Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vikao vya mabosi Yanga vyaibua mazito

Nasreddine Nabi El Nasredinne Nabi, Kocha wa Yanga

Sun, 26 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabosi wa Yanga wako katika vikao vya siri wakipiga hesabu za usajili kupitia dirisha dogo lililofungwa Desemba 16, lakini ripoti ya kocha wao Nesreddine Nabi imewekwa bayana ikitaka mashine mpya nne za haraka na tayari uhakika kuna mastaa wawili wameshaanguka sahihi zao.

Pamoja na kuwa na uhakika wa Salum Abubakar na Denis Nkane, Nabi ametaka pia beki mmoja wa kati atakayewapa presha nahodha Bakar Mwamnyeto na Dickson Job wanaocheza kwa sasa wakipigwa tafu wakati mwingine na Yannick Bangala anayemudu pia kucheza kama kiungo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, inayosimamia pia usajili, Dominic Albinius aliliambia Mwanaspoti kuwa, wamepokea ripoti ya Nabi na tayari imeshaanza kufanyiwa kazi kwa utulivu mkubwa kwenye dirisha dogo la usajili litakalofungwa Januari 15.

Albinius, ambaye kitaaluma ni kocha wa soka alisema katika kutengeneza safu bora ya ulinzi kocha wao, bado anataka aletewe beki wa kati atakayekuja kushindana na nahodha Bakari Mwamnyeto na Dickson Job. Mbali na Job na Mwamnyeto eneo hilo pia lina Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Bangala anayemudu kucheza pia eneo la kiungo mkabaji.

Aidha katika eneo hilo kuna uwezekano baadhi ya mabeki kutolewa kwa mikopo na kuachwa kulingana na mikataba yao.

Albinius alisema pia ripoti hiyo inataka viungo wawili tofauti mmoja wa pembeni anayeziba pengo la Yacouba Songne aliyefanyiwa upasuaji na atakosa msimu mzima, pia akitakiwa kiungo mshambuliaji wa kati na uhakika Mwanaspoti linajua fundi wa pasi za mabao Salum Abubakar ‘Sure boy’ amebakiza kuanza mazoezi. Advertisement

“Tunamtafutia pia kiungo mshambuliaji wa kati atakayekuwa mbunifu zaidi unajua mpaka sasa eneo hilo kuna Feisal Salum pekee wakati huu Mapinduzi Balama akiendelea kutafuta ubora wake akitokea majeruhi,” alisema Albinius.

Mmoja ya mabeki wanaotajwa kuingia kwenye rada za Yanga ni Abdulmajid Mangalo aliyepo Biashara United, pia jina la Kulwa Idd Mobby, aliyepo Geita Gold likitajwa.

Albinius, aliongeza Nabi amehitaji mshambuliaji mwingine mwenye kasi ya kufunga zaidi atakayekuja kushindana na Fiston Mayele na Heritier Makambo.

“Nabi anahitaji mtu wa namna hiyo atakayekuja kushirikiana na Mayele na Makambo, si mnajua Yusuf (Athuman) ameumia tunapambana kumtibu, lakini wakati huu ni vyema tukapata mtu bora.”

Albinius alisema kazi ya kutafuta wachezaji hao inafanywa kwa umakini mkubwa na kila mchezaji wanayemtaka hujadiliwa na kamati yao, kisha kocha kushirikishwa kuangalia ubora wake wa huko anakotoka na kipi kitasaidia timu yao.

“Hapa Yanga usajili haufanywi na mtu mmoja, tupo kama kamati ya ufundi yenye watu bora, pia kocha wetu (Nabi) anahusika kuangalia ubora, ilio kupata wa kuisaidia timu. Tukimaliza kazi mtatangaziwa,” alisema.

KAMBINI SASA

Yanga kesho inatarajiwa kushuka uwanjani kuvaana na Biashara United katika mfululizo wa Ligi Kuu Bara, huko kambini unaambiwa mambo yamenoga baada ya wachezaji karibu wote wa kikosi cha kwanza wapo fiti, ukiondoa wale walio majeruhi.

Mastaa hao na makocha wao wamejichimbia kambini kunoa makali kabla ya kuwashukia Biashara.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live