Juzi usiku timu ya Yanga ilikuwa Ikulu, Jijini Dar es Salaam katika hafla maalumu ya kuwapongeza kwa kushika nafasi ya pili kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyoandaliwa na Rais wa Nchi, Dk Samia Suluhu lakini kubwa zaidi ni hatma ya mshambuliaji hatari wa timu hiyo, Mkongomani Fiston Mayele kuendelea kusalia kikosini hapo.
Licha ya Yanga kushinda 1-0, ugenini juzi Jumamosi pale mjini Alger, Algeria, ilishindwa kubeba ubingwa wa michuano hiyo kwa kigezo cha bao la ugenini na ndoo hiyo kwenda kwa wenyeji USM Alger baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2, lakini waarabu hao wakatwaa taji hilo kwa faida ya mabao mawili ya ugenini iliyoyapata katika fainali ya kwanza iliyopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa Mei 28 mwaka huu na Yanga kufungwa nyumbani 2-1
Ukiachana na machungu ya kukosa ubingwa iliyonayo Yanga lakini kwa sasa pia ipo kwenye wasiwasi wa kuondokewa na baadhi ya nyota wake ambao klabu mbamlimbali kubwa Afrika zimeonekana kuvutiwa nao akiwemo kocha mkuu wa chama hilo, Nasreddine Nabi lakini kubwa zaidi ni vigogo wa Afrika kumtaka Mayele kwa gharama yeyote jambo ambalo huenda likawa gumu kwa Yanga kumzuia kuondoka mwisho wa msimu.
Ubora aliouonyesha Mayele msimu huuakifunga mabao saba na kutoa asisti tatu kwenye Kombe la Shirikisho na kuibuka mfungaji bora wa mashindano hayo sambamba na kuongoza orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Bara akiwa amechika na nyavu mara 16 hadi sasa ni moja ya sababu zilizowazivutia timu za Zamalek ya Misri, ambao ni mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, pia wakitwaa mara moja Kombe la Shirikisho Afrika.
Wengine walio tayari kukaa kwenye meza moja ya mazungumzo na Yanga ili kumng'oa Mayele Jangwani ni Mabingwa mara nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Esperance Sportive de Tunis, ya Tunisia sambamba na Kaizer Chiefs kutoka Afrika Kusini.
Hata hivyo tumepenyezewa na moja ya watu wa karibu wa Mayele kuwa staa huyo tayari anajipanga na maisha mapya ndani ya Yanga akiamini ni muda sahihi wa yeye kutafuta malisho mapya.
"Mayele sidhani kama atabaki Yanga na viongozi wa timu hiyo wanajua hilo, kwa sasa anamalizia msimu kisha ataamua kwa maana ofa alizowekewa na timu hizo ni kubwa sana na wako tayari kumalizana na Yanga.
"Kwa upande wa mchezaji hata yeye anaamini ni muda wa kuondoka Yanga kwani tayari amewatumikia na kuwapa mafanikio makubwa na sasa anataka kutafuta changamoto mpya na hilo ndilo lipo akilini kwake kwa sasa," kilieleza chanzo chetu.
Katika namna nyingine inafahamika kuwa pamoja na Mayele kuwa na shauku ya kupata changamoto mpya lakini pia wasimamizi wake sambamba na marafiki zake wa karibu akiwemo, kocha wa Al Hilal Omdurman, ya Sudan Florent Ibenge ni miongoni mwa watu wanayemsukuma kuondoka Yanga na wapo bega kwa bega kwenye kumtafutia timu nyingine bora zaidi.
"Hizo tatu ni baadhi ya timu ambazo zinamuhitaji lakini ana ofa nyingi na nyingine siwezi kuzitaja. Nyuma yake kuna watu wanasuka mipango yote na siku si nyingi mtaona anaenda wapi na atakuwa miongoni mwa wachezaji wenye thamani kubwa Afrika." kilieleza chanzo chetu.
Kwa upande wa uongozi wa Yanga, Makamu wa Rais wa timu hiyo, Arafat Haji kupitia moja ya mahojiano yake aliyoyafanya na gazeti hili siku chache zilizopita alisema bado wanamuhitaji Mayele na watajitahidi kumboreshea maslahi ili asiondoke.
"Kila timu kwa sasa inahitaji kuwa na mshambuliaji kama Mayele, yuko kwenye mkiwango bora na kwa bahati nzuri bado tuna mkataba naye. Tunajua wapo wanaomtaka lakini na sisi bado tunamuhitaji na tutajitahidi kumboreshea maslahi kuhakikisha haondoki," alisema Arafat.
Kama mambo yatazidi kwenda kama yalivyopangwa kwa upande wa Mayele basi huenda akawa amebakiza mechi tatu tu ndani ya Yanga ambazo ni mbili za kuhitimisha Ligi dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons ambapo tayari Yanga imetwaa ubingwa, na nyingine moja ni ile ya fainali ya Kombe la TFF (ASFC), itakayopigwa Juni 12, mwaka huu kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Hata hivyo, juzi Rais wa Yanga, Hersi Said akizungumzia kuhusu usajili wa Mayele alisema: "Mayele ni mchezaji bora na ninafurahia kuona anahusishwa na timu nyingine, hii inaonyesha kuwa Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wakubwa.
"Kama atakuwa anataka kuondoka, tutaangalia vitu vitatu, moja tutataka kumbakiza, mbili tutaangalia bei nzuri, tatu ni nani atachukua nafasi yake."
Mayele alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu wa 2021/2022 kwa Mkataba wa miaka miwili, na baadae kusaini mkataba mwingine wa miaka miwili ambao utamuweka kikosini hapo hadi mwaka 2024 hivyo timu yeyote itakayomtaka italazimika kununua mkataba huo na Zamalek, Esperance na Kaizer wapo tayari kufanya hivyo.