Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita iko hapa! Mtamkaba nani, mtamwacha nani?

Simba Yanga Vita iko hapa! Mtamkaba nani, mtamwacha nani?

Sat, 15 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wikiendi hii Dar es Salaam itasimama. Mastelingi watakuwa,Robertinho wa Simba na Nasreddine Nabi wa Yanga. Watakuwa mstari wa mbele kuwapa raha na kujibu maswali ya mashabiki wa soka ya nani zaidi baina ya timu hizo zenye ubishani mkubwa mitaani.

Kwa hali ilivyo ndani ya vikosi hivyo na fomu za wachezaji kwa sasa, ni wazi swali kila mmoja anajiuliza nani atamkaba nani? Mtihani wao mkubwa ni kuandaa mpango mkakati wa kudhibiti mastraika na viungo washambuliaji wa timu pinzani wakati miamba hiyo miwili itakapokutana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jumapili kuanzia saa 11:00 jioni.

Uwingi wa nyota wa nafasi hizo ambao wanafanya vyema kwa sasa, unafanya kuwe na ugumu kwa upande kubashiri akina nani wanaweza kutumika katika upande wa kushambulia kwa kila timu katika mechi hiyo jambo ambalo hapana shaka litawafanya Nabi na Robertinho kujikita zaidi na maandalizi ya kudhibiti upande wa pili kitimu badala ya kujiandaa kukabili mchezaji mmojammoja.

Simba na Yanga kila moja ina wachezaji saba wa nafasi za ushambuliaji ambao benchi la Robertinho na lile la Nabi yanaweza kupanga yeyote kati ya hao na kusiwe na shaka ya ufanisi wa kutengeneza nafasi na kufunga mabao. Upangaji wa kikosi hautabiriki kutokana na fomu za mastaa hao.

Machaguo saba ya Nabi katika eneo la mbele kwenye mchezo huo ni Fiston Mayele, Kennedy Musonda, Clement Mzize, Bernard Morrison, Stephane Aziz Ki, Jesus Moloko na Tuisila Kisinda ambaye ana rekodi na mechi hizo.

Mayele ndiye kinara wa ufungaji Ligi Kuu akiwa na mabao 16, wakati Musonda ameonyesha moto katika Kombe la Shirikisho Afrika akifunga mabao matatu kwenye hatua ya makundi na Clement Mzize amepachika mabao manne katika ligi.

Moloko amefumania nyavu mara mbili na kupiga pasi nne za mwisho huku Morrison akiwa amerudi kwa kasi kwa kufunmga katika mechi iliyopita dhidi ya Kagera Sugar.

Ingawa amekuwa hafungi, Kisinda mwenye mabao mawili, kasi yake imekuwa ikiwasumbua mara kwa mara walinzi wa Simba na Aziz Ki ameonyesha uwezo wa kufunga mabao akifanya hivyo mara nane katika ligi na kupiga pasi za mwisho ambapo anazo nne.

Kwa upande wa Simba inayojiandaa na mechi ya robofainaliya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Waydad Casablanca, majembe saba ambayo yamekuwa mwiba kwa safu za ulinzi za timu pinzani msimu huu ni Jean Baleke, Clatous Chama, Moses Phiri, Kibu Denis, Pape Sakho, John Bocco na Saido Ntibazonkiza.

Baleke ndio amekuwa hashikiki zaidi kwa siku za hivi karibuni ambapo amefunga mabao 11 katika mechi tano mfululizo za Simba katika mashindano matatu tofauti ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam.

Phiri licha ya kutofunga kwa muda mrefu, ni tisho la kufunga kwani ndiye anashika nafasi ya pili kwa ufungaji katika ligi akiwa na mabao 10 akiwa sawa na Ntibazokiza ambaye ndiye mchezaji aliyehusika na mabao mengi zaidi msimu huu kwani amepiga pasi za mwisho tisa na silaha nyingine inayowafuatia ni Bocco aliyefunga mabao tisa.

Kasi na uwezo mkubwa wa kupiga chenga pamoja na kufunga mabao, unamfanya Pape Sakho awe silaha nyingine inayotegemewa na Robertinho lakini kuna Kibu Denis ambaye uwezo wake wa kukaba kuanzia mbele umekuwa silaha ya Simba kuwanyima uhuru mabeki wa timu pinzani kuanzisha mashambulizi kutokea nyuma.

Simba wanayo silaha nyingine ambayo ni kiungo mshambuliaji Clatous Chama aliyeonyesha uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho akiwa amefanya hivyo mara 14 na ndiye kinara wa chati ya waliofanya hivyo hadi sasa.

Kutokana na uwepo wa wachezaji hao, Nabi na Robertinho kila mmoja anaweza kuanza na mshambuliaji mmoja wa kati, wawili au hata watatu kutegemeana na aina ya maandalizi waliyofanya kwa ajili ya mechi hiyo.

Kocha wa Rhino Rangers ya Tabora, Athuman Bilali 'Billo' alisema kuwa pamoja na kiwango bora kilichoonyeshwa na wachezaji hao, vikosi vinaweza kuja kwa sura tofauti.

"Hizi mechi kubwa huwa zina mambo ya kushangaza na huwa za tofauti kabisa. Mchezaji anayeonekana yuko vizuri anawza kutofanya vyema na akaja kutamba mchezaji ambaye kwa wakati huo anaonekana hajawa na kiwango kizuri.," alisema Bilali.

Beki wa zamani wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema mechi baina ya timu hizo huwa hazitabiriki.

"Hizi ni mechi ambazo zinakuwa na maandalizi ya tofauti kabisa ambayo hufanya baadhi ya wachezaji hadi kucheza kwa hofu na kushindwa kuonyesha walichonacho na inahitaji ujasiri mkubwa sana kucheza kwani presha inakuwa kubwa sana," alisema Cannavaro.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: