KATIKA mchezo wa Yanga dhidi ya Azam kwenye eneo la kiungo kulikuwa na bato kubwa ambalo lilifanya mchezo huo kuwa na kuvutia.
Eneo la kiungo Yanga alianza Yanick Bangala, Khalid Aucho na Feisal Salum ambao walikuwa wanakabana na viungo wa Azam, Paul Katema, Sospeter Bajana na Keneth Mguna.
Aucho alikuwa anacheza kwa chini sana akisaidiana na mabeki wakati Bangala yeye alikuwa anahusika katika kupeleka mashambulizi akisaidiana na Feisal.
Upande wa Azam, Katema alikuwa anacheza kwa chini sambamba na Sospeter huku Muguna yeye akiwa anasaidia mashambulizi kwenda mbele.
Hali hiyo ilifanya timu zote zikitumia zaidi kushambulia mawinga wao wa pembeni, Yanga wakimtumia beki wake Kibwana Shomari upande wa kushoto na kulia walimtumia Jesus Moloko.
Dakika 40 Fiston Mayele aliifungia Yanga baada ya Kibwana kuingia kwa spidi mpaka ndani ya boksi na kupiga krosi ya jui na Mayele aliimalizia.
Upande wa Azam wao walikuwa wanatumia zaidi upande wa kushoto ambao alikuwa anacheza Idd Seleman ambaye umakini wake ulikuwa mdogo.