Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita kwenye Kariakoo Derby iko hapa

Kariakoo Dabi Vita kwenye Kariakoo Derby iko hapa

Sat, 4 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakinogesha mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga, ni ushindani wa wachezaji kulingana na nafasi wanazocheza ambapo mara kwa mara wale wa upande mmoja hupambana ili wawafunike wale wa upande wa pili.

Na hicho ndicho kinategemewa kuonekana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya timu hizo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumapili, Novemba 5 kuanzia saa 11 jioni.

Gazeti hili linakuletea baadhi ya vita za kuonyesha nani zaidi kiuwezo ambazo zinategemewa kuonyeshwa na baadhi ya wachezaji wa Yanga na Simba wakati timu zao zitakapoumana hiyo Jumapili ambazo kwa kiasi kikubwa zinaonekana zinaweza kuamua matokeo ya mchezo.

Kanoute, Ngoma vs Nzengeli, Aziz Ki, Pacome

Viungo watatu wa Yanga, Pacome, Aziz Ki na Nzengeli kwa pamoja wamefunga mabao 14 kati ya 20 ambayo timu hiyo imefunga hadi sasa kwenye ligi kuu.

Na ni mchezo mmoja tu wa ligi ambao hakuna kati yao ambaye alifunga bao lakini mingine sita, ama mmoja, wawili au wote watatu walifunga bao/mabao.

Katika mabao hayo 14, Aziz Ki ndiye kinara akiwa amefumania nyavu mara sita akifuatiwa na Nzengeli aliye na mabao matano huku Pacome akiwa amefunga matatu.

Nzengeli pia yumo katika orodha ya nyota waliopiga pasi nyingi za mabao katika Ligi Kuu hadi sasa wakiwa na pasi za mwisho mbili huku Pacome na Aziz Ki kila mmoja akiwa nayo moja.

Hapana shaka Sadio Kanoute na Ngoma wa Simba watakuwa na dakika 90 ngumu za kuhakikisha watatu hao hawafui dafu dhidi yao.

Lakini hata nao Nzengeli, Pacome na Aziz Ki wanapaswa kuwachunga vilivyo Kanoute na Ngoma ili kuwadhibiti wasipate fursa ya kuichezesha Simba kwani wawili hao wamekuwa bora katika kupiga pasi zinazoipeleka timu mbele.

Aucho vs Chama, Ntibazonkiza

Simba imekuwa ikiwategemea sana Saido Ntibazonkiza na Clatous Chama katika kutengeneza nafasi na kufanya mijongeo ya kufungua mianya kwa wapinzani ili itumie kufunga mabao yake.

Siku ambayo wawili hao wanakuwa bora ni vigumu kuona Simba ikipoteza mchezo au hata kutoka sare na mara nyingi huibuka na ushindi.

Na hata katika kufunga, wawili hao hawako nyuma kwani hadi sasa wamshaifungia Simba mabao manne katika Ligi Kuu ambapo kila mmoja amefunga mabao mawili na Chama amepiga pasi moja ya mwisho.

Kazi kubwa itakuwa kwa Khalid Aucho kuhakikisha wawili hao hawaleti madhara kwao.

Na Ntibazonkiza na Chama nao watakuwa na shughuli ya kuhakikisha hawampi uhuru Aucho wa kuichezesha yanga na kuipa balansi nzuri ya kuzuia na kushambulia kama ambavyo amekuwa akifanya katika michezo yao mingi tangu alipojiunga nao.

Tshabalala vs Yao

Baada ya kukutana katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021/2022 kisha wakakutana tena katika mechi ya ngao ya jamii mwezi Agosti jijini Tanga, Yao Attohoula Kouassi na Mohammed Hussein 'Tshabalala' watahamishia tena vita baina yao kwenye mechi ya watani Jumapili hii.

Tshabalala anayecheza nafasi ya beki wa kushoto kwa Simba ni mzuri katika kushambulia kama ilivyo kwa beki wa kulia wa Yanga, Yao Kouassi ambaye ndio kinara wa kupiga pasi za mwisho katika Ligi Kuu hadi sasa akiwa nazo nne.

Na hapo katika kupiga pasi za mwisho, Tshabalala hajaachwa mbali kwani na yeye hadi sasa ameshatengeneza pasi mbili za mabao katika mechi sita ambazo Simba imecheza kwenye Ligi Kuu.

Katika mchezo huo wa dabi, kila mmoja atakuwa na jukumu la kuhakikisha mwenzake hapati nafasi ya kupeleka hatari langoni mwa lango lake lakini pia kuhakikisha anamimina majalo ya kusaidia timu yaks na atakayefanikiwa kuwa bora zaidi ataiweka timu yake katika uwezekano mkubwa wa kuibuka na ushindi.

Lomalisa vs Kapombe

Wote ni wazuri katika kusaidia mashambulizi ma pia wanamudu vyema kutoa mchango katika ulinzi.

Katika kusaidia mashambulizi, Kapombe tayari ameshapiga pasi mbili zilizozaa mabao wakati Lomalisa yeye ana pasi moja.

Upande wao kutakuwa na vita ya kila mmoja kuhakikisha mwenzake hafurukuti.

Baleke vs Job, Bacca

Jean Baleke ni mshambuliaji ambaye amekuwa akitumia vyema umbile lake kuwanyima uhuru mabeki wa timu pinzani lakini safari hii anakutana na mabeki wawili ambao hawakubali kushindwa kirahisi, Bacca na Job.

Mzize vs Inonga, Malone

Mshambuliaji ambaye hana masihara pindi mabeki wa timu pinzani wanapofanya makosa, Clement Mzize atakuwa na kibarua cha kuwalazimisha walinzi wawili wenye matumizi makubwa ya akili, Enock Inonga na Malone Fondoh kufanya makosa ili ayatumie kuipatia Yanga ushindi.

Katika Ligi Kuu hadi sasa, Mzize hajafunga bao lolote lakini ameifungia Yanga mabao matatu katika mechi nne za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu walizocheza dhidi ya ASAS ya Djibouti na El Merrikh ya Sudan.

Simba

Ally Salim, Kapombe, Tshabalala, Malone, Inonga, Kanoute, Kibu, Ngoma, Baleke, Chama na Ntibazonkiza.

Yanga

Diarra, Yao, Lomalisa, Bacca, Job, Aucho, Nzengeli, Mudathir, Mzize, Pacome na Aziz Ki.

Chanzo: Mwanaspoti