Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vikosi vya mkwanja mrefu CAF

Vikosi Mkwanja Vikosi vya mkwanja mrefu CAF

Fri, 24 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ikianza leo, moja kati ya mambo yanayozungumziwa ni ukubwa wa vikosi na ukwasi wa timu zinazoshiriki.

Kila timu ina thamani yake kulingana na vikosi vya wachezaji ambao vipo navyo kwa sasa.

Kupitia mtandao wa TransferMarkt tumekuletea orodha ya timu zinazoshika nafasi 10 za juu kwa kuwa na vikosi vyenye thamani zaidi.

AL AHLY- SH81 BILIONI

Unaweza ukawaita Real Madrid ya Afrika, hawa ndio mabingwa watetezi na pia mabingwa mara 11 wa michuano hii ya Afrika. Ndio timu yenye thamani zaidi katika hatua hii ya makundi kutokana na kikosi chao na utajiri walionao.

Katika dirisha lililopita la usajili wababe hawa walisajili mastaa wawili kwa bei kubwa ambao ni Emam Ashour aliyewagharimu Euro 2.6 milioni (Sh7 bilioni) na Reda Slim kwa Euro 2 milioni (Sh5.4 bilioni).

Kiujumla ilitumia zaidi ya Euro 5 milioni kwenye ishu ya usajili ambazo ni zaidi ya Sh13 bilioni za Kitanzania. Thamani yao pia imeangalia thamani ya wachezaji wao kwenye mtandao huu wa Transfer Market.

MAMELODI SUNDOWN - SH79 BILIONI

Unaweza kuwaida ‘Masandawana’ kama jina lao la utani. Hawa ndio mabingwa wa kwanza wa michuano ya African Football League ambako wamekunja zawadi ya Dola 10 milioni.

Hiyo ikutoshe kuonyesha wana ukwasi kiasi gani. Msimu uliopita hawakufanya usajili wa bei mbaya sana ukilinganisha na washindani wao wa karibu, Ahly. Walifanya usajili mmoja tu ambao ni ule wa Junior Mandieta aliyesajiliwa kwa Euro 600,000 (Sh1.6 bilioni).

Mchezaji ghali zaidi kwenye kikosi chao ni Peter Shalulile ambaye ana thamani ya Euro 2.5 milioni (zaidi ya Sh4 bilioni za Kitanzania).

PYRAMIDS - SH57 BILIONI

Hii ni moja kati ya timu zinazofungana na Ahly kwenye rekodi ya kutumia pesa nyingi katika dirisha lililopita la usajili, ikidaiwa kutumia kiasi kisichopungua Euro 5 milioni ambazo ni zaidi ya Sh13 bilioni.

Ilichukua nyota watatu kwa bei ya Euro 1 milioni (Sh2.7 bilioni) kila mmoja ambao ni Mohamed Reda, Mahmoud Marei na Mohanad Lasheen. Lakini pia ilimchukua Mostafa Fathi kwa Euro 900,000 (Sh2.4 bilioni) na Fiston Mayele kwa Euro 700,000 (Sh1.9 bilioni).

Mchezaji ghali zaidi kwenye kikosi chao kwa sasa ni Ramadan Sobhi ambaye kwa mujibu wa mtandao wa Transfer Market jamaa ana thamani ya Euro 3 milioni.

WYDAD CA - SH51 BILIONI

Hawakutumia pesa nyingi kwenye usajili wa dirisha lililopita zaidi ya Euro 100,000 waliyomwaga kumchukua Montasser Lahtimi kwa mkopo kutoka kwa mabingwa wa msimu wa mwaka juzi wa Ligi Kuu nchini Trabzonspor.

Thamani ya wababe hawa inatokana na aina ya wachezaji ghali iliyonao na pesa ambazo imekuwa ikizikusanya kwenye kipindi cha hivi karibuni kwa ushiriki wao kwenye michuano mbalimbali kama Ligi ya Mabingwa, African Football League na hata Ligi Kuu nchini Morocco.

Kwa sasa mchezaji wao ghali zaidi ni Yahia Attiyat Allah mwenye thamani ya Euro 2.5 milioni.

ESPERANCE- SH46 BILIONI

Matajiri wa Tunisia, hii ndio timu yenye ukwasi zaidi nchini humo kwa sasa na kikosi kinatajwa kuwa na thamani ya Euro 17.4 milioni (Sh48 bilioni).

Waliwahi kuwa mabingwa wa michuano hii miaka miwili mfululizo mwaka 2018 na 2019.

Dirisha lililopita hawakumwaga pesa sana kwenye masuala ya usajili lakini kikosi chao kina thamani kubwa huku wachezaji wengi wakionekana kuwa na thamani ya Euro 500,000 na kuendelea.

Staa wao ambaye ndio ghali zaidi kwa sasa ni Yassine Meriah ambaye walimsajili kutoka kwa vigogo wa Ugiriki Olympiakos kwa usajili huru.

CR BELOUIZDAD - SH27 BILIONI

Ndio wenyeji wa Yanga kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi katika kundi D, hii ndio timu pekee kutoka nchini Algeria iliyopo hatua ya makundi kwa sasa baada ya ndugu zao CS Constantine kutolewa mapema na Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia.

Thamani yao inatokana na wingi wa wachezaji ambao wana thamani kubwa sokoni ingawa hawana mchezaji mwenye thamani inayozidia Euro 1 milioni.

ETOILE DE SAHEL - SH27 BILIONI

Vigogo wengine kutoka Tunisia. Kwa sasa ndio wanaonekana kutishia ufalme wa Esperance nchini humo. Msimu wa mwaka juzi walifanikiwa kufika hatua ya makundi lakini hawakwenda robo fainali baada ya kumaliza nafasi yatatu.

Kwa sasa wana mastaa kama Osama Abid na Jacques Mbe ambao ndio wana thamani kubwa zaidi.

PETRO LUANDA - SH8 BILIONI

Licha ya kwamba haijachukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa lakini wababe hawa wamekuwa wakisumbua sana vigogo barani Ulaya wakicheza mara kadhaa hatua ya makundi, robo fainali na nusu fainali.

Uwepo wa mastaa kama Ignatius Miguel mwenye thamani ya Euro 400,000 na Alexandre Guedes raia wa Ureno mwenye thamani ya Euro 300,000 ndio umezidisha thamani ya kikosi hiki.

SIMBA - SH7 BILIONI

Ndio, mnyama yumo humu. Kushiriki kwao michuano ya African Football League na kucheza kwao zaidi ya mara mbili hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabinga vimechangia kuwa kwenye thamani hii.

Mchezaji ambaye amewazidishia thamani zaidi ni kipa wao raia wa Morocco Ayoub Lakred ambaye kwenye Transfer Market ana thamani ya Euro 1.2 milioni (Sh3.3 bilioni).

TP MAZEMBE - SH4 BILIONI

Ingekuwa miaka minne hadi mitano nyuma, wangekuwa kwenye namba mbili au tatu wakishindana na vigogo wakubwa barani Afrika.

Lakini hilo halionekani kwa sasa, ingawa licha ya kuyumba kwao, bado wameendelea kuwa kwenye 10 bora ya moja ya timu zenye thamani zaidi katika hatua hii ya makundi.

Mazembe ambayo ilizoeleka kuwa na mastaa wenye thamani ya zaidi ya Euro 1 milioni kwa sasa mchezaji wao ghali ana thamani ya Euro 300,000 ambaye ni Louis Ameka.

YANGA - SH3.8 BILIONI

Mbali ya kutokuwepo kwenye 10 bora, katika takwimu za Transfermakert Yanga inaonekana kuwa na thamani hiyo ya bilioni 3.8 ikiwa ni kati ya timu zenye vikosi vyenye thamani kubwa zaidi.

Chanzo: Mwanaspoti