Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Marefa watibua posho zao zatikisa, wengine wajitoa

Video Archive
Mon, 10 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

SIKU moja tu baada ya sakata la tuhuma za kuwepo kwa hewa chafu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kuibuka upya kwa uongozi wa Uwanja wa Taifa, kusema watakuja kuzitumia kamera za usalama kuwafichua wahusika, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nalo limejitosa kwenye sakata hilo.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema jana jijini Dar es Salaam jambo hilo linaloendelea wanalifanyia kazi kwa ukaribu kwani, limekuwa likiharibu taswira ya soka la Tanzania.

Kidao alisema matukio ya timu za Ligi Kuu kuhusishwa kufanya vitu vya ovyo kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wanayafuatilia kupitia kamera kama walivyosema wamiliki wa uwanja huo na wakigundua lolote hawatasita kuwachukulia hatua wahusika.

“Uzuri viwanja vyote ambavyo vinalalamikiwa kuna kamera, hivyo tutafuatilia na kama tukikuta matukio hayo, basi timu mwenyeji itachukuliwa hatua au kama ni watu wanafanya,” alisema Kidao.

Aliongeza, hata kama watu wanaongea bila kuwa na ushahidi, pia watachukuliwa hatua kwani hawapaswi kuongea bila kuwa na ushahidi.

Akizungumzia upande wa uwanja, alisema anachotambua hakuna timu inayomiliki uwanja katika viwanja vinavyolalamikiwa zaidi ya wote kukabidhiwa funguo asubuhi, hivyo matukio kama hayo lazima yafuatiliwe kwa umakini.

Pia Soma

Advertisement
“Sio mpira tu wa nchi unaoharibiwa, bali hadi taswira ya nchi inaharibika na hatupo tayari kuona jambo hili likitokea, pia kama watu wanawekewa hivyo vitu inashangaza na nipo katikati, kukataa au kukubali kwa sababu kama unapewa funguo na unakaa humo ndani kuanzia saa kumi na mbili asubuhi mpaka muda wa mechi, mbona hawadhuriki wanaokaa? Halafu unasema timu imefanyiwa vitendo hivyo halafu uwanjani inafanya vizuri inashangaza kidogo,” alisema Kidao.

Kauli ya Kidao imekuja baada ya makocha wa Yanga, Luc Eymael na Hitimana Thierry wa Namungo kulalamika kuhisi hewa nzito vyumbani na kulamizika kukaa nje kwenye mechi zao dhidi ya Lipuli na Simba, huku mwaka jana kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika AS Vita ya DR Congo waliibua timbwili Uwanja wa Taifa kwa kuvaa viziba pua kabla ya mechi yao na Simba wakidai wamepuliziwa dawa vyumbani.

Katika hatua nyingine Kidao alisema presha iliyopo hivi sasa imewafanya waamuzi saba kwa pamoja waombe kutokuchezesha mechi za hivi karibuni, ikiwa siku chache tangu Kamati ya Saa 72 ya Bodi ya Ligi Kuu kuwafungia waamuzi kadhaa akiwamo Kassim Safishwa aliyepigwa rungu la miaka mitatu.

Kidao alikiri kuna changamoto ya waamuzi kufanya makosa na tayari wameshaanza kuifanyia kazi kuhakikisha wanamaliza matatizo yanayojitokeza katika michezo husika kwa kuwapa darasa waamuzi.

“Makosa yanayofanyika sio Tanzania tu bali ni Afrika nzima, kwa wenzetu wanatumia VAR ambayo inawasaidia na sisi huku hatuna, lakini tunashukuru Azam Tv kwa kuja na wao kujiboresha na sisi kuona vizuri matukio yote na kutolewa maamuzi,” alisema.

“Waamuzi wasaidizi wamekuwa na changamoto kubwa katika kutafsiri sheria ya kuotea, kwa hilo tutakuwa tunawapima afya ya macho waamuzi wetu, pia tutaangalia upya waamuzi watakaokuwa wanachezesha mechi na kutakuwa na chombo maalumu cha kujua historia ya waamuzi kuanzia huko kwenye ngazi za mikoa,” alisema.

Juu ya madai ya waamuzi kudai fedha, Kidao alisema ni kweli inawezekana wakawa wanadai lakini hilo haliwezi kuwafanya wafanye maamuzi mabaya.

“Ligi Kuu ya Vodacom ili uweze kuwalipa waamuzi kwa msimu mmoja unahitaji kuwa na milioni 764, ukitaka kuwalipa makamishna, waamuzi na Asesa ni bilioni 1 na milioni 282, lakini kwenye udhamini tunapewa milioni 426 kwa ajili ya kulipa wote hao, kwa maana yake kuna pengo kubwa, lakini Bodi ya Ligi wanatakiwa kutafuta namna ya kuwalipa waamuzi wa Ligi Kuu, hapo bado kuna Ligi Daraja la Kwanza huko,” alisema.

Aliongeza kwa kusema katika raundi 19 walizocheza mpaka hivi sasa, Bodi ya Ligi wameshalipa raundi 12 huku raundi saba ndio hawajalipa, huku upande wa udhamini wakiwa wametoa kota mbili bado hawajatoa kota ya tatu na nne.

Chanzo: mwananchi.co.tz