Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita ya makipa Taifa Stars utamu kolea

Manula Beno Metacha Mshery Vita ya makipa Taifa Stars utamu kolea

Thu, 16 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' iko mazoezini kujiandaa na michezo miwili ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026.

Kazi ni pevu mazoezini, kwani kikosi kinaonekana kuwa ni kipana zaidi na maeneo mengi yana hazina ya mastaa.

Eneo ambalo limeibua gumzo kwenye siku hizi za kwanza za mazoezi ni kipa. Mijadala imekuwa mingi kwenye mitandao ya kijamii na hata mazoezini jijini Dar es Salaam.

Swali ni nani asimame kwenye ile milingoti pale Morocco kuitetea heshima ya Tanzania Jumamosi?

Lakini wakati mastaa wakikamilika kwa wale wanaocheza nje kuwasili vita ya kwanza inaonekana kuwa eneo la makipa.

Kocha Mualgeria, Adel Amrouche amewaita makipa watano ambao ni Aishi Manula (Simba) aliyerejea baada ya kuwa nje kwa majeraha, Metacha Mnata (Yanga), Benno Kakolanya (Singida), Aboutwalib Mshery (Yanga) na ingizo jipya kabisa Kwesi Kawawa (Karlslunden-Sweden).

Ukiondoa Kawawa ambaye ndio mara ya kwanza anajiunga na kikosi hicho, makipa wengine wote uwezo wao unajulikana na hawapishani sana kwa takwimu zao za kuwa langoni kuanzia klabu wanazozichezea na Stars.

Kuna ambao wamepitia panda shuka katika miezi ya karibuni lakini mashabiki kwa kiasi kikubwa wanatamani kuona kitu kipya kutoka kwa Kawawa ambaye hawamjui kabisa. Hata kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakimfurahia. 

Hebu tuwaone;

MANULA Amerudi mchezoni kwenye mechi dhidi ya Yanga ambayo timu yake ya Simba ilipoteza mabao 5-1. Ni kipa mkubwa ambaye Afrika inamjua na ana uzoefu mkubwa wa mechi za kuamua.

Alikuwa ndio chaguo la kwanza la Stars, lakini kwa mechi hii ya Niger bado sio rahisi kukaa langoni.  Hata ile inayofuata Novemba 21 hapa Dar es Salaam, bado hatakuwa vizuri kimchezo ila ni muhimu kuwepo kwenye timu uzoefu wake ni muhimu hata kwa ushauri na morali.

Changamoto yake kubwa ni kwamba bado hajarejesha hali ya kujiamini akihitaji muda zaidi kukaa langoni.

WENZAKE Presha itakuwa kwa makipa wanne waliobaki, Kakolanya, Kawawa, Metacha na Mshery ambao ubora watakaoonyesha mazoezini ndio utakuwa mtaji kwao kupata nafasi kwenye mechi hizo mbili au zaidi.

Makipa hao wanne yeyote atakayepata nafasi nyakati hizi atalazimika kuwa makini akijua makosa yoyote atakayofanya yatamweka kwenye wakati mgumu wa kuendelea kuaminika hasa kutokana na ubora wa wenzake watatu waliopo, pia kurejea kwa kipa namba moja.

TISHIO LA KAWAWA Mashabiki wengi wanataka kumwona kama yaliyomo yamo kwa vile ndio mara ya kwanza wanamsikia. Umbo lake linambeba langoni lakini hata kwa wenzake hapana shaka atakuwa tishio.

 Kipa huyo wa Karlslunden, kuanzia makipa wenzake, makocha na hata mashabiki wanasubiri kuona kama ataitumia kuamua safari yake ya kuiteka Stars au kujipoteza kupitia mechi hizo.

Kawawa ambaye alionyesha kujiamini kwa kuitwa kwake kwenye kikosi hicho anaweza kuwa changamoto mpya mbele ya Kakolanya na wenzake endapo atakuwa ameiva kuwashinda wenzake.

KWA NINI KAKOLANYA ATAANZA? Licha ya ushindani huo uliopo lakini Kakolanya ambaye alikuwa chaguo la kwanza kabla ya kurejea kwa Manula na Mshery na ujio wa Kawawa, kipa huyo wa Singida Big Stars anapewa nafasi ya kwanza kuendelea kuaminika langoni.

Kakolanya licha ya kulaumiwa katika moja ya mabao ambayo alifungwa kwenye mchezo dhidi ya Sudan atahitaji kubadilika ili kujihakikishia nafasi ambayo inawindwa na wenzake.

Ni kipa ambaye ukilinganisha na wenzake waliopo kikosini kwa sasa amecheza mechi nyingi na ana hali ya kujiamini kwa lolote kama hatapata tatizo lolote la kiafya kabla ya Jumamosi. 

Aishi kisaikolojia hayupo na ndio maana hata kwenye mechi na Namungo hakuchezeshwa, lakini Mshery bado hajarudi mchezoni. Metacha ni mzoefu lakini hajakaa langoni sikunyingi, kiushindani si faida kwake wala kwa Taifa kwenye mechi kama hizi.

Presha nyingine mbele ya makipa hao ni kuwa karibu kwa Fainali za Afcon zitakazofanyika mwakani nchini Ivory Coast ambapo makocha hao wanaanza kusaka makipa ambao wataungana nao kwenda kwenye mechi hizo zitakazoanza Januari.

Makocha wa Stars wamebakiza siku tatu pekee za kuamua nani watamuamini langoni tusubiri kuona kipa yupo atakuwa langoni Jumamosi watakapokutana na Morocco.

Ni mechi mbili ambazo zitaonyesha picha halisi ya Tanzania kwenye eneo hilo la kipa. Je, ataanza Kakolanya kweli au Kawawa atalisapraizi Taifa?

Chanzo: www.tanzaniaweb.live