Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vinicius Junior: Mtu na nusu!

Vinicius Jr Real Madrid Vinicius Junior

Tue, 20 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ukipata gawana na wengine. Ndicho unachoweza kusema baada ya winga wa Real Madrid, Vinicius Junior kutumia pesa nyingi sana kwenye kuendesha miradi ya kusaidia wenye hali duni huko kwao Brazil.

Fowadi huyo wa Los Blancos anatumia mafanikio yake kwa kile anachokivuna kwa kusaidia maisha ya wale wenye vipato duni huko Brazil.

Ipo hivi. Vinicius, 24, aliwekeza Pauni 2.6 milioni kwenye kuboresha majengo ya shule iliyokuwa imefungwa huko Sau Goncalo katika mji uliopo karibu na Rio de Janeiro alikokulia yeye na kuibadili kuwa sehemu ya kupata mambo ya kijamii.

Mradi huo umelenga kwenye kutoa elimu, michezo na shughuli za kiutamaduni kwa watu wasiopungua 5,000 na huduma zote ni bure.

Kinachoelezwa ni kwamba mradi huo umasimamiwa na Vini Junior Institute, ambayo ndiyo inayoendesha shughuli zote za miradi ya kujitolea inayofanywa na supastaa huyo wa soka.

Jengo hilo la shule ambalo lilikuwa limefungwa na kutelekezwa kwa muongo mmoja, sasa limebadilishwa, limeboreshwa na kufanywa kuwa makazi ya watu wasiokuwa na uwezo wanaopatikana kwenye eneo hilo.

Vinicius anapewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or mwaka huu badaa ya kuiongoza vyema Real Madrid kushinda ubingwa wa La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.

Na msimu huu huko kwenye kikosi cha Los Blancos anapangwa kwenye fowadi yenye wakali wengine matata kabisa, akiwamo Kylian Mbappe na Jude Bellingham. Usiku wa juzi Jumapili, Real Madrid ilishuka uwanjani kukipiga na Mallorca ugenini katika mchezo wa La Liga uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, ambapo bao la Real Madrid lilifungwa na Mbrazili, Rodrygo baada ya pasi kali ya Vini Jr.

Kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, ripoti zinafichua kwamba Vini Jr aliwekewa mezani ofa ya kibabe sana kutoka Saudi Arabia.

Kinachoelezwa ni kwamba Vini Jr aliwekewa mezani ofa ya kulipwa karibu Pauni 300 milioni kwa mwaka.

Kwenye ofa hiyo kwa mwezi atalipwa Pauni 25 milioni, Pauni 800,000 kwa siku na karibu Pauni 10 kwa sekunde.

Katika kipindi hiki cha mapumziko ya majira ya kiangazi, Vini Jr alitumikia sehemu kubwa huko kwao Brazil, ambako aliteswa na mtoto mmoja kwenye mchezo wa futsal. Picha zilimwonyesha Vini Jr akilambishwa sakafu kwa chenga kali ya mtoto huyo kwenye mchezo huo wa futsal kwenye klabu ya Canto do Rio.

Vinicius alianzia maisha yake ya soka kwenye klabu hiyo alipokuwa na umri wa miaka saba kabla ya sasa kuwa staa mkubwa kabisa kwenye kikosi cha miamba ya soka ya Hispania, Real Madrid.

Chanzo: Mwanaspoti