Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita yahamia ufungaji bora Championship

Vita Cham Vita yahamia ufungaji bora Championship

Sun, 18 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mabao mawili aliyofunga straika wa Mbeya City, Maulid Shaban katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Pan African yameamsha upya vita ya ufungaji bora kwenye Ligi ya Championship msimu huu.

Mbali na vita ya ufungaji bora, hekaheka ipo kwa vigogo wanaoongoza katika nafasi nne za juu ikiwa ni Ken Gold wenye pointi 50, Biashara United (49), Pamba Jiji (47) na Mbeya Kwanza wenye alama 45.

Hata hivyo, mechi zijazo za raundi ya 23, Ken Gold itakutana na Biashara United kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku Pamba Jiji ikiwaalika Mbeya Kwanza huko Nyamagana jijini Mwanza.

Mbeya City ambayo ilishuka daraja msimu huu leo ikicheza katika ubora wake iliwachana mabao 3-0 wapinzani hao na kubaki nafasi yao ya sita kwa pointi 36, huku Pan African wakisalia nafasi ya 15 kwa alama 15.

Katika mchezo huo City walicheza kwa kujiamini na kufanikiwa kupata mabao hayo, huku mawili yakifungwa na Shaban na kufikisha 11 hadi sasa akiweka vita mpya dhidi ya Boban Zirintusa (Biashara United) mwenye 13 na Wiliam Edgar anayeongoza kwa mabao 16, huku la tatu likifungwa na Andrew Kihumbi.

Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha msaidizi wa Mbeya City, Mathias Wandiba amesema kwa sasa hawaangalii matokeo ya wapinzani isipokuwa hesabu zao ni kushinda kila mechi iliyo mbele yao.

Amesema wanaamini katika michezo nane iliyobaki lolote linaweza kutokea ikiwa wanaoongoza nafasi nne za juu watakutana na kuna ambao watapoteza mechi zao na kuwapisha wengine.

"Kwa hiyo hatuwezi kukata tamaa kwani ligi haijaisha tunazo mechi nane zilizobaki hivyo lazima tuelekeze nguvu kwa michezo hiyo bila kuangalia wapinzani wamepata nini," amesema Wandiba.

Chanzo: Mwanaspoti