Beki na Nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk, ameongezewa adhabu ya kukosa mechi moja dhidi ya Wolves na kupigwa faini ya Pauni 100,000, baada ya kubainika alitumia lugha ya matusi kwa mwamuzi.
Tukio hilo lilitokea katika mchezo wa Premier League wakati Liverpool ikishinda 2-1 dhidi ya Newcastle, Agosti 27, mwaka huu ambapo Van Dijk alitolewa uwanjani kwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea faulo Alexander Isak.
Baada ya kuonyeshwa kadi nyekundi katika mchezo huo, ilifahamika kwamba Van Dijk atakosekana katika mchezo mmoja dhidi ya Aston Villa walioshinda 3-0, kisha akarejea uwanjani dhidi ya Wolves, Septemba 16, mwaka huu.
Lakini baada ya FA kupitia upya tukio lake, imebainika beki huyo alitumia lugha ya matusi kwa mwamuzi, akaongezewa adhabu huku mwenyewe akikiri hilo.
Imebainika kuwa, beki huyo alionekana mwenye hasira baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu ambapo wakati anatoka uwanjani, aliongea maneno mabaya kwa mwamuzi wa kati, John Brookes sambamba na mwamuzi wa akiba, Craig Pawson.
Taarifa iliyotolewa na Chama cha Soka England, ilisomeka hivi: “Virgil van Dijk amefungiwa kwa mechi moja zaidi na faini ya Pauni 100,000 kwa kukiuka Kanuni ya FA E3.1 wakati wa mechi ya Ligi Kuu, Liverpool dhidi ya Newcastle United Jumapili ya Agosti 27.
“Beki huyo alikiri kuwa alifanya kitendo kisichofaa na kutumia maneno ya matusi kwa afisa wa mechi baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 29.”