Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka nchini Italia SSC Napoli na Timu ya Taifa ya Nigeria, Victor Osimhen amesema afadhali kucheza Ligi Kuu ya Soka Marekani (MLS), kuliko kuelekeka Ligi ya Saudi Arabia.
Osimhen mwenye umri wa miaka 24, alikuwa na ofa nono kutoka kwa klabu ya Saudi Arabia ya Al Hilal msimu huu wa joto ambayo iliripotiwa kukataliwa na SSC Napoli.
“Nina furaha nikiwa SSC Napoli,” alisema Osimhen katika mahojiano yake na Twitch.
“Watu hawajui jinsi ilivyo ngumu kucheza Serie A. Kwa mtazamo wa kimbinu na kimwili, ni moja ya ligi ngumu zaidi kucheza.”
Alipoulizwa kama angependelea kucheza MLS au Saudi Pro League ikiwa atapewa ofa nzuri, Osimhen alisema: “Nitachagua kucheza Marekani.” Hata hivyo, Osimhen aliisifu Ligi ya Saudi Pro League.
Tangu kuwasili kwa Cristiano Ronaldo katika klabu ya Al Nassr Januari 2023, Ligi ya Saudia imevutia baadhi ya wachezaji wenye majina makubwa wakiwamo mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or 2022, Karim Benzema na mshambuliaji wa Brazil, Neymar Jr.
Msimu uliopita klabu za Saudi zilitumia karibu Dola Bilioni Moja kupata wachezaji 94 kutoka katika Ligi Kuu mbalimbali za Ulaya.
“Wanajaribu kukuza ligi yao, ambayo ni nzuri,” aliongeza Osimhen ambaye sasa anatajwa kuwindwa na Tottenham Spurs, Liverpool na Chelsea.
” Ronaldo bora wa wakati wote amekwenda huko. Kwa sababu ya ushawishi wake Ronaldo amevutia wachezaji wengi wenye vipaji pia kwenda huko. Kwa hiyo kwangu ni nzuri sana, wanajaribu kujenga ligi yao kuwa bora zaidi. Kwangu mimi wanafanya jambo la kuvutia.”
Osimhen bado hajafanya uamuzi kuhusu mustakabali wake: Licha ya miezi kadhaa ya mazungumzo ya kurefusha mkataba, mchezaji huyo bado hajaweka wazi juu ya mkataba mpya na makubaliano yake ya sasa yanamalizika ifikapo Juni, 2025.
SSC Napoli bado wana matumaini Osimhen atasaini mkataba mpya licha ya klabu hiyo kudai mchezaji huyo ana “mawazo ya pili” kuhusu kuendelea kuitumikia klabu hiyo baada ya mwaka 2025.
Osimhen, ambaye alijiunga na SSC Napoli msimu wa joto wa 2020 akitokea Lille, alifunga mabao 31 msimu uliopita na kuwasaidia kushinda taji la Serie A kwa mara ya kwanza baada ya miaka 33.