Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita ya pointi Ligi ya Wanawake leo

JKT Queens Vs Abdijan Vita ya pointi Ligi ya Wanawake leo

Tue, 2 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Utamu wa Ligi ya Wanawake unaendelea leo kwenye viwanja vinne huku bingwa mtetezi JKT Queens ikitarajiwa kukipiga na Amani Queens kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi.

JKT ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo na pointi sita baada ya michezo miwili, ikishinda 4-0 dhidi ya Bunda Queens, kabla ya kuichapa Geita Gold bao 1-0 na huu ni wa tatu inayohitaji ushindi ili kujiwekea mazingira mazuri ya kutetea taji lao msimu huu.

Mchezo mwingine unaosubiriwa kwa hamu leo ni kati ya Alliance Girls iliyo nafasi ya nne na pointi zao sita dhidi ya Fountain Gate Princess iliyo nafasi ya tano na pointi tatu ukiwa ni mchezo wao wa pili kwenye ligi hiyo iliyoanza mwezi uliopita.

Baobab Queens ambayo imeanza vibaya ligi, ikipoteza michezo miwili ya mwanzoni, itavaana na Bunda iliyopoteza michezo yote miwili ya mwanzo.

Mechi nyingine inayotarajiwa kuwa kali ni Ceasiaa dhidi ya Geita Gold Queens, zote zikiwa hazina pointi.

Kocha wa Fountain, Masoud Juma alisema anaujua ubora wa Alliance na wataingia kwa kuiheshimu ili kupata pointi tatu.

"Mechi ya kwanza na Ceasiaa tulipata matokeo mazuri, lakini kuna makosa madogo tulifanya hivyo hatutaki yajirudie kwa kuwa mchezo ule umepita na tunahitaji pointi tatu."

Akizungumzia ugumu wa mechi yao na JKT, Kocha wa Amani Queens, Morice Katembo alisema changamoto za ukata wa fedha zinawashusha morali wachezaji lakini anaamini atapambana kuwaweka sawa ili wapate ushindi.

"Hadi leo (jana) asubuhi bado tupo Dar na mchezo unachezwa Lindi, tutapumzika saa ngapi na jioni mechi, kwa hiyo nitajitahidi kuwaweka sawa wachezaji ili nipate angalau pointi kwenye mchezo huu," alisema Katembo.

katika msimamo wa ligi, Simba Queens inaongoza ikifuatiwa na Yanga, kisha JKT na Alliance na zote nne zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa zikiwa zote na pointi sita.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live