Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Van Dijk acharuka kisa waamuzi

Capture VVD Van Dijk acharuka kisa waamuzi

Fri, 12 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Beki kisiki wa Liverpool na nahodha wa Uholanzi, Virgil van Dijk amesema waamuzi wanatakiwa kuchukuliwa hatua kutokana na vitendo vyao baada ya kuchukizwa na maamuzi ya mwamuzi wa mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya England, Felix Zwayer.

Katika mchezo huo, Uholanzi ilianza kuongoza kupitia bao la Xavi Simons, kisha England ikasawazisha kwa penalti ya Harry Kane iliyopatikana baada ya VAR kutoa uamuzi.

Wakati mchezo unakaribia kumalizika, England ilipata bao la pili lililofungwa na Ollie Watkins aliyeingia akitokea benchi, kuchukua nafasi ya Kane.

Van Dijk amesema wakati bao hilo linaenda kufungwa Uholanzi walitakiwa wapewe kona, hivyo hakuona kama lilikuwa ni sahihi.

“Huwa wanakosea kidogo kufanya uamuzi na kusababisha kuwe na madhara makubwa, nafikiri wao pia wawe wanawajibika, wanapofanya uamuzi huwa hawaji kwenye vyombo vya habari na kusema kwa sababu gani kama ilivyo sisi wachezaji pale tunapokosea.”

Alisema beki huyo na kuongeza mbali ya uamuzi wa mwamuzi, wao pia kama wachezaji walikuwa na makosa ndiyo sababu walipoteza mechi.

“Mchezo umemalizika na tumepoteza, ni ngumu sana kukubaliana na uhalisia lakini huu umekuwa ni mwaka mgumu kwetu, tulikuwa na ndoto kubwa ambazo tulidhani tungezitimiza.”

England ilipata penalti baada ya Denzel Dumfries kumfanyia faulo Kane alipokuwa anapiga mpira kwenda lango la Uholanzi jambo ambalo wachambuzi na mashabiki wengi hawakukubaliana nalo na wanaamini hakukuwa na faulo yoyote.

Vile vile bao la pili inaaminika John Stones aliutoa mpira nje wakati anaokoa krosi na ilitakiwa iwe kona lakini mwamuzi alitafsiri mpira umetoka na uanzishwe na kipa na England ikaanzisha haraka kisha ikafunga.

Chanzo: Mwanaspoti