Ligi Kuu England (EPL), imetoa baadhi ya wachezaji wabunifu wa safu ya kiungo katika soka kwa miaka mingi. Baadhi yao ni pamoja na Cesc Fabregas, David Silva, Juan Mata, Mesut Ozil na Santi Cazorla.
Kuwa na viungo wabunifu ni bonasi kubwa kwa kila timu. Wanasaidia katika kufungua safu ngumu zaidi za ulinzi na kutengeneza nafasi kwa wenzao.
Msimu unaoendelea wa Ligi Kuu England 2022-23, hauna upungufu wa wachezaji kama hao. Hivyo makala haya inawaangalia viungo wanne bora wabunifu zaidi katika ligi hiyo kwa sasa...
#4. Bernardo Silva - Manchester City
Wachezaji wachache sana katika Ligi ya England wanaweza kumshinda nyota wa Ureno na mchezaji wa Manchester City, Bernardo Silva katika suala la ufundi wa pande zote.
Kiungo huyo ameendelea kuwa mmoja wa viungo bora wa ligi tangu aliposajiliwa kwa kitita cha euro milioni 50 kutoka AS Monaco kwenda Manchester City mwaka 2017.
Ingawa Silva anajulikana sana kwa kiwango chake cha juu cha kazi na ustadi, Mreno huyo pia ana uwezo wa ajabu wa ubunifu.
Kiungo huyo wa kati wa Ureno hadi sasa anashika nafasi ya pili kwa asisti nyingi zaidi kwa kikosi cha Pep Guardiola msimu huu, nyuma ya Kevin de Bruyne, ambaye ana asisti tisa. Silva pia yuko katika nafasi ya nne katika chati ya pasi za mabao kwenye ligi, akiwa nazo tano.
#3. Martin Odegaard
Nahodha huyu wa Arsenal amekomaa taratibu na kuwa mmoja wa viungo wabunifu wa Ligi Kuu England, kulingana na kiwango chake msimu huu.
Martin Odegaard amekuwa kiungo muhimu wa timu ya vijana ya Mikel Arteta ambao wamekuwa moto kwenye ligi.
Nyota huyo wa Hispania ameweza kuboresha kiwango chake na kuwa mchezaji wa aina ya Mesut Ozil kutokana na uwezo wake wa kuona na kupiga pasi.
Amekuwa mchezaji aliyechangia mabao mengi zaidi kuliko mchezaji yeyote wa Arsenal kwenye ligi msimu huu baada ya kufunga mabao saba na kutoa asisti tano.
Odegaard pia yuko katika nafasi ya nne kwenye chati ya pasi za mabao katika ligi msimu huu, akiwa nazo tano. Pia alitawazwa Mchezaji Bora wa Ligi wa Desemba.
#2. Christian Eriksen
Mchezaji huyu wa kimataifa wa Denmark bila shaka ni mmoja wa wachezaji waliofanya vema katika usajili wa majira ya joto katika Ligi Kuu England msimu huu. Alijiunga na Manchester United baada ya kumalizika kwa mkataba wake kule Brentford.
Christian Eriksen amekuwa na mchango mkubwa kwa 'Mashetani Wekundu' hao kwani kwa sasa wako kwenye kinyang'anyiro cha kuwania mataji manne.
Kipengele kimoja cha mchezo wa Eriksen ambacho kimejitokeza katika msimu huu unaoendelea ni ubunifu wake. Kiungo huyo wa Denmark kwa sasa anajivunia kutoa pasi nyingi za mabao kuliko mchezaji yeyote wa Mashetani Wekundu kwenye mashindano yote (nane).
Pia kwa sasa anashika nafasi ya pili kwa asisti nyingi kwenye ligi (6), nyuma ya kiungo wa Manchester City, De Bruyne (9).
#1. Kevin de Bruyne - Manchester City
Mchezaji huyu wa kimataifa wa Ubelgiji anaendelea kuonyesha kiwango chake na kuthibitisha thamani yake kama mmoja wa viungo bora zaidi duniani.
De Bruyne anajulikana kwa uoni wake mzuri wa mpira na hivyo kumfanya aandikishe pasi nyingi za mabao katika maisha yake yote ya soka.
Kwa upande wa ubunifu, ni wachezaji wachache sana wanaoweza kushindana na nyota huyo wa Manchester City kwenye Ligi Kuu. Kiungo huyo kwa sasa anaongoza katika orodha ya watoa pasi za mabao kwenye ligi akiwa nazo tisa.
De Bruyne pia ana pasi 14 za mabao kwa jumla katika mashindano yote, jambo ambalo linamfanya kuwa mtoa pasi nyingi zaidi kwa timu ya Guardiola.