Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viroho vinawadunda Arsenal na Man City, Man United na Chelsea ni shida

Hatimaye Chelsea Wapata Mdhamini Wa Jezi.png Viroho vinawadunda Arsenal na Man City, Man United na Chelsea ni shida

Sat, 7 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Cheki msimamo wa Ligi Kuu England unavyosoma. Manchester United mechi saba pointi tisa.

Chelsea mechi saba pointi nane. Mashabiki wamebaki vinywa wazi kwa mshangao.

Wazee wazima aibu imewakuta msimu huu. Vigogo wenzao, Manchester City - mechi saba pointi 18, Tottenham mechi saba pointi 17, Arsenal mechi saba pointi 17. Liverpool mechi saba pointi 16.

Thamani ya mechi saba ni pointi 21. Lakini, Man United imepoteza pointi 12. Chelsea imepoteza pointi 13. Ni aibu ukilinganisha na vigogo wenzao wa Big Six. Man City imepoteza pointi tatu, Arsenal na Spurs pointi nne, wakati Liverpool imepoteza pointi tano. Mashabiki wamebaki vinywa wazi tu, presha.

Man United na Chelsea zitakuwa na nafasi ya kuweka mambo sawa wikiendi hii, zitakaposhuka viwanjani tena kukipiga kwenye Ligi Kuu England. Lakini, mashabiki wao wamebaki na presha juu, timu zao zitatoboa? Man United itakuwa nyumbani Old Trafford kukipiga na Brentford. Lakini, uwanjani hapo, Jumanne iliyopita walikubali kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Galatasaray kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hii leo Jumamosi itakuwaje? Presha ya mashabiki ipo juu. Wengine wakisema “Tunapigwa tena!”

Takwimu zinaonyesha kwamba Man United na Brentford zimekutana mara nne kwenye Ligi Kuu England, ambapo miamba hiyo ya Old Trafford imeshinda tatu, mbili nyumbani na moja ugenini, huku Brentford ikishinda moja, kwenye uwanja wake wa nyumbani, mechi ambayo Man United ilikubali kichapo cha mabao 4-0.

Chelsea wao watasafiri kwenda Turf Moor kuwakabili Burnley. Mashabiki wa The Blues wanasubiri kuona kama kuna kitu timu yao itafanya kurudisha matumaini. Rekodi zinaonyesha timu hizo zimekutana mara 16 kwenye Ligi Kuu England, Chelsea ikishinda 11, nne nyumbani na saba ugenini, huku Burnley yenyewe imeshinda moja tu, ugenini. Mechi nne zilimalizika kwa sare. Burnley haijawahi kuishinda Chelsea uwanjani Turf Moor. Je, itakuwaje hii leo? Ngoja tuone.

Spurs itakuwa na nafasi ya kupanda kileleni mapema tu endapo kama watafanikiwa kuichapa Luton katika mchezo utakaopigwa Kenilworth Road. Ushindi utawafanya Spurs kufikisha pointi 20 na watakuwa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa muda kusubiri wapinzani wao Man City na Arsenal kucheza mechi yao. Hii itakuwa mara ya kwanza Spurs kukipiga na Luton kwenye Ligi Kuu.

Kitu kizuri kwa Spurs ni kwamba Arsenal na Man City zitamalizana zenyewe kesho Jumapili. Kipute hicho cha Emirates kinaonekana kukaa vibaya kwa wenyeji Arsenal baada ya kuchapwa kwenye mechi zote tano za ligi zilizopita walipokabiliana na Man City. Rekodi za jumla, miamba hiyo imekutana mara 52 kwenye ligi, Arsenal ikiongoza kwa ushindi, mara 23, mara 12 ilipokuwa nyumbani na 11 ugenini, wakati Man City imeshinda 19, mara 12 nyumbani na saba ugenini. Mechi 10 baina yao zilimalizika kwa sare. Safari hii itakuwaje, wakati Mikel Arteta atakapomkaribisha bosi wake wa zamani Pep Guardiola?

Liverpool nao watakuwa ugenini hiyo kesho kukipiga na Brighton huko Amex Stadium. Liverpool wanahitaji pointi za kuwasogeza juu, huku wakiomba mbaya kwa Arsenal, Man City na Spurs. Namba zinaonyesha kwamba Brighton na Liverpool zimekutana mara 12 kwenye Ligi Kuu England, huku wenyeji wa mchezo huo wa kesho wakiwa wameshinda mbili tu, moja nyumbani na nyingine ugenini, huku Liverpool ikishinda saba, tatu nyumbani na nne ugenini. Mechi zao tatu zilimalizika kwa sare, ikiwamo moja ya msimu uliopita.

Mechi nyingine zitakazopigwa leo Jumamosi, Everton watakuwa nyumbani kuwakaribisha Bournemouth, wakati Fulham watakipiga na Sheffield United na Crystal Palace watakwenda jino kwa jino na Nottingham Forest. Kesho, West Ham United watakuwa kwao kucheza na Newcastle United ambao wapo moto kwelikweli msimu huu, huku Wolves wakiwa na kasheshe la kucheza na Aston Villa.

Chanzo: Mwanaspoti