Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vichapo 10 vizito kuwahi kutokea kwenye soka

Vichapo Pic Data Vichapo 10 vizito kuwahi kutokea kwenye soka

Sun, 31 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

LONDON, ENGLAND. KUNA wakati soka huwa na matokeo ya kustaajabisha na kuumiza mioyo ya mashabiki wanaoshabikia timu zao ambazo wanazipenda.

Wiki iliopita ilikuwa mbaya kwa mashabiki wa Manchester United baada ya timu yao kupokea kichapo cha mabao 5-0 ilipomenyana na mahasimu wao, Liverpool, kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.

Kipigo hicho kizito kiliwashtua mashabiki wengi wanaoshabikia timu za soka Ulaya na pengine na duniani kwa ujumla hasa kutokana na uzito wa mechi yenyewe.

Mbali na kipigo hicho kizito kwa Man United, mambo sio shwari ndani ya viunga vya Old Trafford kutokana na ukweli kwamba kocha anayeinoa Ole Gunnar Solskjaer amekalia kuti kavu na mabosi wa timu hiyo inadaiwa wanafikiria kumfuta kazi.

Mbali na Man United kupokea kichapo kizito, Bayern Munich ilikutana na fedheha kama hiyo ikikubali kubamizwa mabao 5-0 ilipomenyana na Borussia Mönchengladbach kwenye michuano ya Kombe la Ujerumani.

Bayern haikuwahi kufungwa mabao 5-0 tangu 1978, lakini miamba hiyo ya soka ilikutana na mvua ya mabao dhidi ya timu hiyo na kutolewa katika mashindano hayo.

Hivi hapa vipigo vingine vya kushtukiza kuwahi kutokea katika mashindano ya soka barani Ulaya.

Barcelona 5-0 Real Madrid

Kipigo hicho kizito alichowahi kukipata Kocha Jose Mourinho 2010 kilikuwa ni kipindi anainoa Real Madrid. Supastaa Lionel Messi alionyesha kiwango bora kwenye mchezo huo wa La Liga.

Katika mtanange huo Xavi, Pedro, David Villa na Jeffren waling’ara na kuizamisha Los Blancos.

Manchester City 5 - 0 Arsenal

Arsenal ilianza msimu huu wa Ligi Kuu England kwa kusuasua baada ya kupokea vipigo vitatu mfululizo, lakini kipigo ambacho hawatakisahau ni kile cha mabao 5-0 ilipomenyana na Manchester City katika mchezo uliopigwa Agosti 28, huku ikiwa pungufu baada ya Granit Xhaka kulimwa kadi nyekundu.

Real Madrid 2-6 Barcelona

Mwaka 2009 Real Madrid ilipokea kichapo cha mabao 6-2 kutoka kwa Barcelona iliokuwa inanolewa na Pep Guardiola.

Real Madrid ilifungwa mabao hayo kuelekea mbio za kuwania ubingwa La Liga kina Thiery Henry, Lionel Messi, Carles Puyol na Gerard Pique walipokata ngebe za Los Blancos.

Manchester United 1-6 Manchester City

Yalikuwa matokeo mabaya kuwahi kutokea Old Trafford chini ya Sir Alex Ferguson tangu 1955.

Ushindi huo uliisaidia Man City kubeba ndoo ya Ligi Kuu England kwa tofauti ya mabao ya kufungwa dhidi ya Man United.

Liverpool 4-0 Barcelona

Kilikuwa kipigo cha fedheha kwa Barcelona kwenye nusu fainali ya pili Ligi ya Mabingwa Ulaya 2019 katika Uwanja wa Anfield.

Liverpool ilipindua matokeo baada ya awali kupokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Barcelona huko Camp Nou.

Manchester United 8-2 Arsenal

Arsene Wenger alipokea kichapo hicho bila ya mabeki wake tegemeo ambao walipata majeraha kuelekea mchezo huo.

Carl Jenkinson, Johan Djourou, Laurent Koscielny, na Armand Traoré walipewa nafasi ya kucheza mechi hiyo ya Ligi Kuu England kutokana majeruhi hao kuwa nje.

Ikumbukwe Wenger alikuwa na kikosi dhaifu kuwahi kutokea 2011 wakati Man United ikianza msimu kwa kishindo.

Mastaa kama Robin Van Persie, Theo Walcott, Alex Song, Tomas Rosicky na Andriy Arshavin walikuwa pekee tegemeo kwa Wenger kipindi hicho.

Barcelona 2-8 Bayern Munich

Ulikuwa ni mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uliofanyika msimu wa 2019-2020 katika Uwanja wa Estadio da Luz jijini Lisbon, Ureno.

Miamba hiyo ya Hispania iliweka rekodi mbovu kuruhusu mabao mengi tangu ilipofanya hivyo 1946 kwenye mashindano ya Copa la Generalisimo dhidi ya Sevilla.

Stoke City 6-1 Liverpool

Ulikuwa msimu ambao Liverpool ilikaribia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England 2015.

Vilevile mechi hiyo ya Ligi Kuu England ilikuwa ya mwisho kwa nahodha Steven Gerrard ambaye alistaafu soka baadaye.

Mbali na hayo, Liverpool iliweka rekodi mbovu ya kuruhusu mabao mengi tangu ilipofanya hivyo miaka 52 iliyopita.

Chelsea 6-0 Arsenal

Wenger hakuwahi kumfunga Jose Mourinho katika Ligi Kuu England, rekodi ambayo ni mbaya kwa Mfaransa huyo dhidi ya kocha mwenzake mkongwe. Mfaransa huyo kila alipokutana na Mourinho alipokea kichapo jambo ambalo lilimnyima usingizi.

Msimu wa 2013-2014 Wenger alipokea kichapo hicho kizito huku mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England zikiyeyuka.

Barcelona 6-1 PSG

PSG iliweka historia mbovu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuondoshwa na miamba hiyo kutoka Camp Nou ikiwa chini ya kocha Unai Emery 2019. PSG ilipata ushindi wa kwanza hatua ya 16 bora kwa mabao 4-0. Hata hivyo, Barcelona ilipindua matokeo katika Uwanja wa Camp Nou na kuichapa kwa mabao 6-1.

Tottenham 2-7 Bayern Munich

Tottenham Hotspur haitasahau kipigo hicho kizito ilichokipata kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ilipokuwa ikinolewa na Mauricio Pochettino, 2019.

KochaPochettino alikalia kuti kavu baada ya kudumu Tottenham kwa muda wa miaka mitano. Mbaya zaidi supastaa Serge Gnabry alifunga mabao manne peke yake kwenye mtanange huo.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz