makocha wengi kutokana nje.

Presha

Kila Mwanasimba anatamani kuiona timu hiyo inatwaa makombe msimu ujao baada ya kuyakosa kwa misimu mitatu mfululizo. Hiyo tayari ni presha kwa kocha mpya atakayetambulishwa Simba kwa kuwa mashabiki hawawezi kuvumilia kukosa ubingwa msimu wa nne mfululizo.

Kocha mpya ana kazi ya kurejesha furaha na kupunguza presha kwa wadau, wanachama na mashabiki wa timu hiyo ambao wamechoka kushuhudia watani wao Yanga wakitwaa makombe kila msimu, lakini wakiwa wanataka kuona timu hiyo inatimiza malengo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika angalau kufika nusu fainali.

Dabi

Jambo lingine ni Dabi ya Kariakoo. Mechi yenye mvuto na msisimko wa hali ya juu.

Kocha mpya wa Simba anakuja wakati timu hiyo ikiwa na kidonda kikubwa kutoka kwenye dabi. Imepoteza mechi mbili zote za ligi kwa msimu uliopita mbele ya mtani wake, Yanga na kubwa zaidi ilichapwa idadi kubwa ya mabao kwa jumla ya 7-2 kwenye mechi mbili za ligi.

Kocha atakutana na presha hii na kwa bahati mbaya mechi yake ya kwanza ya mashindano itakuwa dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii. Akishinda ataanza kurudisha imani kwa mashabiki wa timu hiyo bila kujali timu imechezaje.

Maoni ya wadau

Kocha wa zamani wa Simba, Patrick Aussems ‘Uchebe’ alisema ili kocha mpya wa timu hiyo afanye mambo yake kwa weledi anatakiwa kutimiziwa mahitaji yote.

“Kocha atakayekwenda Simba kabla ya kumhukumu wanapaswa kumtimizia matakwa yake yote. Wakifanya hivyo kisha akashindwa ndipo waanze kumlaumu,” alisema Aussems.

Nahodha wa zamani wa Simba, Masoud Nassor Cholo alisema timu hiyo inaweza kufundishwa na kila kocha lakini anatakiwa kupewa muda.

“Ujue hizi timu kubwa kila kocha anaweza kufundisha kama akiaminiwa na kupewa muda lakini shida ni kitakachotokea kwake, akifanya vizuri atasifiwa na akikosea ni ngumu kumvumilia hivyo anaweza kuja kocha mzuri akashindwa kutimiza malengo yake kwa kuwa timu haina uvumilivu.

“Kumekuwa na makocha wazuri wanafukuzwa lakini pia wale tunaowaona wa kawaida wanadumu na huo ndio mpira wetu ulivyo, naamini watapata kocha bora,” alisema Cholo

Kwa upande wa Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye naye amewahi kuichezea Simba na kuifundisha, amesema makocha wengi wana uwezo lakini shida ya timu nyingi za Afrika zimekuwa na kasumba ya kuhukumu mapema pia kutowaamini wazawa.

“Makocha wengi ni wazuri lakini hawapewi nafasi, wapo wanaopewa nafasi lakini hawapewi mahitaji yote muhimu pia hawaamini wazawa, hili ni janga la Afrika,” alisema Julio.

Chanzo: Mwanaspoti