Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita 7 Singida FG vs Simba

Simba Vs Singida.jpeg Vita 7 Singida FG vs Simba

Wed, 10 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Saa chache zimesalia kabla kuona mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi kati ya Singida Fountain Gate dhidi ya Simba SC.

Wakati mchezo huo utakaoanza saa 2:15 usiku ukisubiriwa kwa hamu kuna vita saba zitaubeba mchezo huo wa nusu fainali ya pili na ya mwisho kwa msimu huu.

Che Malone vs Elvis Rupia

Beki wa Simba Che Malone Fondoh na mwenzake Kennedy Juma kama Kuna kazi itasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu yao basi ni juu ya kumdhibiti kinara wa mabao wa mashindano hayo aliyesalia kwenye mashindano hayo Elvis Rupia mwenye mabao manne.

Rupia mbali na kufunga pia ameonyesha umahiri wa kutengeneza nafasi kwa wengine na kama mabeki hao watafanya makosa kidogo tu ya kumsahau Mkenya huyo watamkuta anashangilia pembeni ya uwanja wa New Amani Complex.

Kennedy vs Habib Kyombo

Mshambuliaji wa Singida Habib Kyombo alipambana sana kuifunga timu yake ya zamani Simba kwenye mchezo wa hatua ya makundi lakini leo wanakutana tena, Kennedy ana kazi ya kufanya kuhakikisha hesabu za mshambuliaji huyo hazitimii kama mechi iliyopita.

Jean Baleke vs Joash Onyango

Mshambuliaji hatari kwa Simba ni Jean Baleke mwenye bao moja, hapa Singida watahitaji kuona beki huyo Mkenya anatumia ukongwe wake kumdhibiti Mkongomani huyo.

Kijili vs Onana

Kule pembeni kushoto Simba kutakuwa na winga Willy Onana anayeendelea kuonyesha makali yake hapa kutakuwa na vita na beki kiberenge Kelvin Kijili ambaye amekuwa na ubora wa kupandisha mashambulizi na hata kuzuia Onana ni winga ambaye hatakiwi kupewa nafasi ya kufanya maamuzi lakini kama Kijili akashindwa kucheza naye kwa ubora huo tarajia lolote kumuona Mcameroon huyo akisababisha bao au kufunga.

Kapombe vs Marouf Tchakei

Beki wa kulia wa Simba Shomari Kapombe hana utofauti mkubwa sana na Kijili kwa ubora wao na upande wake huenda akawa ana pambana na Mtogo Marouf Tchakei ambaye naye hatakiwi kupewa nafasi ya kutosha kufanya maamuzi.

Ikumbukwe kuwa Tchakei hakucheza mechi ya makundi baina ya timu hizo wakati Singida ikilala kwa mabao 2-0 na leo atakuwepo uwanjani kuonyesha makali yake.

Miquissone vs Gadiel

Gadiel Michael beki wa kushoto wa Singida atakuwa anapambana na winga Luis Miquissone ambaye taratibu ameanza kurejea kwenye ubora wake hasa akitumia muda aliopewa kwenye mechi hizo.

Gadiel anasifika kwa kujua kukaba kwa nidhamu lakini Miquissone anajulikana kwamba ni winga mbishi anayejua kulazimisha sehemu ngumu hapa kutakucha leo.

Ngoma vs Duke Abuya

Kiungo wa Simba Fabrice Ngoma yuko kwenye ubora mkubwa sana katika mechi hizi hapa atatakiwa kuhakikisha kiungo Singida Duke Abuya hachezi kwa ubora wake kwani anajua kujaribu kwa mashuti makali kama akipewa nafasi ya kufanya maamuzi kwa utulivu.

Chanzo: Mwanaspoti