Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita ya Diarra, Manula ni hii..

Makipa Pic Aishi Manula(Kushoto) na Djigui Diarra (Kulia)

Sun, 14 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Makipa hao mbali ya kuongoza kwa kucheza idadi kubwa ya michezo katika raundi hizo tano za mwanzo, pia wamekuwa na ubora wa kiufundi ambao unaonekana kuwatofautisha na makipa wengi wa timu nyingine 14 zilizopo Ligi Kuu Bara msimu huu.

Manula anayeshiklilia tuzo ya Kipa Bora kwa misimu mitatu mfululizo, ikiwamo ya msimu uliopita ndiye kinara wa kucheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao ambapo hajaruhusu nyavu zake kutikiswa katika mechi zote tano ambazo Simba imecheza dhidi ya Biashara United, Dodoma Jiji, Polisi Tanzania, Coastal Union na Namungo.

Diarra anamfuatia kwa karibu Manula kwani katika mechi tano alizoichezea Yanga, ameruhusu bao katika mechi moja tu dhidi ya Ruvu Shooting, huku nyavu zake zikiwa hazijaguswa katika michezo minne waliyoumana na Kagera Sugar, Geita Gold, KMC na Azam FC.

Makipa hao wamekuwa na sifa nyingi zinazoelekea kufanana huku wakitofauti ubora katika maeneo machache ambayo kama kila mmoja atayaimarisha anaweza kuwa bora na tishio zaidi sio tu Tanzania bali Afrika kiujumla.

Sifa ambazo wawili hao wanaonekana kufanana ni utulivu na uwezo wao wa kulimiliki lango na eneo la hatari, mawasiliano mazuri na safu yao ya ulinzi na kusoma mchezo na timu pinzani, makadirio mazuri pindi wanaposhambuliwa pamoja na uwezo wa kudaka mipira ya juu na chini pamoja na uanzishaji mzuri wa mipira. Pia ni wazuri kwa kuchezea mipira kwa miguu wakati wakitengeneza mashambulizi ya timu zao.

Kocha wa makipa wa kituo cha soka kwa vijana wadogo cha Magnet, Abel Mhagama alisema kubwa linalowatofautisha Manula na Diarra ni ukomavu wa kiakili walionao.

“Diarra na Manula huwa hawatolewi mchezoni kirahisi pindi wanapofungwa bao au kufanya makosa. Ni watu ambao wakifanya makosa hawatetemeki na kutetereka. Ni viongozi wazuri wa mabeki na timu kiujumla.

Huwa hawacheleweshi muda kwa kujilaza chini kila wakati au kujifanya wameuamia pindi timu zao zinapokuwa zinaongoza. Wana uwezo wa kudaka mipira na hawatemi ovyo,” amesema Mhagama.

Hata hivyo, licha ya kila mmoja kuwa na uwezo wa kuanzisha mipira, Manula na Diarra wanatofautiana kwa aina ya uanzishaji wao mipira ambapo kwa mujibu wa kocha Mhagama, mmoja ana uwezo wa kupiga pasi za mbali na mwingine fupi.

“Diarra ni mzuri wa kupiga pasi fupi za ndani ya yadi 50 na kucheza pamoja na timu wakati Aishi ana uwezo wa kupiga mipira mirefu ya juu kwa kutumia miguu yote miwili,” amesema Mhagama.

Kipa wa zamani wa Simba, Steven Nemes alisema ushindani wa makipa uliopo baina ya Diarra na Manula, unawapa kazi ngumu mastraika kujiuliza mara mbili mbili namna ya kuzifumania nyavu zao.

“Ukiona watu wanawalinganisha makipa hao, basi wana vitu vya aina yake vyenye mvuto kwenye macho ya wadau, ukiachana na hilo ushindani wao ni chachu kwa makipa wengine kujituma ili kuwa na kitu cha kujivunia kwa msimu huu,” alisema.

Alisema nje ya Diarra na Manula kuna makipa wengine ambao anawaona wameanza vizuri ligi kama Mathias Kigonya wa Azam, Metacha Mnata (Polisi Tanzania), Mussa Mbissa (Coastal Union), Haroun Mandanda (Mbeya City), Mohamed Makaka (Ruvu Shooting) na wengine. Tofauti na msimu uliopita, Mbissa safari hii amekuwa imara zaidi na kuepuka ile aibu ya kucheza mechi 23 na kuruhusu mabao 58 akiwa na Mwadui iliyoshuka daraja kabla ya kusajiliwa Coastal.

Mnata aliyepo pia timu ya taifa, Taifa Stars na Makaka wamekuwa imara katika kuokoa michomo ya hatari wakichupa kiufundi, pia ni makini katika kulinda lango na kupanga mabeki wake, sambamba na kuanzisha mashambulizi kwa timu zao, kitu ambacho wengine hawana ukiondoa Manula na Diarra. Pia Kocha wa Azam Kigonya ukiacha papara yake ya kutoka bila hesabu, ni mzuri wa kuokoa hasa shambulio la ana kwa hana na pia kupanga mabeki wake na kufanya akomae na kina Manula na Diarra.

Kocha wa Makipa wa KMC, Fatuma Omary amesema ushindani uliopo kwa makipa wa ligi msimu huu, unasaidia kuongeza umakini kwa washambuliaji kutafuta mbinu jinsi ya kuwafunga.

“Ligi kuu ya msimu huu kwa ujumla wake ni ngumu, upande wa makipa nje na hao wa Simba na Yanga, nawaona wengi wapo vizuri na imara, hii inatafsiri namna ambavyo soka linazidi kukua,” amesema.

Kwa upande wa kipa wa zamani wa Yanga, Benjamin Haule alisema anafurahishwa kuona ushindani unakuwa mkali kuanzia kwa makipa hadi washambuliaji na kwamba itasaidia ligi kuwa ngumu na ya kiushindani.

“Ni raha sana kuona kila eneo hakuna urahisi, kwamba straika anapofunga bao anaonekana kutumia akili, kipa akipangua anaonekana anatumia akili, hii ligi ya msimu huu siyo mchezo kabisa,” amesema.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz