Mabingwa wa Soka nchini Uganda Vipers SC wametangaza hadharani kuitamani Simba SC kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Hatua ya Makundi msimu huu 2022/23.
Vipers SC ilitinga Hatua ya Makundi kwa kuwaondoa Mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika TP Mazembe kwa changamoto ya Penati, mjini Lubumbashi-DR Congo.
Meneja Masoko wa Klabu ya Vipers Robert Sentongo amesema, anaamini ikitokea wamepangwa na Simba SC katika Hatua ya Makundi, watapata upinzani mzuri kutoka kwa klabu hiyo ya Dar es salaam.
Amesema utakuwa mchezo ambao utaibua hisia kubwa za Mashabiki wa pande zote mbili, ambapo kila upande utahitaji kwenda kwa mwenzake kuishangilia timu yake ili iweze kufanya vizuri.
“Tunatamani kukutana na Simba SC kwenye Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kwa sababu tunaamini tutapata upinzani mzuri kutoka kwao.”
“Simba SC ipo katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ tunaamini kama tutapangwa nayo itatusaidia sana hata kwa mashabiki wetu kusafiri kutoka Uganda kwenda Tanzania, na Mashabiki wao kutoka Tanzania kuja Uganda, naamini utakua mchezo mzuri sana.” amesema Sentongo
Hata hivyo kuna uwezekano Mkubwa kwa Vipers SC kukutana na Simba SC kutokana na timu hizo kuwa katika Vyungu (POT) tofauti, ambavyo vitatumika kama Kigezo cha kupanga makundi ya Michuano hiyo mwezi Novemba.
Simba SC ipo katika Chungu (POT) cha tatu chenye timu za CR Belouizdad (Algeria), JS Kabylie (Algeria) na Al Hilal (Sudan) huku Vipers ikiwekwa Chungu (POT) cha nne chenye timu za Coton Sport (Cameroon) na Al Merrikh (Sudan).
Chungu cha kwanza kina timu za Al Ahly (Misri), Wydad AC (Morocco), Espérance de Tunis (Tunisia) na Raja Casablanca (Morocco).
Chungu cha Pili kina timu za Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini, Zamalek (Misri), Petro de Luanda (Angola) na Horoya (Guinea).