Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Varane, Kanoute wampa jeuri kocha

Pjimage (50) Kiungo wa Simba SC, Sadio Kanoute

Tue, 26 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Licha ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabigwa Afrika na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa faida ya bao la ugenini baada ya kulala 3-1, Simba sasa imeelekeza nguvu zake kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu Bara huku wachezaji Henock Inonga ‘Varane’ na Sadio Kanoute wakimpa jeuri kocha wa chama hilo, Didier Gomes.

Kipigo cha hicho kilifanya matokeo ya jumla kuwa 3-3 baada ya awali Simba kushinda 2-0 kule Botswana, lakini Jwaneng wamesonga mbele kutokana na faida ya kufunga mabao mengi zaidi ya ugenini.

Simba sasa imeangukia kwenye Kombe la Shirikisho na itarejea kwenye Ligi Kuu Bara kujaribu kutwaa taji lao la tano mfululizo. Nyota wawili waliosajiliwa hivi karibuni, Inonga na Kanoute wameonekana kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha Simba tofauti na wengine tisa ambao bado wapo kwenye programu maalumu na mdogo mdogo wataingia kikosini.

Wachezaji hao ni Peter Banda, AbdulSamad Kassim, Duncan Nyoni, Pape Sakho, Jimmyson Mwanuke, Kibu Denis, Yusuph Mhilu, Israel Mwenda na kipa Jeremiah Kisubi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gomes alifunguka kuhusu nyota wake wawili hao huku akitamba kuwa uwezo wao ni mkubwa na utaisaidia Simba kwenye michuano inayoshiriki.

“Wachezaji wote wapya uwezo wao ni mkubwa lakini mechi inawahitaji 16 tu na 11 ndio waanze hivyo hauwezi kuwapanga wote bali utachagua wachache kulingana na mchezo husika,” alisema Gomes na kuongeza;

“Kanoute na Henock wamepata nafasi kutokana na uhitaji wa mechi, mpira ni mipango na wao wameweza kufanya vizuri katika mipango ya mechi hizi ndio na ubora wao umeonekana.

“Wako vizuri na wataisaidia timu kwenye mashindano tunayoshiriki. Wengine nao wanakuja kwa kasi hivyo natarajia kuwa na machaguo mengi katika mechi zijazo kwani mtu kama Kibu, Duncan, Banda, Israel na Mhilu nao wako tayari,” amesema Gomes.

Kiungo wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Athuman Iddi ‘Chuji’ naye aliwachambua wachezaji hao kwa kusema.

“Wote nimewaona ni wachezaji wazuri, Varane ni kiongozi,” amesema Chuji.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz