Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vigogo FIFA, CAF waiteka Dar

Infantino, Motsepe Vigogo FIFA, CAF waiteka Dar

Tue, 17 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ugeni wa viongozi wa soka wapatao 250 kutoka maeneo tofauti duniani unatarajiwa kuanza kuingia leo Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki tukio la uzinduzi wa mashindano ya Ligi ya Mpira wa Miguu Afrika (AFL) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Oktoba 20 litakalohusisha mechi baina ya Simba na Al Ahly.

Msafara huo unaoongozwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa), Gianni Infantino na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), Patrice Motsepe utahusisha wakuu wa idara mbalimbali za mashirikisho hayo, maraisi wa vyama na mashirikisho ya soka kwa nchi zote Afrika pamoja na marais waalikwa wa mashirikisho ya mabara mengine.

Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Ally Mayay alisema Tanzania ipo tayari kuupokea ugeni huo mkubwa ambao utashiriki sherehe za uzinduzi huo

"Marais wote wa vyama na mashirikisho ya soka Afrika watakuwepo, sekretarieti ya Caf itakuwepo. Maofisa wakubwa wa Fifa watakuwepo hapa hivyo ni msafara wa zaidi ya watu 200 utakuwepo hapa wameshaombewa vibali. Kwa hiyo serikali imeshafanya maombi katika hoteli zote kubwa na zimeshajaa.

"Tunategemea kuwa na shughuli kubwa sana ambayo imebeba watu wakubwa katika mpira wa miguu duniani hivyo ni faraja na fahari kwa taifa kupokea ujumbe mkubwa kama huo," alisema Ally Mayay.

Mayay alisema kuwa maandalizi ya msingi kwa ajili ya kupokea ugeni huo na uzinduzi wenyewe ya mashindano hayo kwa asilimia kubwa yamekamilika na kinachosubiriwa kwa sasa ni ujio wa viongozi hao pamoja na tukio lenyewe.

Mbali na ujio wa wageni hao, pia wapinzani wa Simba katika mechi hiyo ya keshokutwa, Al Ahly wanatarajiwa kuingia leo.

Mashindano ya AFL yanafanyika kwa mara ya kwanza ambapo bingwa atavuna kitita cha Dola 4 milioni huku mshindi wa pili akipata Dola 3 milioni na kiasi cha Dola 1.7 milioni kitaenda kwa kila timu itakayoishia nusu fainali.

Timu ambayo itaishia robo fainali, itapata kifuta jasho cha Dola 1 milioni.

Benjamin Mkapa kuzoa noti

Katika hatua nyingine Serikali itavuna kiasi cha Sh 80 milioni kutoka klabu za TP Mazembe na Al Hilal ikiwa zitaamua kuutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kwa mechi zao za kimataifa kuanzia baadaye mwezi huu.

Mapema jana Esperance ya Tunisia ilitangaza kupitia katika kurasa zake za mitandao ya kijamii kuwa mchezo wake wa ugenini wa mashindano ya African Football League (AFL) dhidi ya TP Mazembe utachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa badala ya ule wa TP Mazembe Lubumbashi kutokana na kile kinachodaiwa serikali ya DR Congo kuzuia vifaa vya kurushia matangazo ya mchezo huo kuingia nchini humo.

"Esperance ya Tunisia hivi karibuni imepokea ujumbe kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika ukisema kwamba mechi ya kwanza ya robo fainali ya AFL dhidi ya timu ya TP Mazembe itachezwa Oktoba 22, Dar es Salaam, Tanzania huku mechi ya ugenini ikichezwa Tunisia, Oktoba 25," ilifafanua taarifa hiyo ya Esperance.

Wakati huohuo ripoti kutoka vyanzo mbalimbali vya habari vya Sudan zimetaarifu kwamba miamba ya soka nchini humo imepanga kutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mechi zake za nyumbani katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Gharama za kukodi Uwanja huo kwa mechi moja ya timu ya kigeni ni Sh 20 milioni hivyo kwa mechi moja ya TP Mazembe na tatu za Al Hilal utapata kiasi cha Sh 80 milioni.

Alipotafutwa meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Milinde Mahona alisema hajapata taarifa za ujio wa timu hizo. "Sijapokea taarifa rasmi hata Mimi naona tu kwenye mitandao, nasubiri taarifa rasmi kutoka kwa wakubwa wangu," alisema Maona.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live