Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita ya kisasi Simba, Jwaneng ipo hapa

Ahmed Ally Awatetea Mastraika Simba .jpeg Vita ya kisasi Simba, Jwaneng ipo hapa

Sat, 2 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwa maneno rahisi kabisa. Leo ni vita ya kisasi Kwa Mkapa. Simba imepania kwa namna yoyote ile kuwang’oa Jwaneng Galaxy ya Botswana ya kutinga robo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Jwaneng msimu wa 2021, siku ya Jumapili ilitibua mambo baada ya kuichapa Simba mabao 3-1 katika mchezo wa kufuzu makundi Ligi ya Mabingwa na kutolewa kwa mabao ya ugenini, baada ya sare ya jumla ya 3-3 kutokana na kushinda 2-0 kwenye mechi ya kwanza Gaborone.

Simba wanataka kufuta aibu hiyo kwa kulipa kisasi leo saa 1 jioni. Wamesisitiza hakuna namna yoyote ambayo watakubali kuwa nje ya robofainali na kuvumilia kelele za Yanga ambayo kabla ya jana walishafuzu.

Kama Simba itafanikiwa kuungana na Yanga kwenye robo itakuwa rekodi ya aina yake kwenye soka la Tanzania na Afrika Mashariki kwa watani wa jadi kutinga hatua hiyo kwa pamoja.

Kufuzu ni kupata ushindi huku ikiungana na Asec Mimosas ya Ivory Coast ambayo ilijihakikishia mapema kutinga hatua hiyo pamoja na uongozi wa kundi B.

SIMBA IMEZOEA ROBO

Kimpira sio jambo rahisi lakini historia ya Simba katika Ligi ya Mabingwa msimu wa 2018/2019 na uliopita, pia katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021/2022 inawapa wengi matumaini wawakilishi hao wa Tanzania leo wataitoa nchi kimasomaso kwa kutinga robo fainali na kuungana na Yanga ambayo ilifanya hivyo tangu wiki iliyopita.

Msimu wa 2018/2019 ikihitaji ushindi katika mechi yake ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba iliichapa AS Vita Club ya DR Congo kwa mabao 2-1 na kusonga mbele na msimu uliopita ilionyesha jeuri kwa kuichapa Horoya ya Guinea kwa mabao 7-0.

Ikaja kufanya hivyo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021/2022 ilipoitandika USGN ya Niger kwa mabao 4-0 na kuingia robo fainali.

Kanuni ya kutumia matokeo ya mechi baina ya timu mbili kuamua mshindi pindi zinapolingana pointi, ndio inailazimisha Simba kupata ushindi leo ili isonge mbele kwani itafikisha pointi tisa ambazo Wydad inaweza kuzipata pia kama itaibuka na ushindi wa nyumbani dhidi ya Asec Mimosas lakini Simba ina faida kwani yenyewe ilipata matokeo mazuri zaidi ya timu hiyo ya Morocco pindi zilipokutana, ikifungwa bao 1-0 ugenini na yenyewe ikipata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani.

ISHARA NZURI

Takwimu za timu hizo mbili kwenye mechi za kundi hilo, kwenye makaratasi zinaiweka Simba katika nafasi nzuri ya kupata ushindi ingawa hilo sio lazima litokee ndani ya dakika 90 za mchezo.

Kama Simba itatumia vyema udhaifu wa wapinzani wao ulioonekana katika mechi zilizopita, basi mambo yanaweza kuwa mazuri kwa mwakilishi huyo wa Tanzania.

Jwaneng Galaxy inayoshika mkia katika kundi hilo ikiwa na pointi nne, imekuwa na safu dhaifu ya ulinzi ambayo katika mechi tatu zilizopita za hatua ya makundi imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa kila mechi.

Licha ya kutoruhusu bao katika mechi mbili za mwanzo dhidi ya Wydad na Simba, ilijikuta ikifungwa mabao 2-0 nyumbani na Asec Mimosas kisha ziliporudiana ikafungwa mabao 3-0 na katika mechi ya juzi ikafungwa bao 1-0 na Wydad.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Jwaneng, Simba yenyewe safu yake ya ulinzi imeruhusu mabao mawili tu katika mechi tano za kundi hilo na bao la kwanza ilifungwa dhidi ya Asec Mimosas kwenye mechi ya kwanza na lingine ikafungwa dhidi ya Wydad kwenye mechi ya tatu.

Ubutu wa safu ya ushambuliaji ya Jwaneng Galaxy unaweza kuipa Simba tumaini lingine katika mechi hiyo ambayo ushindi wa aina yoyote utaifanya itinge hatua ya robo fainali pasipo kuathirika na matokeo ya mchezo baina ya Wydad na Asec Mimosas.

Katika mechi tano za hatua ya makundi, Jwaneng Galaxy imefunga bao moja tu ambalo ilipata katika mechi ya kwanza dhidi ya Wydad na baada ya hapo imecheza mechi nne mfululizo pasipo kufunga bao hivyo ina wastani wa bao 0.2 kwa mechi.

Simba nayo inaonekana kutokuwa tishio kwa ufungaji ingawa angalau ina namba nzuri kulinganisha na Jwaneng Galaxy kwani imefunga mabao matatu katika mechi tano ikiwa ni wastani wa bao 0.6 kwa mechi, mabao yote ikiwa imeyapata katika mechi ilizocheza uwanja wa nyumbani.

REFA HANA MZAHA

Mechi hiyo ya Simba na Jwaneng Galaxy itakuwa chini ya usimamizi wa refa Daniel Nii Laryea kutoka Ghana.

Ni refa ambaye kuchezesha mechi moja ya Simba ambayo ilikuwa ni ya ugenini dhidi ya RS Berkane kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Februari 27, 2022 ambayo Simba ilipoteza kwa mabao 2-0, pia kwenye michuano ya Afcon 2023 alichezesha mchezo kati ya Tunisia na Mali.

Laryea mwenye umri wa miaka 36, katika mechi 21 za mashindano ya klabu Afrika ambazo amechezesha, ametoa kadi 79 na nyekundu ni tatu na za njano ni 76.

UTEMI NYUMBANI

Simba ina rekodi na takwimu bora kwenye mashindano ya klabu Afrika pindi inapocheza nyumbani, jambo ambalo linaweza kuchangia iwe na ari kubwa katika mechi dhidi ya Jwaneng.

Hilo linaweza kujionyesha katika mechi 10 zilizopita za kimataifa ambazo Simba ilikuwa nyumbani na imepata ushindi mara sita, kutoka sare tatu na kupoteza moja huku ikifunga mabao 18 na yenyewe imefungwa mabao saba tu.

Wakati Simba ikiwa tishio nyumbani, Jwaneng Galaxy imekuwa haina namba nzuri za kuibeba ugenini na katika mechi 10 zilizopita, imepata ushindi mara mbili tu na kupoteza mechi nane, ikifunga mabao nane na yenyewe nyavu zake zimetikiswa mara 19.

USHINDI UPO HAPA

Hapana shaka kocha Abdelhak Benchikha ataingia na mfumo wa 4-2-3-1 ambao amekuwa akiutumia mara kwa mara kwa lengo la kuifanya timu iwe na balansi nzuri katika kushambulia na kuzuia.

Kikosi cha Simba katika mechi ya leo kinaweza kuundwa na Ayoub Lakred, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Enock Inonga, Che Fondoh Malone, Babacar Sarr, Clatous Chama, Fabrice Ngoma, Omary Jobe, Sadio Kanoute na Saido Ntibazonkiza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live