Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vipigo vyatibua Alliance, makocha njia panda

Alliance Vipigo Vipigo vyatibua Alliance, makocha njiapanda

Mon, 1 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Benchi la ufundi la timu ya Alliance FC muda wowote huenda likapewa mkono wa kwaheri na uongozi kutokana na mwenendo mbaya katika michuano ya First League, huku kukosekana amani ndani ya kikosi kukitajwa kuwa sababu mojawapo.

Joto liliongezeka zaidi juzi baada ya timu hiyo kufungwa mabao 2-1 na Mwadui FC katika Uwanja wa Nyamagana mjini hapa, jambo lililosababisha kocha mkuu Atuga Manyundo na msaidizi wake, Ahmed Simba baada ya mchezo kumalizika washindwe kuondoka uwanjani wakitumia muda mrefu kukaa.

Alliance ilimtambulisha Manyundo, Agosti 4, 2023 na kuiongoza timu hiyo katika mechi saba za First League bila ushindi akiambulia sare nne na kupoteza tatu, huku akiletewa Ahmed Simba kuwa kocha mkuu na yeye kuwa msaidizi jambo ambalo hakukubaliana nalo.

Mmoja wa wachezaji wa timu hiyo (jina tunalo), ameiambia Mwanaspoti kwamba ndani ya kikosi kuna matabaka kwani baadhi ya wachezaji waliodumu muda mrefu wanasikilizwa kuliko kocha na pia mbinu na mfumo wa kocha (3-5-2) umekuwa ukipingwa na uongozi ambao unataka atumie 4-4-2, lakini kocha kagoma.

Amesema awali uongozi ulisema wasiposhinda dhidi ya Mwadui FCchochote kingetokea, hata hivyo, baada ya mchezo huo walitakiwa kurudi kambini kwa ajili ya kikao cha uongozi, wachezaji na benchi la ufundi.

“Kwa mfano mechi ya Shirikisho na Azam, kocha mkuu alipaswa kuwa Simba, lakini Atuga (Manyundo) akawahi akabeba majukumu. Kwa hiyo baada ya hapo alisema haji tena, lakini leo (juzi) amekuja kwa hiyo hali ndiyo iko hivyo,” amesema mchezaji huyo.

“Shida nyingine kwenye timu hiyo ni kuwa kuna wale wachezaji waliokaa muda mrefu wanaona kama timu ni ya kwao, wanamdharau hadi kocha na wanasikilizwa wao. Halafu namba zao hazina ushindani, kwa hiyo kocha akisema na wao wakisema wao ndiyo wanasikilizwa.”

Mwanaspoti iliwatafuta Mwenyekiti wa Alliance, Stephano Nyaitati na kocha Manyundo kuzungumzia mustakabali wa kikosi hicho, lakini wote hawakuwa tayari kuzungumza, ambapo Mwanaspoti inaendelea kufuatilia na itakujuza kitakachojiri.

Chanzo: Mwanaspoti