Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita ya usajili GSM aitikisa Congo

GSM X Hesri Vita ya usajili GSM aitikisa Congo

Wed, 5 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga ilikuwa jijini Lubumbashi na juzi usiku walitakiwa kurejea nchini baada ya kumalizana na wenyeji wao TP Mazembe katika mchezo wa kukamilisha ratiba lakini kuna vita ya matajiri wawili ilikuwa inapigana kimyakimya jijini hapo.

Tuanze na Yanga ambao walisafiri na vigogo wao wazito kibao lakini tajiri wao namba moja Ghalib Said Mohamed anarejea na faili zito la usajili kwa mastaa ambao vijana wake wawili Rais wa Yanga injinia Hersi Said na makamu wake Arafat Haji walikuwa wakipambana nao kimyakimya.

Yanga inataka kusuka kikosi chao bora zaidi kwa msimu ujao na Mwanaspoti inafahamu kuwa tayari vigogo hao wanajua maeneo ambayo kocha wao Nasreddine Nabi licha ya kutokuwepo Congo lakini walishaweka sawa wapi kwa kuboresha.

Tayari kuna majina yasiyopungua manne vigogo hao watayawasilisha kwa tajiri wao ambaye kiu yake kubwa ni kutamani kuona Yanga inakuwa na mziki mnene utakaoendelea kusumbua miaka ya mbele.

Ingawa vigogo hao wamefanya siri lakini Mwanaspoti linafahamu Yanga imepiga hodi kwa klabu tatu nchini humo wakiwemo Mazembe wenyewe wakitaka kuchukua mashine mpya ndani ya timu hizo.

Mwanaspoti linafahamu kuwa moja ya eneo linalowatesa Yanga msimu huu ni kutokuwa na winga hatari anayejua kusababisha madhara kwa wapinzani ambapo msimu huu wamekuwa wakitegemea ubora wa Mkongomani Jesus Moloko pekee ambaye sasa anaandaliwa mkataba mpya.

Yanga pia inasaka kiungo mshambuliaji mwenye kasi anayejua kuharakisha mashambulizi lakini pia ubora wa kupiga mashuti wakianza kujiandaa na maisha mapya bila ya Feisal Salum 'Fei toto' ambaye bado hajarejea klabuni hapo.

KATUMBI NAYE AJIBU MAPIGO

Wakati Yanga wakijikusanya hivyo mpinzani wao Moise Katumbi ameumia kumkosa kocha Nasreddine Nabi katika msafara wa Yanga jijini Lubumbashi kwani kocha huyo ni kama amempiga chenga ya mwili tajiri huyo wa Mazembe.

Katumbi anamsaka Nabi akitaka arejee nchini humo kwa mara ya pili lakini sasa akimtaka ndani ya Mazembe kwenda kurudisha heshima ya timu hiyo lakini bado Nabi hajatoa msimamo wake juu ya ofa aliyopewa.

Mkataba wa Nabi na Yanga inaisha mwisho wa msimu huu na Katumbi aliamini kuwa Nabi kama angetua nchini humo basi angemsaka baada ya mchezo kisha kuweka sawa dili hilo lakini safari ya kocha huyo kurejea kwao Ubelgiji kusaka pasi mpya ya kusafiri ikawaokoa 'Wananchi'.

Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kuwa Katumbi ameanza mazungumzo na beki wa kulia wa Yanga Djuma Shaaban akitaka kumshusha Mazembe hesabu za Katumbi na makocha wake wanaona beki wao wa kulia kwa sasa mkongwe Djo Issama Mpeko makali yake yanazidi kupungua na mtu sahihi anayeweza kuvaa jezi yao kwa badala yake ni Djuma ambaye habari njema kwao mkataba wake unafikia ukingoni mwisho msimu huu ukimalizika.

Djuma amewaomba Mazembe kusubiri kidogo hadi msimu uishe huku Katumbi akimbana akitaka afanye maamuzi ya haraka akidai anataka kuanza kusuka kikosi chake haraka kabla ya kukipeleka Ulaya kwa maandalizi.

Chanzo: Mwanaspoti