Wikiendi iliyopita ilikuwa mbaya sana kwa mashabiki wa Manchester United baada ya timu yao kukubali kichapo cha mabao 6-3 kutoka kwa Manchester City katika mchezo wa Ligi Kuu England.
Mabao ya Man City yalifungwa na Erling Haaland na Phil Foden ambao kila mmoja alifunga hat-trick. Lakini hii sio mara ya kwanza Man United kupokea vichapo vya aina hii kwenye Ligi Kuu England kwani imewahi kuwatokea hivyo mara kadhaa. Hivi hapa vipigo vitano vikubwa walivyowahi kukutana navyo.
5. Newcastle 5-0 Man United (1996-97)
Wakati huu Newcastle ilikuwa moja ya timu nne za juu kwenye Ligi Kuu England. Msimu huu ikiwa chini ya Kevin Keegan, Newcastle United ilipaa ushindi huo mnono mbele ya Man United iliyochukua ubingwa baadae.
Licha ya ubora wa Newcastle bado Man United ilionekana kuwa bora zaidi yao na hakuna aliyeamini kama wangeweza kupokea kipigo cha aina hiyo.
Darren Peacock alianza kupeleka kilio dakika ya 12 na baadae David Ginola, Les Ferdinand na Alan Shearer wakafunga bao mojamoja kila mmoja kukamilisha idadi ya mabao manne lakini wakati mpira upo kwenye dakika za mwisho Philippe Albert alipiga shuti la mbali ambalo lilimshinda Peter Schmeichel na kulifanya jahazi la Man United lizame kwa matofali matano.
4. Chelsea 5-0 Manchester United (1999/00)
Haikupita muda mrefu tangu Man United ilipochukua mataji matatu kwa pamoja msimu wa 1998-99, ilikuwa ni siku ya kushangaza kwa mashabiki wa soka duniani kote kutokana na ubora ambao Man United ilikuwa nao kwa wakati huo.
Wakati inaenda kucheza na Chelsea, Man United ilikuwa haijapoteza mchezo katika mechi 29 za Ligi Kuu England lakini Chelsea iliivunja rekodi hii.
Gus Poyet alifunga bao la kwanza kabla ya Chris Sutton kufunga la pili, mambo yalizidi kuwa magumu kwa United baada ya staa wao Nicky Butt kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 21 kwa kumchezea vibaya Denis Wise.
Poyet pia alifunga bao la tatu dakika ya 54, Henning Berg akajifunga mwenyewe na mwisho Jody Morris akakamilisha karamu ya mabao matano katika dakika ya 81.
Licha ya kipigo hicho cha aibu Man United ilifankiwa kuchukua ubingwa tena kwa tofauti ya alama 18 juu ya Arsenal iliyokuwa nafasi ya pili.
3. Man United 1-6 Tottenham Hotspur (2020-21)
Hii ilikuwa ni siku nyingine mbaya kuwahi kutokea kwenye historia ya Man United, mechi ilianza vizuri kwa Man United kwani dakika ya pili tu Bruno Fernandes alimfanya kocha wa Spurs wa wakati huo Jose Mourinho kushika kichwa baada ya kuipatia bao la kuongoza Man United kupitia mkwaju wa penalti.
Lakini ndani ya dakika saba tu Tanguy Ndombele na Son Heung-Min, tayari wakawa wamesawazisha na kuongeza la ziada kuifanya Spurs iwe mbele kwa bao 2-1.
Mambo yaliendelea kuwa hivyo hadi pale Anthony Martial alipoonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Erik Lamela.
Baada ya hapo ndio mvua ya magoli ikaanza kwa Kane kufunga bao la tatu akifuatiwa na Son aliyefunga la nne, Serge Aurier akafunga la tano na Kane akamaliza kazi kwa kufunga la sita kwa penalti dakika 79.
2. Man United 0-5 Liverpool (2021-22)
Ni moja kati ya vipigo vya hivi karibuni ambavyo mashetani hawa wekundu wamevipata. Kawaida mechi ya Man United na Liverpool huwa ina upinzani mkubwa na kuna wakati haikuwa inachezwa usiku kwa sababu mara zote kumekuwa na vurugu za hapa na pale kwa mashabiki wake.
Kwenye mechi hii ya mzungumko wa kwanza wa msimu uliopita, Man United iliyokuwa chini ya Ole Gunnar Solskjaer ilikuwa ikionekana kama ni timu ya vijana wa shule mbele ya Liverpool ya Jurgen Klopp, walizidiwa kila idara.
Mohamed Salah alifanya mauaji kwa kufunga hat-trick wakati Naby Keita na Diogo Jota wakifunga bao mojamoja kukamilisha karamu hiyo. Kwenye mechi hii kiungo wa Man United Paul Pogba alitolewa nje kwa kadi nyekundu.
1. Man United 1-6 Man City (2011-12)
Kipigo hiki kiliifanya Man United iweke rekodi ya kuruhusu mabao sita kwenye Uwanja wa Old Trafford kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1930.
Mario Balotelli na Edin Dzeko wote walifunga mabao mawili mawili huku Sergio Aguero na David Silva wakikamilisha karamu kwa kila mmoja kufunga bao moja.
Bao pekee la Man United lilifungwa na Darren Fletcher, hii ilikuwa ni moja ya siku mbaya ambayo uwanja mzima wa Old Trafford ulikuwa kimya huku baadhi ya mashabiki wakionekana kutokwa na machozi na hawaamini macho yao.