Timu ya Vipers kutoka nchini Uganda inatarajia kuwasili nchini Jumatatu ya Machi 6 ,2023 kwaajili ya mchezo wa makundi wa Ligi ya mabingwa Barani utakaochezwa siku ya Jumanne ya Machi 7-2023 kwenye dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam
Akizungumza na waandishi wa habari,Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba SC Ahmedy Ally amesema wanataraji mgeni rasmi kuelekea mchezo huo kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma huku kauli mbiu kuelekea mchezo huo ni Nguvu Moja ,Kwa Mkapa Hatoki Mtu.
''Siku hiyo tumeipa jina la "Jumanne ya wenye nchi" kwa maana ya kwamba wananchi wapo ila sisi ndio tutaishika nchi kwa mkapa hii mechi inaenda kuamua hatma yetu wanasimba",
" Itakuwa aibu kubwa kama wanasimba kama tutaishia hatua ya mtoano hii ni michuano yetu jumanne tunampiga vipers na kuiona hatua ya robo fainali kule".amesema Ahmed
Kwa Upande mwingine,Msanii Khalid Ramadhani maaarufu Tunda Man amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo wa Jumanne dhidi ya Vipers huku wakianzia kwenye shamra shamra za kuelekea mchezo huo zinazotaraji kufanyika Jumapili ya Machi 05 -2023 kwenye fukwe za Coco Beach Jjini Dar es Salaam.
Simba SC inakamata nafasi ya 3 kwenye msimamo wa Kundi C wa ligi ya mabingwa barani Afrika baada ya kucheza michezo mitatu na kukubali vichapo kwenye michezo miwili na kushinda mchezo mmoja mpaka sasa.