Mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu Bara, Geita Gold iliwapoteza wakali wa mabao, klabu hiyo msimu huu ilifanya maboresho ya kikosi chao na miongoni mwa majembe mapya kwenye safu ya ushambuliaji ni Velentino Mashaka aliyekuwa akikipiga Ruvu Shooting.
Geita iliwapoteza mastaa watatu wenye uwezo wa kufunga mabao ambao ni George Mpole anayekipiga DR Congo, Saido Ntibanzonkiza yupo Simba na Dany Lyanga.
Mashaka tayari ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa klabu hiyo Oktoba, akiwa ni mchezaji wa pili kubeba tuzo hiyo baada ya mkongwe, Kelvin Yondani kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa Septemba.
Mashaka anaongoza kikosini kwa mabao akiwa ametupia mawili katika mechi 11 za timu yake, akifuatiwa na Edmund John, Elias Maguli, Mahamud na Tariq Kiakala wenye bao moja kila mmoja.
Mabao yote mawili ameyafunga kwenye Uwanja wa Nyankumbu dhidi ya KMC na Namungo, pia amefunga mabao matatu katika mechi tano za kirafiki.
Katika mechi 11 za ligi msimu huu, ameanza mechi sita mfululizo na kati ya hizo alizoanza ni moja pekee (dhidi ya KMC) ambayo timu yake ilipoteza, mechi nyingine tano ilishinda mbili na sare tatu.
Mashaka hakuanza michezo mitano ya mwanzo dhidi ya Ihefu, Mashujaa, Kagera Sugar, Yanga na Mtibwa Sugar ambayo timu yake, ilishinda moja, sare moja na kupoteza tatu.
Katika mahojiano maalumu yaliyofanya na Mwanaspoti pamoja na mshambuliaji huyo, amefunguka mambo mengi ikiwemo kiwango chake, malengo yake, bao lake la kwanza ligi ahadi kwa mashabiki wa timu yake.
KILOMBERO, AZAM ZAMUIBUA
Mashaka ni mtoto wa pili kwenye familia ya watoto watatu ya mzee Mashaka Kusengama wa Mbagala, Dar es Salaam, anasema licha ya kuanzia katika akademi ya Kilombero Soccer lakini kipaji chake kimekuzwa na kuonekana zaidi akademi ya Azam.
“Safari yangu ya mpira ilianzia kituo cha Kilombero Soccer kilichopo Morogoro kuanzia 2016 hadi 2018 ndipo nikapata nafasi ya majaribio kituo cha Azam nikafuzu na kujiunga nao kuanzia 2018 hadi 2021,” anasema Mashaka na kuongeza;
“Nikiwa Azam mwaka 2021 nikapelekwa Transit Camp kwa mkopo niliporejea 2022 nikapandishwa timu ya wakubwa na kukosa namba nikaambiwa nitafute changamoto kwingine, niliomba barua yangu nikaenda majaribio Ruvu Shooting nikapita na kuanza kucheza Ligi Kuu nilifunga mabao matano.”
“Ukiachana na mimi kuna mdogo wangu, anaitwa Izack Mashaka pia hivi karibuni utamwona akicheza timu za vijana, kwa sasa bado yupo mtaani.”
UBORA WAKE
Baada ya kuanza vizuri na Geita Gold msimu huu, Mashaka anasema kujituma mazoezini na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ndiyo silaha kubwa inayombeba, huku akifichua kile ambacho benchi la ufundi lilikibadilisha ndani ya timu na kuanza kupata ushindi baada ya kucheza mechi nane sawa na siku 100 bila kushinda mchezo.
“Kwa upande wangu nashukuru kiwango kimeanza kuja kama nilivyokuwa natarajia, nina imani hadi msimu ukiisha kwa uwezo wa Mungu nitakuwa kwenye wakati mzuri ambao wana Geita pia wanautarajia.”
“Kwa ujumla timu na benchi la ufundi lilikaa na kuona matatizo yote ambayo yanafanya timu ifanye vibaya waliyatatua na sasa unaona timu inaanza kufanya vizuri, ligi ni ngumu na yenye ushindani lakini niwahakikishie mashabiki tutapambana kuifikisha timu kwenye nafasi za juu na kuwapa furaha,” anasema Mashaka.
ANAJIONA MBALI
Mkali huyo wa mabao anasema bado hajaridhika na hapo alipo kwa sasa kwani anatamani kufanya vizuri na kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu kama alivyofanya Mpole msimu wa 2021/22 na kucheza soka la kimataifa.
“Malengo yangu kwanza mimi kama mshambuliaji ni kuwa mfungaji bora pia kufanya vizuri ili msimu ujao nicheze soka la kulipwa, pia kuisaidia timu yangu ya taifa,” anasema mshambuliaji huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi zote za mbele huku akipenda kuvaa jezi namba 35 kwani ndiyo iliyomtambulisha katika soka.
BAO LA KWANZA LIGI KUU
Akizungumzia matukio ya furaha na huzuni ambayo hatayasahau katika safari yake ya soka, Mashaka anasema bao lake la kwanza kufunga Ligi Kuu akiwa na Ruvu Shooting msimu uliopita ndiyo tukio ambalo analikumbuka zaidi na lilimpa furaha kubwa.
“Jambo la furaha ambalo siwezi kusahau kwenye maisha yangu ya mpira ni ile siku ambayo nafunga bao langu la kwanza la Ligi Kuu niliwafunga Mbeya City pale Mbeya nilifurahi sana,” anasema Mashaka na kuongeza;
“Upande wa kusikitisha ni wakati niko Azam Academy kuna siku tulikuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya Yanga U-20 kwa kuwa madaktari wa timu hawakuwepo kocha akatuambia kila mtu achukue mafuta yake ili ajichue mwenyewe misuli yake maana tulifanya mazoezi magumu kipindi kile
“Tukafanya hivyo, mimi pamoja na washambuliaji wenzangu tunapiga stori tukiendelea kujichua misuli kama kocha alivyosema, wakati tukiendelea kocha alikuja pale tulipokuwa ilikuwa usiku alivyoniona akaniambia mbele ya wenzangu na wewe unajichua unakwenda kucheza mechi gani, baadae nikatoka nikaenda jukwaani usiku ule nikalia sana.”
BOCCO, MAGULI HATARI
Mashaka anakiri ligi msimu huu ni ngumu na yenye ushindani huku wachezaji wanaomvutia zaidi na anajifunza kwao ni washambuliaji John Bocco (Simba) na Elias Maguli (Geita Gold).
“Katika ligi yetu nawakubali wachezaji wote, ila nitoe nafasi hii kwa wakongwe ninaowakubali mbali na hao wawili, pia kuna Kelvin Yondani na Fulzulu Maganga, hao ndiyo watu ambao huwa naongea nao sana na wananipa ushauri,” anasema Mashaka ambaye nje ya Bongo anawakubali Christiano Ronaldo, Marcus Rashford na Dimitar Babatov.