Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Van de Beek atimkia Ujerumani

Donny Van De Beek Kiungo wa kati wa Manchester United, Donny van de Beek

Thu, 4 Jan 2024 Chanzo: Dar24

Kiungo wa kati wa Manchester United, Donny van de Beek, amekamilisha uhamisho wa mkopo kwenda Eintracht Frankfurt kwa mujibu wa ESPN.

Kiungo huyo amejiunga na timu hiyo ya Ligi Kuu Ujerumani, Bundesliga, hadi mwishoni mwa msimu huu.

Frankfurt itailipa United ada ndogo ya mkopo na kugharamia sehemu kubwa ya mshahara wa Van de Beek.

Pia kuna chaguo la kumnunua lililojumuishwa katika makubaliano yaliyowekwa kwa euro milioni 11 pamoja na euro milioni tatu katika nyongeza zinazowezekana.

Van de Beek amevumilia hali ya kufadhaisha kutokana na uhamisho wake wa Pauni Milioni 40 kutoka Ajax mwaka 2020.

Amecheza mara mbili pekee msimu huu na ameichezea United mechi 12 katika mashindano yote tangu kuanza kwa msimu wa 2022-23.

Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Uholanzi alitumia kipindi cha pili cha msimu wa 2021-22 kwa mkopo akiwa Everton, lakini alicheza mechi saba pekee.

Alifika Old Trafford akitoka kuisaidia Ajax kufika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya mwaka 2019 chini ya kocha wa sasa wa United, Erik ten Hag.

Alitajwa kwenye orodha ya walioteuliwa kuwa mchezaji bora wa Ballon d’or mwaka 2019, lakini amecheza mechi sita tu za Ligi Kuu England ndani ya miaka mitatu na nusu akiwa United. Ana mkataba katika klabu hiyo hadi Juni 2025.

Chanzo: Dar24