Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana wa Gamondi wajivika mabomu kuwamaliza Medeama

Yanga Caf Mks Vijana wa Gamondi wajivika mabomu kuwamaliza Medeama

Fri, 8 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga wameamua kwamba kuanzia leo saa 1: 00 usiku dhidi ya Medeama kila dakika ni fainali kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Baba Yara jijini Kumasi ambao ni mji ambao una kadiriwa kuwa na watu 3.348 Milioni kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2020 nchini humo.

Habari njema kwa Yanga ni kutua kwa staa wao, Stephanie Aziz KI ambaye mara baada ya mchezo wa Al Ahly alitimka nchini kwa ruhusa maalum akirejea kwao kwa matatizo ya kifamilia na juzi alirudi kundini na kufanya mazoezi na wenzake akionekana yuko sawasawa.

KARATA ZA GAMONDI

Kocha wa Yanga Miguel Gamondi licha ya kukiri kwamba mchezo utakuwa mgumu alisema wamejipanga sawasawa kucheza kwa nidhamu na kuweka mipango ya kuwaondolea Medeama hesabu za ushindi.

“Kwenye mashindano kama haya kila timu unatakiwa ucheze nayo kwa heshima kwa kuwa wote wamestahili kuwa hapa tulipo, tunatakiwa kucheza kwa umakini mkubwa hii ni timu ambayo ina wachezaji bora wenye mbinu,”alisema Gamondi.

“Tunajua namna wanavyocheza wakiwa nyumbani nafikiri kila kitu tumeshamaliza kwa wachezaji tusubiri kuona kipi kitatokea karibu wachezaji wote tuliokuja nao wako sawasawa.”

TAJIRI ASHTUA

Nje ya uwanja tajiri wa Yanga Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ na uongozi wa klabu hiyo umecheza mechi hiyo kwa akili na wachezaji wao wakiwapa ahadi nzito ambayo ni sawa na ile aliyowapa ilipocheza dhidi ya Simba na Al Ahly.

Mwanaspoti linafahamu kwamba endapo Yanga itashinda kila bao la mchezo huo litanunuliwa kwa Sh100 milioni na idadi ya mwisho ya mabao hayo kutakuwa na ziada ya Sh200 milioni.

Ahadi kama hii imewahi kuwaponza Simba ilipochapwa mabao 5-1 lakini Al Ahly pekee ilinusurika kwenye mtego huo ikiwanyima fedha ndefu wachezaji wa Yanga ambao hawakuambulia kitu kwenye sare ya bao 1-1.

Hata hivyo Yanga inafahamu kwamba malengo yao hayo hayataweza kutimia kirahisi kwani Medeama sio timu rahisi ikiwa nyumbani, rekodi zikionyesha kwenye mechi zao tatu za nyuma za ligi ya mabingwa wameshinda zote dhidi ya Remo Stars (1-0),Horoya AC (3-1) na Belouizdad (2-1).

Yanga pia itakumbuka kwamba mara ya mwisho walipokutana na Medeama nchini humo mwaka Julai 26, 2016 kwenye mchezo wa makundi wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua kama hii walikubali kichapo cha mabao 3-1 ambapo mapema walitangulia kulazimishwa sare ya bao 1-1 hapa nchini.

Msimu huu Medeama ina kitu cha hatari ambacho lazima Yanga ijipange nacho kwani katika mechi zao mbili za makundi imekuwa na mabadiliko manne kutoika kikosi kilichocheza dhidi ya Al Ahly wakipoteza kwa mabao 3-0 na kile kilichokuja kushinda nyumbani dhidi ya Belouizdad nyumbani.

Yanga itatakiwa kuwa makini na mshambuliaji Jonathan Sowah ambaye alikosekana kwenye mchezo uliopita, taarifa zikionyesha jamaa anajua kufunga mabao kwa aina zote.

Sowah aliikosa mechi ya nyumbani dhidi ya Belouizdad kwa kufikisha kadi tatu za njano baada ya kupata kadi ya tatu kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya Al Ahly. Mabingwa hao wa Tanzania akili yao kwenye mchezo huo ni moja tu kubwa kusaka ushindi wao wa kwanza kwenye hatua hii ikikumbuka kwamba ilishapoteza mechi ya kwanza ugenini dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria kisha kulazimisha sare nyumbani dhidi ya bingwa mtetezi Al Ahly ya Misri.

Ushindi huo wa Yanga leo kama itaupata utawarudishia afya yao ikifufua matumaini ya kwenda kusaka nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali.

Yanga ambayo ilitua mapema siku tatu kabla nchini humo tayari kwa mchezo huo ambapo jana ilifanya mazoezi yake ya mwisho huku kila kitu kikionekana kwenda sawasawa kambini kwao wakijificha kwenye hoteli ya kisasa ya Ridge Condos.

MABEKI HAWACHEKANI

Sio ukuta wa Yanga wala Medeama wote una rekodi sawasawa ambapo katika mechi zao mbili zilizopita kila timu imeruhusu mabao manne hatua ambayo zitahitaji kujipanga sawasawa.

Kocha wa Medeama Evance Adotey ameliambia Mwanaspoti kwamba licha ya kushinda kwao mechi ya pili nyumbani kikosi chake kitaingia kwa tahadhari kubwa wakijua kwamba Yanga sio timu rahisi.

Adotey alisema wamejipanga kushinda mechi yao ya pili nyumbani lakini hilo litategemea wachezaji wake watazingatia kwa kiwango gani kucheza kwa nidhamu ya mchezo.

“Tunakwenda kukutana na timu bora kaka, mimi sio mtu wa kupenda kuangalia matokeo ya mechi zilizopita kitu nafahamu na nimewaambia wachezaji wangu hatutakiwi kuwadharau Yanga hata kama haijapata ushindi mpaka sasa,”alisema Adotey.

“Wana wachezaji bora tunatakiwa kukumbuka kucheza kwa nidhamu najua kwamba wana rekodi bora wanapocheza ugenini lakini mwisho tunahitaji kushinda hapa nyumbani.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live