Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita ya namba Stars usipime

73789 Stars+pic

Mon, 2 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Vita ya namba kwenye timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ huenda ikasababisha baadhi ya nyota kusotea benchi au kutopata uteuzi kikosini.

Mastaa hao huenda wakajikuta wakipoteza namba na wengine kutoteuliwa katika kikosi cha timu hiyo siku za usoni kutokana na viwango bora vinavyoonyeshwa na baadhi ya nyota wanaocheza kwenye nafasi zao.

Dalili za hilo zilianza kujionyesha mapema kwenye mechi za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (Chan), baada ya kipa Aishi Manula kupoteza namba mbele ya Juma Kaseja ambapo Stars ilicheza dhidi ya Kenya.

Kaseja alionyesha kiwango bora msimu uliopita akiwa na KMC ambapo alicheza michezo 18 bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa, kitu ambacho ameendelea nacho msimu huu, jambo linaloweza kumfanya awe chaguo la kwanza la kudumu mbele ya makipa Metacha Mnata na Beno Kakolanya.

Hata hivyo, Kaseja naye anapaswa kufanya kazi ya ziada kulinda nafasi yake kwani Kakolanya na Mnata wamekuwa wakionyesha viwango vizuri kwenye mechi za klabu zao Simba na Yanga.

Upande wa beki wa kulia kuna vita ya ushindani baina ya Shomary Kapombe wa Simba na Hassan Kessy wa Nkana FC ambayo inaingia mwaka wa tatu sasa.

Pia Soma

Advertisement   ?
Kapombe ambaye ameonekana kuanza kurejea kwenye makali yake, hapo awali ndiye alikuwa chaguo la kwanza lakini baada ya kupata majeraha mwaka jana, alipoteza nafasi hiyo kwa Kessy ambaye amekuwa chaguo la kwanza.

Lakini pia wawili hao wanapaswa kujichunga mbele ya beki Paul Godfrey ‘Boxer’ wa Yanga ambaye amekuwa akicheza vyema tangu alipopandishwa kikosi cha wakubwa cha timu hiyo. Pia kuna vita baina ya mabeki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Gadiel Michael wanaocheza upande wa kushoto.

Tshabalala ni mzuri zaidi katika kupandisha mashambulizi wakati Gadiel amekuwa akionyesha kiwango bora kwenye kuzuia na ushindani baina yao umesababisha hata ndani ya Simba kusiwepo aliyejihakikishia namba. Vita kubwa ipo kwenye nafasi ya kiungo mkabaji ambapo nahodha msaidizi, Himid Mao anaweza kujikuta akipoteza nafasi mbele ya Jonas Mkude au Ally Ng’anzi.

Mao anayechezea Enppi Club inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri ndiye anamiliki nafasi hiyo kwa muda mrefu kabla ya kuipoteza baada ya ujio wa kocha aliyetimuliwa Emmanuel Amunike na kiwango bora cha Mkude wa Simba na kinda Ally Ng’anzi anayetamba nchini Marekani kwenye timu ya Forward Madison FC.

Sifa kubwa ya Mao ni kukaba na kutibua mashambulizi ya timu pinzani, wakati Mkude ni kiungo anayeichezesha timu kuanzia nyuma, lakini wawili hao wana wakati mgumu mbele ya Ng’anzi ambaye anaweza kutimiza majukumu hayo yote mawili kwa wakati mmoja.

Lakini pia yupo kiungo wa Yanga, Abdulaziz Makame ambaye amekuwa fundi wa kutibua mipango ya wapinzani na kuwalinda mabeki wake. Lakini pia kuna ushindani kwenye nafasi ya kiungo namba nane baina ya Frank Domayo na Mudathir Yahya ambao wote wanachezea Azam FC.

Mudathir na Domayo wanasifika kwa uwezo wao wa kuunganisha vyema timu na kutengeneza uwiano wa timu uwanjani na pia kuanzisha mashambulizi.

Kuna vita nyingine kwa wachezaji wanaocheza nafasi za winga wa pembeni ambayo inawahusisha Iddi Seleman ‘Nado’, Hassan Dilunga, Thomas Ulimwengu na Farid Musa. Ulimwengu anayechezea JS Saoura ya Algeria na Farid wa CD Tenerife ya Hispania wamekuwa wakipata nafasi ya kucheza mara kwa mara, lakini kiwango bora cha Hassan Dilunga wa Simba na Nado wa Azam kinawaweka hatarini mastaa hao ikiwa hawatakaza buti.

Ukiondoa hao wachezaji wengine ambao wanatishia nafasi za mastaa kwenye kikosi cha Stars hapo baadaye ni mabeki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (LA Galaxy), Nickson Kibabage (Difaa el Jadida), Abdi Banda (Highlands Park), viungo, Mohamed Issah ‘Banka’ (Yanga), Abubakar Salum ‘Sure Boy’ (Azam) na washambuliaji Eliuter Mpepo (Buildcon) na Eliud Ambokile (TP Mazembe).

Akizungumzia vita ya namba Stars, beki wa zamani wa Simba na timu ya Taifa, Boniface Pawasa alisema ushindani huo ni ishara ya kukua kwa soka la Tanzania.

Chanzo: mwananchi.co.tz