Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana wa Emery na rekodi mpya

Aston Villa Hesabu Vijana wa Emery na rekodi mpya

Fri, 17 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Aston Villa chini ya kocha mwenye rekodi kali Ulaya Unai Emery, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1996, itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, jambo ambalo ilikuwa halitarajiwi na wengi.

Mwanzoni mwa msimu huu, wachambuzi wa masuala ya soka walikuwa wanaitaja Villa kati ya timu ambazo zitakuwa zinapambana kuhakikisha kuwa zinabaki kwenye ligi, lakini imewashangaza baada ya kufuzu kwa michuano hiyo mikubwa Ulaya, baada ya Tottenham Hotspur kupoteza mchezo wa juzi dhidi ya Man City.

Aston Villa sasa ina pointi 68, zikiwa ni tano mbele ya Spurs timu zote zikiwa zimebakiza mchezo mmoja wa mwisho wa msimu utakaopigwa wikiendi hii.

Idadi hii ya pointi ni ya pili kwa ukubwa kuanzia Villa imeanzishwa, ambapo msimu wa 1992-93, timu hiyo ilikusanya pointi 74, ikishika nafasi ya pili kwenye ligi nyuma ya Man United lakini bado haikufanikiwa kufuzu kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Villa imekuwa kwenye timu tano za juu kwenye msimamo kuanzia Septemba mwaka jana, ikiwa imekaa kwenye eneo hilo kwa siku 150, ikiwa ni mara yao ya kwanza kufanya hivyo tangu msimu wa 1998/99, ambapo ilimaliza katika nafasi ya sita chini ya kocha John Gregory.

Kwa msimu huu, Tottenham pekee ndiyo ilikuwa inaweza kuipiku Villa kwenye nafasi ya nne msimu huu kwa kuwa vigogo wakubwa Manchester United na Chelsea zimekuwa na vikosi dhaifu msimu huu.

Villa haikuweza kufika kwenye hatua hii tangu michuano hiyo ilipobadilishwa kutoka kwenye mashindano ya European Cup na kuitwa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 1991-92.

Mara ya mwisho kwa timu hiyo kucheza michuano hiyo ya Ulaya kabla haijabadilishwa jina ilikuwa miaka 41, iliyopita ambapo ni msimu wa 1982-83 ambapo ilifanikiwa kutwaa ubingwa.

Rekodi kubwa kwa Villa kwa miaka ya hivi karibuni ni kumalizika kwenye nafasi ya pili na ya nne kwenye Ligi Kuu England msimu wa 1992-93 na 1995-96

Yasheherekea kichapo cha Spurs

Wakati mashabiki wa Arsenal walikuwa wanataka kuona Spurs inaibuka na ushindi kwenye mchezo dhidi ya Man City, ili timu hiyo iwe na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu, wachezaji na benchi la ufundi la Villa walikuwa hotelini wakiiunga mkono City kuibuka na ushindi kwenye mchezo huu.

Klabu hiyo ilituma picha kwenye mitandao yake ya kijamii ikiwaonyesha wachezaji pamoja na benchi la ufundi wakifungua shampeni mara baada ya mchezo wa Spurs na City.

"Hii ni siku nzuri kwetu, ilikuwa ndoto yetu kuanzia mwanzoni mwa msimu kuwa tunatakiwa kuishia hapa, tulikuwa na wachezaji wenye majeraha katikati ya msimu, lakini kila mchezaji alionyesha kiwango cha juu uwanjani kuhakikisha kuwa hatuyumbi."

"Hakuna aliyekuwa anatarajia kuwa tunaweza kumaliza tukiwa kwenye nafasi hii ilikuwa vigumu lakini tumeweza kufanya kile ambacho mashabiki wetu walikuwa wanakitaka," alisema beki wa Villa Lucas Digne.

Emery aibadili Villa

Aston Villa ilimchukua Emery kama meneja wa timu hiyo Oktoba 2022, wakati Villa ikiwa inashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, zikiwa ni pointi tatu kabla ya kufikia timu zinazoweza kushuka daraja.

Villa ilikuwa kwenye wakati mgumu kwa misimu miwili ya nyuma ambapo ilikuwa imemaliza kwenye nafasi ya 14 na 17, huku mwaka 2019 ikiwa ilicheza Daraja la Kwanza Championship.

Lakini Emery amefanya mambo makubwa kwenye timu hiyo na kuifanya iwe bora ya timu ya ushindani, kuanzia ameichukua timu hiyo na sasa imekuwa na ushindani mkubwa.

Msimu huu vijana hao wa Emery wameweka rekodi ya kufika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Europa Conference League, ikiwa ni mara yao ya kwanza kufika kwenye hatua hiyo kubwa.

Kocha huyo wa zamani wa Arsenal, hii itakuwa timu yake ya sita kuifundisha kwenye Ligi ya Mabingwa baada ya awali kuwa na Valencia, Spartak Moscow, Sevilla, Paris St-Germain na Villarreal.

Akiwa anaweka rekodi ya kuchukua ubingwa wa Europa mara nyingi akiwa ameutwaa mara nne, tatu kati ya hizo akiwa na Sevilla.

Chanzo: Mwanaspoti